“Kwa yakini nyumba ya kwanza iliyowekwa na kwa ajili
ya watu (kufanya ibada) ni ile iliyoko Makka, yenye baraka na uwongozi kwa
ajili ya walimwengu wote, Humo mna Ishara zilizowazi (za kuonesha utukufu wake
na ukongwe wake miongoni mwa hizo ni) mahali alipokuwa akisimama Ibrahim; na
kuwa anayeingia (Nchi hiyo) anakuwa katika Salama; na kuwa Allah
amewawajibishia watu wafanye Hija kwenye Nyumba hiyo; wale wawezao kufunga
safari ya kwenda huko”.
“(Tukawaambia): Na utangaze kwa watu habari za Hija,
watakufikia, (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyekonda
(kwa machofu ya njiani) wakija kutoka katika kila njia ya mbali, ili
washuhudiye manufaa yao na ili wakithirishe kulitaja jina la Allah katika siku
zinazojulikana na fadhila zake juu ya yale aliyowaruzuku, nao ni wanyama wenye
miguu minne, na kuleni katika wanyama hao na mlisheni mwenye shida
aliyefakiri.”
Hija ni nguzo ya tano katika nguzo za Kiislamu na
ndiyo iliyo na vitendo vigumu zaidi kuliko nguzo zote nyingine. Basi unapotaka
kwenda kuhiji na kufanya Umra au kufanya Umra tu ili upate hadhi ya
kujikaribisha na Allah na ujipeleke kwenye upepeo wa Rehema zake na uzunguke
Al-Kaaba yenye kuheshimika na ufanye saayi baina ya Safa na Al-marwaa na kupata
hadhi ya kuzibusu zile sehemu tukufu ambazo amezipitia Mtume Salallahu Alayhi
Wasalam (ametembea juu yake) pamoja na watu wa mwanzo aliosuhubiana nao yaani
Masahaba na waliofuata njia zao, Mataabiin. Na kwa hao ilibadilika hali kutoka giza kwenda kwenye elimu
na kutoka katika Ushirikina kwenda kwenye Tawhiid (kumpwekesha Allah Subhanahu
Wataala ).
Ukitaka kwenda kuhiji au Umra kwa uwezo wa Allah na
Tawfiiq yake basi na ufanye kama ifuatavyo:
Isahihishe niya yako hata iwe kutoka kwako huko ni kwa
kutaka radhi yake Subhanahu Wataala. Wala usimshirikishe pamoja naye mwingine
(kujionesha kwa watu kuwa sasa wewe pia umekuwa Al-Hajji au kwenda huko kwa
kufanya biashara na mengineyo). Unuiye kufanya Umra na kuhiji au kufanya Umra
tu au Kuhiji tu. Kwa hali yoyote inakulazimu utiye niya kabla hujaondoka na
vile vile inakulazimika urudishe haki zote za watu zilizo juu yako. Iwapo
huwezi kuzirudisha kwa wakati huo basi andika karatasi rasmi ya kishariya kuwa
ukipatwa na mauti katika Hija yako hiyo walipwe hao wenye haki zao. Hakikisha
wasiya wako huo utatekelezwa (kwa kuacha kitu kinachofidiya hizo haki na
kumwakilisha mtu madhubuti) kwani mja yuko katika kabdha ya Muumbaji wake
Subhanahu Wataala (wakati wowote akimtaka atamchukua).
Hakuna budi safari yako ima iwe kwa gari au kwa ndege
na kwa hali zote mbili Umra inayoanziwa Dhul huleifa (sasa inaitwa Abyaar Ali)
ni bora zaidi, kuliko kuanzia kwengine kwani inayoanziwa Dhul huleifa inakuwa
mfano wa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kisha ni Mikaati iliyo mbali zaidi
kuliko zote na kila Ihraam ikiwa ndefu inazidi thawabu.
Iwapo utakwenda kwa gari basi nenda moja kwa moja
mpaka Madina Al-Munawarah, ama ukiwa umesafiri kwa ndege na umeteremka Jedah
basi nenda zako moja kwa moja Madina bila ya kuingia Makka.
Ukifika Madina kwa uwezo wake Subhanahu Wataala
ukithirishe kumsalia na kumsalimia Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na uingie
msikiti wa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam unaohishimika baada ya kuweka mizigo
yako hapo mahala ulipofikilia.
Ukiingia msikitini usali rakaa mbili “Tahiyyatul
Masjid” na ukiweza kusali hizo rakaa mbili pamoja na Salaa zote katika asli ya
msikiti alioujenga Mtume Salallahu Alayhi Wasalam fanya bidii usali hapo kwani
nafsi inahisi raha zaidi, lakini hakuna kitu ukisali popote katika Msikiti huo
kwa sababu Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amesema: Kila kilicho wasiliana na
msikiti wake hukumu yake sawa sawa na msikiti wake hata ukafika San’aa. Baada
ya kusali hizo rakaa mbili uwende kwa adabu na unyenyekevu pale lilipo kaburi
la Mtume Salallahu Alayhi Wasalam usimame mbele yake kisha useme:
(السلام عليك يارسول الله السلام عليك يا نبي
الله ورحمة الله وبركاته أشهد أنك رسول الله حقاً وأنك بلغت الرسالة وأديت الأمانة ونصحت الأمة وجاهدت في الله حق جهاده
فجزاك الله عن الإسلام والمسلمين خيراً وآتاك الوسيلة والفضيلة والدرجة العالية
الرفيعة وأرجو يا رسول الله أن أكون من أهل شفاعتك يوم القيامة )
Baada ya hapo utasogea upande wa kulia kidogo, na
utamtolea Salamu Assadiq (Abu Bakr RA) na utasema :
( السلام عليك يا صاحب رسول
الله في الغار ويا خليفته على المسلمين السلام عليك ورحمة الله وبركاته أشهد أنك
خلفت رسول الله وقمت بواجبك ونصحت للأمة فجزاك الله خيراًَ )
Kisha utasogea kuliani kwako
kidogo na utamsalimia Al-Faaruuq (Omar bin Al-Khattaab RA) na useme:
( السلام عليك يا أبا حفص
السلام عليك يا أمير المؤمنين أشهد أنك أمرت بالمعروف ونهيت عن المنكر واجتهدت لأمة محمد نصحاً
وإخلاصا فجزاك الله خيرا )
Baada ya hapo uondoke na tahadhari usiguse kwa mkono
wako kitu au uchezee kitu usije ukajiharibia nafsi yako na madhehebu yako.
Kwani madhehebu ya Ibadhi imesafika wala
haikuchafuliwa na chochote nayo ni kilele katika adabu na wala haichukuwi
mafundisho isipokuwa kwa Allah Subhanahu Wataala na Mtume wake Salallahu Alayhi
Wasalam.
