الصف:
١٠ - ١٢
“10. Enyi mlioamini! Je! Nikujuulisheni biashara
itakayokuokoeni na adhabu iumizayo?
11. Basi biashara yenyewe ni hii: Muaminini Allah na
Mtume wake na piganieni dini ya Allah kwa mali zenu na nafsi zenu haya ni
bora kwenu ikiwa mnajua (Kuwa ni bora, basi fanyeni).
12. (Mkifanya hayo) Atakusameheni dhambi zenu na
atakuingizeni katika mabustani yapitayo mito mbele yake na (atakupeni) masikani
mazuri katika bustani za milele huku ndiko kufuzu kukubwa.”
Jihadi kilugha ni kufanya juhudi na kujikalifisha
katika kufanya yaliokuwa na tabu na mashaka. Nayo (جهاد) jihadi ni asili ya
neno (جاهد) amejahidi nafsi yake kama katika kauli yake Allah Subhanahu Wataala:
الحج: ٧٨
“Na
ipiganieni dini ya Allah kama inavyostahiki kupiganiwa.”
Jihadi katika sharia maana yake ni kupigania na
kuihami dini, heshima na mali na imechukuliwa kutokana na maana yake ya kilugha
kwa hivyo ilivyokuwa katika kupigania dini uchukivu na uzito wa nafsi. Amesema
Allah:
البقرة:
٢١٦
“Mmelazimishwa
kupigana vita (kwa ajili ya dini). Nalo ni jambo zito kwenu.”
Aina ya Jihadi
Jihadi ni aina mbili:-
Fardhi inayompasa kila Muislamu.
Fardhi ambayo wakifanya jihadi baadhi basi haiwi
lazima kwa baadhi nyingine (haiwalazimu).
Katika hiyo fardhi ya kwanza ipo iliokuwa khaas mtu
binafsi na iliokuwa kwa ujumla (wote). Hiyo khaas ni jihadi ya nafsi yaani
kuilazimisha nafsi kumtii Allah Subhanahu Wataala na kuwa na tabia njema na
kujifundisha mambo ya dini na kuwafundisha wengine vilevile na kuikataza
kufanya maasi na shubha yanayopeleka katika hilaki kwani nafsi imeumbwa kupenda
raha ya dunia ya haraka na kupenda kujidhulumu na kudhulumu wengine bila ya
kujifikiria, imesemwa:-
“Kudhulumu ni katika tabia za nafsi, ukimkuta mwenye
kujitakasa basi kuna sababu ya kuwa hadhulumu”
Lakini mujahid anaimiliki nafsi yake na kuiongoza
anavyotaka mwenyewe kwa tawfiiq ya Allah kama
alivyosema katika kitabu chake Subhanahu Wataala:
ﭽ ﮠ ﮡ
ﮢ ﮣ ﮤ ﭼ العنكبوت: ٦٩
“Na wale
wanaojitahidi kwa ajili yetu kwa yakini tunawaongoza katika njia zetu”.
Basi
yule anayeitakia kheri nafsi yake na afuate njia za kuitengeneza na
kuilazimisha (hiyo nafsi) kuchukuwa mafundisho aliyoyapata katika wakati huu wa
sasa ili yamsaidie katika mustaqbal (kipindi kijacho) kwa kuogopa asije
akafanya makosa waliyoyafanya wenzake na kuizoesha kumdhukuru Allah Subhanahu
Wataala wakati wote na kuipa mawaidha. Imesemwa kuwa yule aliyekuwa wakati
haukumpa mafundisho basi hafaliwi na mawaidha atakayoyasikia kwa yeyote yule.
Yule aliyekuwa siku hazikumpa mafundisho basi upotofu ni karibu kwake kuliko
uongofu. Yule anayeyapima yale ambayo bado hajayaona kwa yale anayoyaona basi
yale yaliyo karibu naye yamuoneshe yale yaliyokuwa mbali naye.
Nafsi ikiwachiwa kama inavyopenda basi itaona raha
kufanya yenye ladha naye hajui kuwa sumu imo ndani ya kilionona, basi juu yake
kuizoesha (nafsi), tokea mwanzo mambo mazuri ya dini na dunia ili aondokee
katika hali hii tokea ujana wake mfano wa mtoto anayenyonya akifika umri wa
kuachishwa maziwa, akiachishwa, huwa rahisi kwake na huzoea, basi kama hivyo
nafsi ikiwa itafundishwa kufanya mambo mema, imetolewa shairi katika jambo
hili:-
Na nafsi ni kama
mtoto (mchanga) akipuuzwa huondokea kupenda kunyonya na akiachishwa huacha
(kunyonya).