Na ukae huko Madina kama utakavyojaaliwa
(utakavyoweza) na wala hakushurutishwi kukaa muda fulani na ukiwa huko uzidishe
kusali katika msikiti wa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kwani sala moja hapa ni
sawa na sala elfu kwa hiyo usipoteze fursa hiyo. Vile vile utembelee msikiti wa
Quba na usali ndani yake kwani Allah Subhanahu Wataala ameteremsha juu yake
kauli yake katika Qur’ani
tukufu:
التوبة: ١٠٨
“Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa kumcha Mungu
tangu siku ya kwanza (ya kufika Mtume Madina) unastahiki zaidi wewe usimame
humo. Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa. Na Allah anawapenda wajitakasao.”
Wasema wanavyuoni kuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam
aliwauliza watu wa msikiti wa “Quba”: Kwa nini Allah kawasifu? Wakamjibu:
tulikuwa tukifuatishia maji (baada ya kujipangusa kwa ) mawe iwapo tukienda
choo kidogo au kikubwa.
Na inapendelewa kuzuru makaburi ya Mashahidi wa Vita
vya “Uhud” na uwasalimie na uwaombee maghufira. Inataka wakati huo ukumbuke
mapambano yaliyotokeya hapo baina ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na
Washirikina wa Quraish na wengineo Allah Subhanahu Wataala akawashinda ushindi
mbaya. Baada ya kuwafanyiya Waislamu mtihani mara ya kwanza na wakashindwa (na
maadui zao kwa sababu hawakufaulu huo mtihani waliopewa kwa kutofuata amri ya
Mtume Salallahu Alayhi Wasalam) kisha ukarudi ushindi kuwa wao (Waislamu).
Basi ujue kuwa Dini hii haikutufikia kwa urahisi bali
imetufikia kwa juhudi kubwa na jihadi ya tabu na uchungu mkubwa na leo Waislamu
waichezea na wabomoa kile kilichohifadhiwa na wale wenye ikhlasi (basi huu ni
msiba mkubwa sana) إنا لله وإنا اليه راجعون
“Sisi ni wa Allah na kwa
hakika kwake tunarejea”.
Unapoazimia kwenda Makka
Al-Mukarrama ni lazima utakuwa katika hali moja ya hali tatu zifuatazo:
Iwe umekusudia kufanya Umra
kisha uvue Ihram upumzike halafu uvae Ihram ya Hija.
Iwe umekusudia kufanya Hija
peke yake.
Iwe umekusudia kuchanganya
baina ya Haji na Umra kwa Ihram moja.
Hali hizi tatu hazitokei
isipokuwa katika miezi ya Hija nayo kuanzia siku ya mwanzo wa Shawal (Mfungo
Mosi) mpaka siku ya nane ya mwezi wa Dhil Hija (Mfungo tatu) na katika hali
zote tatu ufanye kama ifuatavyo: Uoge kama unavyooga janaba kisha utawadhe tena
uvae nguo mbili, ambazo hazikushonwa moja uifanye kikoi na ya pili uivae juu
ujizungushie mwilini na wala usiziunganishe kwa kuzipiga fundo au kwa shindano
na ziepushe kuguswa na manukato halafu usali rakaa mbili ya “Ihraam” usome
katika rakaa ya mwanzo (baada ya sura Al-Fatihah):
( قل يا أيها الكافرون )
Na katika rakaa ya pili baada
ya Al-Hamdu:
( قل هو الله احد )
Kisha unaweka niya baada kutoa
Salamu useme:
( لبيك اللهم لبيك لبيك لا
شريك لك لبيك إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك)
Na ukiwa mutamattii (yaani
ukiwa katika hali ya kwanza katika zile hali tatu) uzidishe kwa kusema:
( بعمرة تمامها وبلاغها عليك يا الله )
Na ukiwa mufrid (yaani katika
hali ya pili) uzidishe kwa kusema:
( بحجة تمامها وبلاغها
عليك يا الله )
Na ukiwa umechanganya baina ya
Hija na Umra (hali ya tatu): uzidishe kwa kusema:
( بحجة وعمرة تمامهما
وبلاغهما عليك يا الله )
Useme haya mara tatu halafu
uongeze kusema:
( اللهم إني أسألك رضاك والجنة وأعوذ بك من سخطك
والنار لا إله إلا أنت وصلى الله على رسوله سيدنا محمد وآله )
Ufanye haya yote ukifika
“Dhul-Huleifa.” Na ukifanya haya Madina hapana kitu (inafaa).
Ama kuoga ni rahisi kwako na
ni utaratibu kwako kuoga katika nyumba uliofikia huko Madina na uvae nguo ya
Ihram huko huko. Ama kutia niya ya Ihram na kufanya Ihram ni bora kufanya haya
Dhul-Hulaifa ikiwa wewe ni katika mahujjaji wanaosafiri bara, ama ukiwa katika
mahujjaji wanaosafiri angani usiharakishe kutia Ihram mpaka uhakikishe kuwa
umepata okey katika ticket yako kwa sababu ukifanya Ihram nawe hukusafiri
utabakia katika tabu na mashaka (kwani Ihraam ina masharti yake usipoyashika
itakubidi damu yaani uchinje).
Wala haifai kuihalalisha hiyo
Ihraam mpaka umalize vitendo vya Hija au Umra na iwapo utahakikisha usafiri
wako (kwa kupata okey katika booking yako) basi sali rakaa mbili katika kiwanja
cha ndege utakachosafiria na utie Ihram baada ya hizo rakaa (useme: Labbaika
Allahuma Labbaika n.k). Na utawakali kwa Allah, na utahadhari ewe mwenye Ihram
usije ukakata unywele au kucha au kufanya kazi yoyote ambayo inaweza
ikakusababishia kuumia ukatoka damu au usije ukagusa mafuta mazuri au
usijikumbushe jimai kwani mambo haya yote huharibu Ihramu yako na kusabibishia
damu yaani kuchinja mbuzi au kondoo katika ardhi ya Al-haram. Na wala
usighafilike kufanya “Talbiya”
(“Labbeika”…) baina ya wakati na
mwingine bila ya kukazania sana (yaani kufanya
talbiya moja kwa moja) na hakika talbiya ni katika vitendo muhimu sana vya Hija basi
usiikate mpaka utakapoiona Baitul Al-Haram.
Ufikapo Makka Al-Mukarrama
teremka kwanza katika mahala ambapo utafikia ili ushushe mizigo yako (Ipo
nyumba hapo Makka, Bait Ribaat, imeekwa wakfu na baadhi ya watu wema kwa
mafakiri wa Kiibadhi kwa hiyo haifai kwa asiye Muibadhi kukaa ndani yake na
vile vile haifai kwa Muibadhi aliye tajiri kukaa humo kwa sababu kukaa kwao
humo kutaibadilisha wasiya iliyoekwa na mwenye
kuiweka wakfu. Kwa sababu aliemkusudia Allah katika kitendo chake basi
asimwendee kinyume kwa cho chote.)
Ukisha weka mizigo yako jitie
udhu na uwende Masjid Al-Haram, na utakapoiona Al-Kaaba ukate talbiya yako na
useme:
( اللهم إن هذا بيتك وأنا عبدك فأنلني فيه مناي
واغفر ذنبي ووفقني للعمل بطاعتك وصلى الله على سيدنا محمد وآله )
Kisha uende kwenye Hajar
Al-aswad ukilifikia libusu ikiwezekana bila ya kuudhi au kuudhiwa ama sivyo
inakutosha kulishika kwa mkono wako na hata iwapo hukuweza hivyo basi lifanyie
ishara kwa mkono wako kwani Mtume Salallahu Alayhi Wasalam aliliashiria kwa
bakora iliyokuwa mkononi mwake. Kisha uanze kuzunguka Al-Kaaba (Tawaaf) kabla
hujauona mlango (wa kaaba) uzunguke mara saba, na mzunguko mmoja (“shawt”) ni
kutoka Hajar Al-aswad mpaka Hajar Al-aswad. Lazima udhibiti mizinguko yako kwani ikiwa hukuihifadhi inakubidi uirudie
tena upya. Na haitimii tawaaf mpaka uwe na hakika nayo na usome katika
mizunguko yako yote:
( سبحان الله والحمد لله ولا إله إلا الله والله أكبر ولا حول ولا
قوة إلا بالله )
Masahaba radhi za Allah ziwe
juu yao walikuwa hawazidi juu ya maneno hayo. Iwapo utaomba kwa Dua unayoijua
hapana kitu(inafaa) lakini kinachokatazwa ni kushika kitabu cha Dua chenye Dua
ya mzunguko wa kwanza (shawt) na Dua ya
shawt ya pili mpaka shawt ya saba basi hivo ndivyo wafanyavyo wengi katika
mahujjaji wala hawajui kitu gani wanasoma na wana Imani kuwa tawaaf haitimii
isipokuwa kwa kusoma Dua hizo. Na msingi wa kisheria unasema ukiomba Dua
uliokuwa huijui maana yake basi hutakabaliwi (hupokelewi). Twamuomba Allah amchunge
kwa Rehema zake yule anaemkusudia yeye tu na akafanya Ikhlaas kwa ajili yake.
Na kwa hakika inapendelewa
useme upitapo baina ya “Rukni Al-yamaniy” na Hajar Al-aswad useme:
Vile vile inapendelewa upitapo
kwenye Al-Miizaab useme:
( اللهم إني أسألك الراحة عند الموت والعفو عند
الحساب والفوز بالجنة والنجاة من النار )
Na upitapo Rukn Al-yamaaniy
uiguse kwa mkono wako bila ya kuibusu kwani linalobusiwa ni Hajar Al-aswad tu
kwa mujibu wa Sunna. Na umalizapo kuzunguka (Al-Kaaba) mara saba umshukuru
Allah Subhanahu Wataala kwa kukupa tawfiiq (ya kufanya vitendo hivyo vitukufu).
Ikiwa utaweza kusimama kwenye huo mlango (wa Al-Kaaba) na uligusanishe tumbo
lako ukutani na ukamate kwa mkono wako chini ya mlango na umuombe Allah kadiri
utakavyojaaliwa kwani inahimizwa kufanya hivyo. Na Dua iliyo bora zaidi ni
kumuomba Allah akusamehe katika Dunia na Akhera kwani Dua hiyo inakusanya yote.
Aliyemsamehe Allah Subhanahu Wataala katika Dunia yake na Akhera yake ataka
nini zaidi ya hayo?
Kisha sali rakaa mbili nyuma
ya Maqamu Ibrahim na hizo ni rakaa mbili za tawaaf (kuzunguka Al-Kaaba) faridha
na ukiwa huwezi kusali nyuma ya Maqamu Ibrahim kwa sababu ya msongamano wa watu
basi unaweza ukasali mahali po pote katika msikiti huo. Usome katika rakaa mbili
baada ya sura Al-faatihah: Qul Yaa Ayuha lkaafiruun (rakaa ya kwanza) na Qul
Huwa Allahu Ahad (rakaa ya pili). Na umuombe Allah kiasi utakavyojaaliwa. Kisha
unywe maji ya Zam Zam mpaka ushibe maji na ujirushie kichwani kwani ni baraka
na kuifuata Sunna ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam.
Kisha baada ya hayo yote uende
kufanya Saayi (mwendo baina ya Safa na Marwa) uanze na Safa na usome ukipanda
juu ya kilima chake:
( أبدأ بما بدأ الله به )
البقرة: ١٥٨
“Hakika Safa na Marwa
(Majabali mawili yanayofanyiwa ibada ya kusai huko Makka) ni katika alama za
kuadhimisha Dini ya Allah. Basi anayehiji kwenye nyumba hiyo au kufanya Umra,
si kosa kwake kuvizunguka (vilima) hivyo viwili; na anayefanya wema (atalipwa)
kwani Allah ni Mwenye shukurani na Mjuzi (wa kila jambo)”.
Wanavyuoni wamefanya utafiti
katika Aya hii wakasema: kwa sababu gani Allah amesema: “Si kosa kwake
kuvizunguka (vilima hivyo viwili) pamoja ya kuwa tawaaf ni sunna, wakaona kuwa
katika wakati wa ujahiliya yalikuweko masanamu mawili katika vilima viwili
hivyo yaitwa “Asaaf” na “Naailah”. Ulipokuja Uislamu wakaona taabu Waislamu
kufanya Saayi baina ya hiyo milima miwili wasije wakafata mfano wa washirikina. Ndipo ilipoteremka Aya hii
kuwaambia kuwa Ushirikina umeondoka na umetoweka na sasa huu Uislamu katika
nguvu yake na ukubwa wake.
Na upandapo kilima cha Safa
useme:
( لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك
وله الحمد وهو على كل شيء قدير، تائبون آيبون عابدون لربنا حامدون، لا إله إلا الله وحده صدق وعده
ونصر عبده وهزم الأحزاب وحده )
Baada ya kusema hayo uteremke
kuelekea Marwa na ukifika katikati ya bonde na leo hakuna athari ya bonde
isipokuwa imewekwa ishara ya taa za kijani sakafuni inayoonyesha mwanzo wa wadi
na mwisho wa wadi (bonde).
Ukifika mahali hapa kimbia
kidogo kidogo (polepole) kama uwezavyo siyo kupiga mbio sana na useme:
( اللهم اجعل ممشاي هذا كفارة لكل مشي كرهته مني
اللهم إني أسألك العمل بما ترضى والفوز بالأخرى ، اللهم اغفر وارحم وتجاوز عما تعلم )
Na useme katika Saayi yote
kama ulivyosema katika tawaaf na unamalizika mzunguko (shawt) wa kwanza katika
Marwa na inaanza hapo shawt ya pili na vivyo hivyo mpaka zikamilike shawt saba,
unaanza katika Safa na unamalizia katika Marwa, na uelekee Al-Kaaba ukifika
Safa na Marwa.