Katika mambo muhimu yaliyokuwa yawajibika kuwa nayo
mtu katika kupigana jihadi ya nafsi yake ni kujifunza elimu iliyo lazima kwa
nafsi kuijua na iliyo juu yake kuijua. Aina ya kwanza ni kujuwa haki za Allah Subhanahu
Wataala zilizo wajibu na zinazojuzu na zilizo kuwa muhali kusifika nazo Allah Subhanahu
Wataala na kuwa yeye ni Mpweke na ndiye pekee anaye kusudiwa kwa haja za waja
naye amejipwekesha katika umoja hana mshirika wala aliye sawa naye wala ampingaye wala hakuna aliye mfano wake.
Hakuna chochote kilicho mfano wake. (Wenye) Macho hawamuoni Yeye na hakika yeye
ana uwezo wa kila kitu. Na katika yaliyo kuwa wajibu juu ya nafsi kujua yale
iliyokalifishwa nafsi kufanya katika mambo ya faridha na ya nafla na kujiepusha
yale aliyoyaharimisha Allah Subhanahu Wataala katika maasi yaliyo dhahiri kama
uongo na kulewa na kula mali ya watu isipokuwa kwa haki, na maasi yaliyofichika
kama riyaa, na kujipenda mtu nafsi yake na kutakabari na mengineyo, na
kuizowesha (nafsi) ukweli na uaminifu na kuhifadhi ulimi usiwaseme watu na
usiwafitinishe watu na kuacha yaliyokuwa hayamuhusu. Na kumkirimu mgeni na kwa
kufanya yote hayo itapata (hiyo nafsi) furaha ya nyumba zote mbili (dunia na
akhera). Na faridha (ya jihadi) iliyowahusu watu wote ni ile iliyomlazimu kila
iliyomuwajibikia taklifu afanye jihadi kwa nafsi yake na mali yake kwa dalili ya kauli yake
Allah Subhanahu Wataala:
التوبة:
٤١
“Nendeni (vitani) mkiwa wepesi na mkiwa wazito (wazima na
wagonjwa) na piganieni dini ya Allah kwa mali zenu na nafsi zenu”.
Katika jumla ya jihadi kumzuia
adui kwa kupigana nae anapohujumu milki ya binafsi, nchi, jamaa (mjumuiko wa
watu) au mali .
Ikiwa jeshi halina uwezo wa kuihami nchi basi inawapasa raia wote washirikiane
na jeshi hilo kwa kupigana na adui huyo
kwa mali na nafsi zao ili wamzuie na waivunje tamaa yake ya kutaka kuiteka nchi
yao.
Kuamrishana mema na kukatazana mabaya ni nguzo mbili
za msingi zinampasa kila baleghe kadiri ya daraja ya nguzo mbili hizo. Daraja yake
ya juu kabisa ni kupigana kwa ajili ya Allah Subhanahu Wataala ili kulinyanyua na kulitia
nguvu Neno (kalima) la Haki
nalo ni لا إله إلا
الله “La Ilaaha Illa Allah” na daraja
ya chini kabisa kuondoa uchafu njiani.
Aina ya pili ya jihadi ni
fardhi kifaya wakisimama baadhi ya raia kuifanya hiyo jihadi basi haiwajibikii
waliobaki nayo ni kuilinda nchi kutokana na adui ambaye anatarajiwa ubaya wake
(uadui wake) kwa kulinda zile sehemu ambazo ni wepesi adui kupenya ili kuhujumu
nchi, basi hata ikiwa huyo atakayejifunga kulinda ni mtu mmoja lakini ikiwa
wote wakakataa kujifunga katika hizo sehemu basi wote watahiliki, Allah Subhanahu Wataala atuepushe na kurudi nyuma
katika Jihadi.
Imefaridhishwa Jihadi katika
mwaka wa pili wa Al-Hijra baada ya kutulia Uislamu na waislamu katika mahala
pake pa amani napo ni Madina
Al-Munawarrah kwa dalili ya kauli yake Subhanahu Wataala:-
الحجرات:
١٥
“Wenye kuamini kweli kweli ni
wale waliomuamini Allah na Mtume wake kisha wakawa si wenye shaka, na
wakapigania dini ya Allah kwa mali
zao na nafsi zao. Hao ndio
wenye kuamini kweli”.
التحريم: ٩
“Ewe
Nabii shindana na makafiri na wanafiki”.