Mwanamke asipande juu ya
kilima cha Safa wala kilima cha Marwa wala asikimbie baina ya alama mbili (za
kijani) kwani haya yote makhsusi kwa wanaume. Ama mwanamke anatakiwa asimame
chini ya As-Safa na Al-Marwa na atembee mwendo wa kawaida baina ya alama mbili
(za taa ya kijani) kama anavyotembea katika Saayi iliyobakia, na haya yote ni
kwa ajili ya kuhifadhi sitara yake kwani anawajibikiwa kuihifadhi katika hali
zake zote wala hakuruhusiwa kuonesha kitu cho chote katika mapambo yake (sehemu
zake za mwili zinazovutia) katika hali yoyote isipokuwa kuruhusiwa kwake kuacha
wazi uso na mikono miwili katika hali ya Ihram na kuzifunika sehemu hizo katika
nyakati nyinginezo ni bora.
Ukishamaliza kufanya Saayi
(mwendo baina ya Safa na Marwa) ukate nywele lakini ukizinyoa ni bora zaidi. Na
huko kukata nywele ni kupunguza baadhi ya nywele katika kichwa chako. Ama
mwanamke yeye apunguze kadiri ya kidole kimoja au vidole viwili katika ncha ya
nywele zake wala asipunguze zaidi ya hivyo. Mwanamme haruhusiwi kukata au
kupunguza kitu katika ndevu zake kwani kupunguza ndevu ni haramu, kwani haiwi
katika utiifu wa Allah kufanya maasi (huko kukata ndevu). Na bora muhrim akatwe
nywele na asiyekuwa muhrim wako vinyozi hapo nje ya Al-Haram; kisha
ukishanyolewa wewe mwanamme uchukue mkasi umkate mkewo au ndugu yako na
mwanamke amkate mwanamke mwenzake wala asimkate nywele zake mwanamme isipokuwa
akiwa mahrim yake kama baba, ndugu, ami mjomba
wake n.k. Na mpaka hapa imemalizika Umra kwa tawfiki ya Allah na anaejitahidi
hupata tawfiki.
Mwenye kuihalilisha Ihram yake
(Mutamatii) na akawa amepumzika kuingojea Hija huvua ngua zake za Ihram na
hufanya kila alichoharimishiwa katika hali ya Ihram. Ama mwenye kuchanganya
Umra na Hija (Al-Muqrin) hubakia katika Ihram yake (nguo zake za Ihram) kwani
yeye bado ni Muhrim na anaharamishiwa kila alichoharimishiwa Muhrim. Mpaka
itakapofika siku ya nane ya Dhil Hija. Yule aliyejihalilisha na Ihram yake
(Mutamatii) ya Umra sasa anafanya Ihraam ya Hija huko Al-Bat-haa au katika
Masjid Al-Haraam au katika nyumba aliyofikia. Kisha wanaelekea Mahujjaji wote
huko Muna baada ya kupindukia jua na hawatasali Sala ya Adhuhuri na Sala ya
Al-asiri mpaka wafike Muna wazichanganye (jama’an) na wazisali rakaa mbili
mbili (qasraan).
Mwenye kutia niya ya kuhiji tu
(Al-Mufrid) hubakia katika Ihraam yake. Iwapo atafika Makka kabla ya tarehe 8
nane Dhil Hija hatofanya tawaaf (kuzunguka Al-Kaaba) bali atabakia na Ihraam
yake na atasali katika Masjid Al-Haram.
Usiku wa kuamkia tarehe 9 tisa
Dhul Hajji ulale hapo Muna na usali Sala tano hapo (kama tulivyosema kabla kuwa
uchanganye Adhuhuri na Al-Asiri na
kadhalika Al-Maghrib na Al-Ishaa katika
tarehe 8 Dhil Hajji na Sala ya Al-Fajiri mnamo tarehe 9 Dhil Hija). Ufikapo
Muna useme:
( اللهم إن هذه منى وهي مما دللت عليه من
المناسك وأسألك أن تمن علي فيها وفي غيرها بما مننت به على أوليائك وأصفيائك فها
أنا ذا عبدك بين يديك وفي قبضتك وصلى الله على سيدنا محمد )
Na asubuhi ya siku ya tisa
nayo ndiyo siku ya Arafa baada ya kwisha toka jua (sio kabla ya kutoka jua)
uende huko Arafaat na usimame hapo (Wuquuf) na useme:
{اللهم إليك قصدت وإليك صمدت
وما عندك أردت أسألك أن تبارك لي في رزقي وأن تلقيني في عرفات حاجتي وصلى الله على
سيدنا محمد وعلى آله وصحبه وسلم{
Usiwache kusoma talbiya baina
ya wakati na mwingine na baada ya kusali Sala za faridha (usome talbiya) na
ukiona mjumuiko wa watu (vile vile usome talbiyah) kila ukizidisha talbiyah ni
kheri kwako na katika hadithi: (الحج العج والثج) maana yake Hija ni
kupandisha sauti kwa kufanya talbiyah (العج) na kumwaga damu ya mnyama unaemtoa sadaka (الثج) .
Ukifika Arafaat napo ni mahala
panapojulikana kuna sehemu hapo inaitwa “Arina” iko jirani na Arafaat
anaesimama hapo huyo hana Hija (Hija yake imekuwa baatil) basi na watahadhari
wasiojua wasije wakafanya kosa hilo ,
wengi katika wanaowachukua Mahujjaj (Muqawiliin) huwapeleka huko hawajali
kufanya kosa hili kwa hoja ya kukimbia fujo ya watu (iliyoko Arafaat). Hii ni
khiyana na kitu kinachompasa anaekwenda kuhiji aulize na asiwe mjinga ili
ajiepushe na mambo yanayoharibu Hija yake.
Kusimama Arafaat (Wuquuf bi
Arafaat) ni nguzo ya pili ya Hija baada ya Al-Ihraam na ukifika hapo useme:
(اللهم هذه عرفات فاجمع لي
فيها جوامع الخير كله واصرف عني فيها جوامع الشر كله وعرفني فيها ما عرفت أولياءك
وأصفياءك وصلى الله على سيدنا محمد )
Kisha ujitayarishe kwa msimamo
(Wuquuf bi Arafaat) kwanza ule na kisha utawadhe na likishapindukia jua huo
ndio wakati wa Wuquuf umewadia na usali Adhuhuri na Al-Asiri pamoja na kuzifupisha
(jama’an qasraan) Sala ya Jamaa. Halafu usimame kumuomba Allah Subhanahu
Wataala akughufirie madhambi yako na akufutie makosa yako na akutekelezee haja
yako kwani Allah Subhanahu Wataala yu Karimu hamrudishi katika siku hii mwenye
kumuomba kwa Ikhlasi ikiwa hakumuomba Allah haja isiyofaa kuombwa. Na kila
msimamo huo ukiwa wima ni bora zaidi na ikiwa huwezi ukae na ikiwa huwezi ujinyooshe.
Msimamo huko Arafaat maana
yake: Kuomba haja zako kutoka kupindukia kwa jua mpaka kuzama jua. Unatumia
wakati huu wote katika kumtaja (kumkumbuka) Allah, kumuomba, na kunyenyekea
kwake akukubalie maombi yako, uhudhurishe madhambi yako uliyoyafanya
(uyakumbuke na umwombe Subhanahu Wataala akughufurie) na ujihisabu nafsi yako
na unyenyekee kwake Subhanahu Wataala akutakabalie na uzidishe kumdhukuru Allah
Subhanahu Wataala kwa kusema:
( لا إله إلا الله وحده لا شريك له )
Kwani hiyo ni katika Dua iliyo
bora kuliko zote kama ilivyokuja katika hadithi:
( أفضل ما قلته وقال
النبيون قبلي لا إله إلا الله وحده لا شريك له )
Bora ya niliyoyasema mimi na
waliyoyasema Manabii kabla yangu ni:
( لا إله إلا الله وحده لا
شريك له )
Na wala usijishughulishe na
lolote katika mambo ya Dunia isipokuwa lenye dharura kwani hiyo ni fursa ambayo
haipotezwi na wala hairejesheki. Na tawfiiq iko katika mkono wa Allah Subhanahu
Wataala .
Na utahadhari usije ukaondoka
mahala pako kabla halijatua jua ama baada ya kwisha tua uondoke pamoja na
mahujjaji kuelekea Muzdalifah nayo vile vile huitwa Jamaa ukifika hapo useme:
( اللهم إن هذه جمع، فاجمع لي فيها جوامع الخير كله )
Usiwache kufanya talbiya mpaka
upige mawe jamrat Al-Aqabah katika siku ya pili, na usisali Al-Maghrib na
Al-Ishaa kabla hujafika Jamaa na hivyo ndivyo katika Sunna na ukifika hata lau
katika mwisho wa usiku wakati huo ndio usali Al-Maghrib na Al-Ishaa pamoja. Na
ulale hapo na umdhukuru Allah Subhanahu Wataala kama ilivyotuelekeza Qurani
Tukufu.
البقرة: ١٩٨
“Na mtakaporudi kutoka Arafat
mtajeni Allah penye Mash’aril Haraam na mkumbukeni kama
alivyokuongozeni.”
Na Mash’aril Haraam ndio
Muzdalifah na amesema Allah Subhanahu Wataala :
البقرة: ٢٠٠
“Na mwishapo kuzitimiliza
ibada zenu (za Hija), basi mtajeni Allah kama mlivyokuwa mkiwataja wazee wenu;
bali mtajeni zaidi (Allah)”.
Waarabu walikuwa
wakijifakharisha kwa mababa zao, kwani walikuwa wakiwataja sana
basi akawaamrisha Allah Subhanahu Wataala wamtaje yeye badala ya kuwataja
mababa zao na hiyo ndiyo kheri kwa mwisho wao (khatima yao ).
Baada ya kusali Sala ya
Al-fajiri hapo Muzdalifa uharakishe kuondoka kuelekea Muna na hapo mashariki ya
Muna kuna bonde (wadi) linaloitwa “Wadi Muhassar”. Limeitwa hivyo kwa sababu
yule tembo wa Abraha alipokuja kutaka kulivunja Al-Kaaba alishindwa kuendelea
asijue pa kwenda akakaa na kila alivyojaribu mwenyewe kumsimamisha ili ende
upande wa Al-Kaaba alishindwa na alipokuwa amuelekeza ende upande usiokuwa wa
Al-Kaaba alikuwa anakwenda lakini akimuelekeza upande wa Al-Kaaba anakataa
kwenda na hukaa chini. Pia huitwa bonde hilo “Wadi Annaar” (bonde la Moto ) na lazima anaehiji
kulivuka bonde hilo
kabla ya kutoka jua siku ya kumi ya Hija.
Kitu cha kwanza unachokifanya
katika siku hii huko Mina ni kutupa vijiwe kwenye Jamrat Al-Aqaba na vile vile
huitwa Jamrat Al-Kubra nalo liko karibu zaidi ya Makka kuliko hizo jamaraat
mbili nyingine. Unalitupia vijiwe saba vidogo, ukubwa wake hivyo vijiwe kama
kunazi na visipindukie ukubwa huo wala usitupe kisichokuwa jiwe kama
wanavyofanya wengi miongoni mwa wajinga watupa viatu au mbao na wayapandia hayo
majamaraat na kuyakanyaga kwa miguu yao na kuyapiga kwa mikono yao wengine
wayarukia ili wayang’ate, wakiamini kuwa hilo jamarat ndilo shetani na kuwa ati
wakimfanyia hivyo huwa wanamdhalilisha. Hawajui masikini kuwa shetani ndiye
aliyewapanda wao na kuwa yeye anafurahika na vitendo vyao hivyo kwa sababu ni
kinyume na sheria na kinyume na aliyoyaleta Mtume Salallahu Alayhi Wasalam. Na
hapa mahala anapopakusudia shetani, Allah amdhililishe na awahidi Waislamu
wafanye yanayomridhisha na watende yenye utiifu kwa Mola wao Subhanahu Wataala.
Katika masharti ya kutupa
hivyo vijiwe ni kuwa ulione hilo jiwe wakati
linapopiga hilo
Jamarat na upige takbira kwa kila kijiwe unachokitupa useme:
( الله أكبر ولله الحمد ، اللهم هذه حصياتي وأنت أحصى لهن مني
فتقبلهن مني واجعلهن في الآخرة ذخرا لي وصلى الله على رسوله سيدنا محمد وعلى آله
وصحبه وسلم
Baada ya hapa ukiwa ni
miongoni mwa wafanyao Hija ya Tamattuu (waliotia Ihram ya Umra kisha wakaitoa
na kupumzika na ukawafaa wakati huo wa mapumziko kufanya mambo mengine ya
kawaida halafu wakatia Ihram ya Hija ukiwadia wakati wake) utakwenda huko
wanakouzwa wanyama ununue mbuzi au kondoo kisha umchinje au ushirikiane na watu
sita (muwe jumla saba) mchinje n’gombe au ngamia kwani wanyama wawili hawa
watosheleza watu saba. Baada ya hapo unyoe nywele zako au upunguze (ukate
nywele) na kunyoa ni bora zaidi kwa mujibu ya hadithi ya Mtume Salallahu Alayhi
Wasalam :
( رحم الله المحلقين قيل والمقصرين قال رحم الله المحلقين قيل
والمقصرين قال رحم الله المحلقين وفي الرابعة قال والمقصرين )
"Allah amewarehemu wanaonyoa" akaambiwa: Je
wanaopunguza akasema "Allah amewarehemu wanaonyoa" akaambiwa: Je
wanaopunguza akasema "Allah amewarehemu wanaonyoa" na katika mara ya
nne ndio akasema: "na wanaopunguza".
Baada ya hapo unavua nguo zako
za Ihram na uvae nguo zako zilizoshonwa na mpaka hapa utakuwa umehalalika
mhalaliko mdogo (Tahallul Al-Asghar) na uzidishe kusoma kauli hii:
( الحمد لله رب العالمين رب السموات السبع ورب العرش العظيم وله
الكبرياء في السموات والأرض وهو العزيز الحكيم )
Halafu uende Makka ukatufu
Al-Kaaba na ufanye Saayi baina ya As-Safa na Al-Marwa kama ulivyofanya wakati
ulipofika Makka mara ya kwanza (Al-Quduum) na tawaaf hii huitwa Tawaaf Al-Ifaadhah),
nayo ni nguzo ya tatu katika nguzo za Hija na kwa nguzo hii inatimia Hija na
hii huitwa mhalaliko mkubwa (Attahallul Al-Akbar).
Iliobakia juu yako sasa ni
kurudi Muna ukalale huko usiku wa kuamkia kumi na moja na kumi na mbili kwa
wenye haraka na wasiokuwa na haraka walale usiku wa kuamkia tarehe kumi na tatu
vile vile. Kulala hapo Muna ni “Sunna Muakaddah” sunna iliyotiliwa nguvu ni
lazima ifanywe na atakayeacha kulala lazima achinje na wala wasiseme walio
matajiri na wenye kupenda starehe sisi tutalala mahala penye raha halafu
tutaziba kosa hilo kwa kuchinja akifanya hivi itakuwa ametoka nje ya sunna na
namuogopea kwa kitendo chake hichi kuwa hatokuwa na Hija. Atahadhari.
Katika siku hizi atakazobakia
Muna atakuwa kila siku baada ya kupinduka jua (wakati wa adhuhuri) ende kwenye
Jamaraat na ayapige kila moja katika hizo Jamaraat tatu vijiwe saba, aanze
kwanza Jamarat Assughraa, nayo ndiyo inayofuatia Muna yaani iko mashariki ya
zile Jamaraat nyingine kisha apige Jamar Al-Wusta halafu Al-Kubra na zote tatu
hizo azipige kutoka kwenye tumbo la wadi (bonde).
Hivi sasa serikali ya Saudia
Allah aijazi kheri imepatengeneza hapo mahali kwa kuwajengea sakafu chini na
kuwaekea vivuli na mapanka (mafeni). Lakini juu ya hivyo utalijua hilo tumbo la
bonde kuwa liko kusini ya hiyo Jamarat Al-Aqaba, na kwa hivyo wakati
unapolipiga hilo
Jamarat unakuwa umeelekea kasikazini na unaiweka Makka kushotoni mwako. Na hali
hiyo hiyo lile Jamarat Assughra lakini Jamarat Al-Wusta inakuwa kinyume ya
hivyo, huwa hilo bonde kaskazini yake na ukilitupia mawe huwa unaelekea kusini
na unaiwacha Makka kuliani mwako.
Hivyo vijiwe unavyovitupa
lazima iwe umeviokota wakati uko katika Ihraam sio wakati umevua hiyo Ihraam.
Si lazima kuviokota huko Muzdalifa bali yawezekana kuviokota mahala popote
katika Al-Haram hata hapo unapokaa Muna, kwani lazima vijiwe hivyo viwe safi sio kutoka sehemu
zenye uchafu kwa sababu hapo wewe unajikaribisha na Allah na haiwezekani kufanya
hivyo kwa kitu kilicho kichafu. Ndio maana inapendelewa uvioshe hivyo vijiwe
hata vikiwa safi, na inasemwa kufanya hivyo ni katika Sunna.
Jumla ya vijiwe vinavyotupwa
sabini kwa mwenye kuchelewa na arubaini na tisa kwa mwenye kufanya haraka.
Miongoni mwa wanavyuoni wapendelea kwa mwenye kuharakisha achukue vijiwe
ishirini na moja vya nyongeza ambavyo vyampasa mwenye kuchelewa avichukuwe
kisha avizike chini ya Jamarat Al-Aqaba. Iwapo litakuchwa jua siku ya kumi na
mbili naye bado yupo Muna basi inampasa alale hapo na akae mpaka adhuhuri siku
ya kumi na tatu kisha atupe vijiwe ishirini na moja kwenye hizo Jamaraat (kila
Jamara moja vijiwe saba).
Kwa kupiga hizi Jamaraat ndio
huwa mwisho wa vitendo vya Hija. Hapo umuombe Allah Subhanahu Wataala akukubalie
amali zako, wala asikujaalie miongoni mwa waliokhasirika basi ni juu ya mja
kufanya jitihada na ni juu ya Allah kupokea vitendo na ni wajibu kwa mja
atawakali kwake:
العنكبوت:
٦٩
“Na wale wanaojitahidi kwa ajili yetu, kwa yakini tunawaongoza
kwenye njia zetu. Na bila ya shaka Allah yu pamoja na wafanyao mema”.
Ukitaka kuondoka Makka kwa
niya ya kutorejea tena katika wakati huu basi inakuwajibikia kutufu tawaaf
Al-Wida’a hapo Al-Kaaba. Anayeiwacha tawaaf hii bila ya udhuru basi lazima
achinje na haikupasi kufanya saayi baina ya Safa na Al-Marwa.
Kila anayewacha kitendo kimoja
katika vitendo vya Hija au ametanguliza kitu badala ya kingine basi lazima
achinje mbuzi au kondoo katika ardhi ya Al-Haram, na asiile nyama yake yeye
wala aliofuatana nao.
Inapendelewa baada ya Tawaaf
Al-Wida’a ende kwenye mlango wa Al-Kaaba na akamate kizingiti chake na aegemeze
tumbo lake kwenye ukuta wa Al-Kaaba akiweza kufanya hivyo ama sivyo popote
alipo katika Msikiti huo wa Al-Haram aombe Dua ifuatayo:
( اللهم لك حججنا وبك آمنا
ولك أسلمنا
وعليك توكلنا وبك وثقنا وإياك دعونا فتقبل نسكنا واغفر ذنوبنا واستعملنا
لطاعتك اللهم إنا نستودعك ديننا وإيماننا وسرائرنا وخواتم أعمالنا اللهم أقلبنا
منقلب المدركين رجاءهم والمحطوطة خطاياهم ، الممحاة إساءتهم المطهرة قلوبهم منقلب من لا يعصي لك أمرا ولا يحمل وزرا
منقلب من عمرت بذكرك لسانه وزكيت بزكاتك نفسه ودمعت من مخافتك عيناه اللهم إني
عبدك وابن عبدك وابن أمتك حملتني على دابتك وسيرتني في بلادك وأقدمتني حرمك وأمنك
وقد رجوت بحسن ظني أن تكون قد غفرت لي فازدد عني رضى وقربني إليك زلفى اللهم لا تجعل
هذا آخر العهد مني عن بيتك الحرام ومن علي بالعودة مرات عديدة وصلى الله على رسوله
سيدنا محمد وآله وسلم )
4. Usiondoke Muzdalifa kabla
ya kusali Al-fajir isipokuwa kwa dharura.
5. Usisali Sala ya Magharibi
na Isha isipokuwa baada ya kufika Muzdalifa (kutoka Arafa) hata ikiwa mwisho wa
usiku.
6. Usipuuze kuvuka bonde la
“Muhassar” (Wadi Muhassar) kabla ya kuchomoza jua.
7. Uhakikishe kuwa vijiwe
unavyovitupa vimefika katika hizo sehemu unazozilenga nazo ni Jamaraat.
8. Uhakikishe kuwa unapovitupa
vijiwe uvitupe kutoka ndani ya wadi (hilo bonde lilioko hapo).
9. Usichinje kabla ya kutupa
vijiwe.
10. Usinyoe kabla ya kuchinja.
11. Usivue nguo za Ihram kabla
ya kunyoa.
12. Usiende kutufu Beit Al-Haram(Tawaaf
Al-Ifaadha) kabla ya kutupa vijiwe na kuchinja na kunyoa.
13. Uwe na yakini katika tawaf
yako kuwa umetufu mizunguko saba. Ukitia shaka basi rudia tena kutufu mpaka uwe
na yakini (kuwa umezunguka mara saba).
Hizi zote ni sunna ambazo
hamna budi kuzihifadhi au ikiwa hukuzihifadhi utaharibu Hija yako.
Mambo manne yanaharibu Hija
moja kwa moja na inambidi anayeyafanya ahiji tena mwaka ufuatiao:
1. Ikiwa hakuhirimia kwa Hija
na hakutia niya kutoka mwanzo basi huyo hana Hija.
2. Asiesimama katika Arafa
angalau kwa muda wa nusu saa kabla ya kutua jua katika siku ya tisa basi huyo
hana Hija.
3. Asietufu Tawaf Al-Ifaadha
na kufanya Saayi baina ya As-Safa na Al-Marwa huyo hana Hija.
4. Aliemuingilia mkewe katika
hali ya Ihraam au akamchezea mpaka ikamtoka manii basi hana Hija.
Inampasa mwenye Kuhiji
aziheshimu amri za Hija na azitukuze kwa mujibu wa kauli yake Subhanahu
Wataala:
الحج:
٣٢
“Namna hivi, anayehishimu alama za (Dini ya) Allah, basi hilo ni jambo
la katika utawa wa nyoyo.”
Na inampasa mwenye kwenda
kuhiji asikithirishe mazungumzo ya Dunia bila ya dharura bali azidishe
kumdhukuru Allah na wala asidhulumu, asigombane au kubishana na asighadhibike
ghadhabu itakayomsababisha afanye maasi na asubiri katika kila hali inayohitaji
subra na hakika Allah yu pamoja na wanaosubiri.
Katika mambo yanayosikitisha sana
kuwa baaadhi ya Mahujaji hawataki kuifupisha Sala huko Makka (wakasali zile
Sala zenye rakaa nne, kama Adhuhuri, Al-Asiri
na Al-Isha, rakaa mbili) kwa madai kuwa mahala hapa ndio asli ya Uislamu na
chanzo cha sheria kwa hiyo haisihi kufupisha Sala ndani yake. Na katika kutopea
kwao katika ujinga wanatoa fatwa kuwa haifai kusali “Qasran” (kufupisha) basi
hatusemi isipokuwa:
إنا لله وإنا إليه راجعون . Tunawaambia watu: Je
Waislamu wamechukua Dini yao kutoka kwa nani? Sio kutoka kwa Mtume Muhammad
Salallahu Alayhi Wasalam na yeye ndiye atoaye sheria na hana haki mtu yoyote
mwingine kufanya hivyo isipokuwa yeye hata akiwa na cheo kikubwa vipi. Mtume
Salallahu Alayhi Wasalam alipokwenda Makka na ndipo alipozaliwa na watani wake
wa mwanzo na watani wa baba zake, alipokwenda huko baada ya kuchukua Madina
watani wake, alifupisha Sala (za rakaa nne akazisali rakaa mbili) akasema
Salallahu Alayhi Wasalam: أتموا فإنا قوم سفر Timizeni Sala kwani sisi
ni wasafiri.
Jambo hili wamekubaliana nalo
Umma wa Kiislamu bila ya kupingana juu yake kwa hiyo hoja gani aliyo nayo yule
anayesali Sala kamili bali anapinga kufupisha Sala hapo Makka. Kama ingekuwa kutimiza Sala inaruhusiwa basi wa kwanza aliye na haki
hiyo ni Mtume Muhammad Salallahu Alayhi Wasalam kwa sababu yeye kazaliwa hapo
na kama alivyosema mwenyewe kuwa katika nchi
za Allah anazozipenda kuliko zote ni hiyo Makka na yeye ndiye aliyetuletea
sheria ya Allah Subhanahu Wataala. Basi fikirini sana
enyi mnaotimiza Sala hapo Makka ima mtakuwa nyie vile vile mmeleta sharia kama
alivyoleta yeye Salallahu Alayhi Wasalam basi imebakia kudai Utume na kuwa nyie
Mitume au awe Mtume ameficha kitu katika wahyi, na katika jumla ya aliyoficha
jambo hili la kufupisha Sala lakini nyie mkaweza kuligundua. Basi mcheni Allah
na jihurumieni nafsi zenu, msiende kinyume cha sharia na hali mnadai kuwa nyie
ndio mlio katika haki na waulizeni wenye elimu msiharibu amali zenu (vitendo
vyenu). Ewe unaetaka radhi ya Allah muendee katika njia yake (aliyoileta) ama
sivyo utanyimwa hicho unachokitaka (radhi yake Subhanahu Wataala).
Leo wamekuwa watu wa Dunia
nzima majirani wa Beit Al-Haram watu wa Japan katika mashariki, na watu wa
kusini ya Canada katika magharibi, na watu wa visiwa vya Siberia katika
kaskazini mashariki, na watu wa visiwa vya Hawaii katika kusini magharibi, wote
waweza kufika Makka siku hiyo hiyo wanaondoka kwao na wao wako mbali sana na
Makka. Ama watu wa Oman
anaweza mtu kusali Oman Sala ya Adhuhuri na Sala ya Al-asiri akasali Makka
Al-Mukarramah akisafiri kwa ndege.
Ama kwa njia ya bara mtu
anaweza kufika Makka katika muda wa saa arubaini bila ya juhudi wala
kujikalifisha na njia ina usalama Al-Hamdulillah. Na vyakula na vinywaji na
vinavyohifadhiwa katika mafridge na mafreezer vimejaa njia nzima, cho chote mtu
anachokitaka zaidi huwa chapatikana. Na wakati huu ndio ule aliokuwa akiutamani
Imam “Qeiyd Al-ardh” Allah amrehemu kwani katika niya yake ilikuwa amjaaliye
kila mtu anaekwenda kuhiji kutoka Oman asichukue chakula (cha njiani, yaani
ajaalie kila kitu kipatikane njiani).
Walikuwa Mahujjaji wachukua
kutoka Dhil Huleifa kwenda Makka siku nane na hakuna kinachowazuia na mwangaza
wa jua wala na baridi wala na mvua na wao wako katika Ihraam. Leo anapanda mtu
gari yenye Air Conditioner katika muda wa masaa manne kutoka Madina mpaka Makka
au kwa ndege muda wa nusu saa mpaka Jiddah.
Ilikuwa sehemu wanapotufu watu
(kuzunguka Al-Kaaba) wadi chini ya Al-Kaaba hawezi anaezunguka kunyanyua uso
wake kutokana na ardhi kwani akifanya hivyo atajikwaa na mawe na mavi ya
wanyama na mikojo yao
waliokuwa wakiwatumia kutufu juu yake. Leo kama ulivyoona au ulivyosikia ardhi
ya eneo hilo linalozungukwa ni safi zaidi kuliko jicho la jogoo wala hamna
mteremko wala mlima.
Ilikuwa sehemu inayofanyiwa
saayi baina ya Assafaa na Al-Marwa imezongwa na maduka haizidi upana wake mita
tano watu wasukumana ndani yake, wakati unapofanya saayi mara wajiona
umesukumwa na umerudishwa nyuma mita ishirini. Leo sehemu hii imefanywa njia
mbili ya kwenda mbali na ya kurudi mbali na kila njia upana wake mita tano na
katikati baina ya njia mbili hizi kuna njia ya kupitishia vigari vya wazee na
wasiojiweza. Vile vile kumetiwa ma Air Conditioner (yaburudishayo) na mataa
yaangazayo vizuri na juu ya sehemu hii kumejengwa sehemu nyingine ya kufanya
saayi isipokuwa mimi binafsi sipendi kufanya saayi huko.
Na alikuwa anaekwenda kusimama
Arafah anabeba chakula chake na maji yake juu ya mgongo wake na hubeba kiriba
cha maji kutoka Makka mpaka Muna na kutoka Muna mpaka Arafah, na huenda akakosa
maji siku nzima kwani ni katika vitu vilivyokuwa shida kupatikana. Leo kila
utakapokwenda unayapata maji kwa wingi bali maduka yako kila mahala na hukosi
unachokitaka ndani yake.
Ilikuwa kupiga vijiwe
“Jamaraat” kazi ngumu sana kwani njia za kukufikisha huko zilikuwa finyu na
hazikutengenezwa na ulikuwa msongamano wa watu mkubwa sana , na ilikuwa mtu hafiki huko ila baada ya
mashaka makubwa. Leo njia zimepanuliwa na zimesawazishwa na zimetiwa lami na
kufika Jamaraat leo ni wepesi sana na vile vile zimeezekwa sakafu hizo njia ili
kufanya kivuli na zimetiwa mafeni. Vile vile juu ya sakafu kumefanywa sehemu
nyingine ya kurusha mawe lakini mimi sipendi kurusha kutoka huko. Basi tizama
neema za Allah Subhanahu Wataala zilizo kubwa za kutusahilishia vitendo hivi
vya Hija, na sasa watu wanakwenda kwa wingi sana , zile tabu za mwanzo zimeondoka lakini
imekuja tabu ya wingi wa Mahujaji na msongamano kila mahala. Juu ya wingi wa
Mahujaji unakuta labda asili mia tano waliokuwa katika njia nzuri ya uongofu kama ilivyosemwa: “Wapandaji (ngamia) ni wengi na
Mahujaji ni kidogo”.
Katika athari kuwa mwaka
aliohiji Mtume Salallahu Alayhi Wasalam wamehiji pamoja naye watu laki moja
(100,000) na katika wakati wetu wa sasa wanaohiji hawapungui milioni mbili
2,000,000, na katika hao asili mia tano 5% kwa wingi kabisa ambao ndio Mahujaji
wa kweli kwa mujibu ya hukumu yetu ya dhahiri, na Allah ndie mwenye kujua
hakika. Na hiyo idadi ya Mahujaji wa kweli inawafikiana na idadi ya waliohiji
pamoja na Mtume Salallahu Alayhi Wasalam. Na imepatikana katika athari: “Ikiwa
idadi ya Mahujaji haifiki laki moja basi Allah Subhanahu Wataala anaikamilisha
idadi hiyo (laki moja) kwa Malaika”. Yakasihi maneno haya basi yamesihi yale
niliyoyakusudia (katika paragraph hii). Na Allah ni mwenye kutoa tawfiiq na
kuwaepusha na makosa waja wake, na yeye ndiye anayepokea na kukubali kidogo na
kusamehe kingi na yeye ni Mwingi wa Rehema.
Leo unaona maasi wazi wazi
chini ya Al-Kaaba hata angalau ile kuihishimu (hiyo Al-Kaaba) ikiwa
hawaihishimu Dini yao na Mola wao. Inasemekana kuwa katika zama za mwanzo
alimtizama mwanamme mwanamke katika tawaaf basi yakapofuka macho yake basi
wasidanganyike wafanyao maasi hapo wakiona haiwashukii adhabu ya Allah haraka:
آل عمران: ١٧٨
“Wala wasidhani wale wanaokufuru kwamba huu
muda tunaowapa (wanaishi kwa starehe) ni bora kwao. Hakika tunawapa muda na
inatokeya ya kuwa wanazidi madhambi katika muda huo. Na itakuwa kwao adhabu ya
kuwadhalilisha.”
Akasema yule mtu mwema: Basi alipomaliza kusema ile
Dua sikumuona tena, nikauliza juu yake nikaambiwa yule ni Al-Khadhr AS na
nikaihifadhi hiyo Dua. Twamuomba Allah atupe mwisho mwema na atufishe katika
hali ya uongofu (hali ya Uislamu).
Tanabahisho:
“Tahiyatul Masjid” ya Msikiti mtukufu huu wa Beit
Al-Haram ni “tawaaf”yaani kuizunguka
Al-Kaaba. Anaeingia msikiti huu kitu cha mwanzo anachokifanya ni kuzunguka
Al-Kaaba na hiyo ndiyo “Tahiyyatul Masjid” (maamkio) ya msikiti huwo kinyume na
misikiti mingine kwani maamkio yake ni Sala. Katika vitendo vilivyo bora sana
kuvifanya ni kutufu khasa kwa wanaotoka mbali. Inasemwa kuwa Mtume Salallahu
Alayhi Wasalam kasema:
( إن لله كل يوم مائة وعشرين نظرة ستون منها
للطائفين وأربعون للمصلين وعشرون للناظرين )
“Hakika Allah anatazama kila siku mitazamo(ya
Rehma) mia na ishirini miongoni mwa hiyo sitini ni ya wanaotufu na arubaini ni
ya wanaosali na ishirini ni ya wanaotazama” (Al-Kaaba). Basi inataka kuitumia
fursa hii kwani ni fursa ambayo haina badili.
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.