Hii ni amri ya ujumla (si kwa watu makhsusi katika
wakati makhsusi) imewajibikia umma wa Muhammad -rehema za Allah na amani
zimshukie- wote katika wakati wowote na mahali popote pale walipo.
Na kauli yake Al Haq:
الحج:
٣٩ - ٤٠
“Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa, kwa sababu
wamedhulumiwa. Na kwa yakini Allah ni Muweza wa kuwasaidia (39). Ambao
wametolewa majumbani (mijini) mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema “Mola
wetu ni Allah”. Na kama Allah asingaliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine,
bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyingine za ibada na
misikiti ambamo jina la Allah hutajwa kwa wingi."
Na kauli yake:
النساء:
٧٤ - ٧٥
“Basi nawapigane katika njia ya Allah wale wanaouza
maisha (yao) ya dunia kwa (kununua) ya Akhera. Na anayepigana katika njia ya
Allah kisha akauawa au akashinda, tutampa ujira mkuu (74) Na mna nini hampigani
katika njia ya Allah na (katika kuwaokoa) wale walio dhaifu katika wanaume na
wanawake na watoto ambao husema: Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu
wake ni madhalimu, na tujaalie tuwe tuna mlinzi anayetoka kwako, na tujaalie
tuwe tuna wa kutunusuru kutoka kwako”.
Na kauli yake:-
الصف:
١٠ - ١١
“Enyi mlioamini! Je! Nikujulisheni biashara
itakayokuokoeni na adhabu iumizayo? (Basi biashara yenyewe ni hii) Muaminini
Allah na Mtume wake na piganieni dini ya Allah kwa mali zenu na nafsi zenu haya ni
bora kwenu ikiwa mnajua (kuwa bora basi fanyeni)”
Na kauli yake:
التوبة:
١١١
“Allah amenunua kwa waislamu nafsi zao na mali zao (watoe nafsi zao na mali zao katika
kupigania dini) ili na yeye awape pepo. Wanapigana katika njia ya Allah, wanaua
na wanauawa. Hii ndiyo ahadi aliyoilazimisha (Allah) katika Taurati na Injili
na Qurani. Na ni nani atekelezaye zaidi ahadi yake kuliko Allah? Basi furahini
kwa biashara yenu mliyofanya naye (Allah), na huko ndiko kufuzu kukubwa.”
التوبة:
٢٤
“Sema; kama babu zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na
jamaa zenu na mali mlizochuma na biashara mnazoogopa kuharibikiwa, na majumba
mnayoyapenda, (ikiwa vitu hivi) ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Allah na Mtume
wake na kupigania dini yake basi ngojeni mpaka Allah alete amri yake”.
Unaona basi kuwa Allah Subhanahu Wataala ametanguliza
mapenzi ya jihadi kabla mapenzi ya mababa na watoto na mali na kila kilichoko
katika dunia na akamkaripia yule aliyoacha jihadi na akatishia kwa kauli yake فتربصوا yaani “basi ngojeni” na
akamwita yule anayeacha jihadi kuwa ni “Fasiq” yaani mwenye kufanya maasi
makubwa kwa mujibu wa kauli yake katika mwisho wa aya iliyopita:
التوبة:
٢٤
"Na Allah hawaongozi
watu maasi (njia iliyonyooka)”.
Basi kama inavyoonekana katika
aya hii kuwajibika kwa jihadi kuko wazi kabisa bila ya kufichika na kupendelewa
na kuekwa mbele (kiupaumbele) kabla ya kitu cho chote kingine. Na wakati Allah Subhanahu Wataala anapotaja Jihadi katika
Qur'ani anawasifu wale waliojisubirisha nafsi zao katika kupigania dini kwa
kujidhibiti nafsi zao na subra.
Anasema:
آل عمران: ٢٠٠
“Enyi
Mlioamini! Subirini na muwashinde makafiri (katika kusubiri) na kuweni imara
(nyoyo zenu) na mcheni Allah ili mpate kufaulu (kufuzu)".
Na mwendo wake Mtume -rehema
za Allah na amani zimshukie- ni ushahidi mkubwa na wa kutosha kabisa wa
kuwajibika kwa jihadi. Kwani yeye tokea mwanzo wake -rehema za Allah na amani
zimshukie- mpaka alivyomchukua Allah Subhanahu Wataala hakuiwacha wala hakuingiwa na udhaifu katika kupigana
jihadi tokea kupewa amri ya kufanya hivyo na Mola wake Subhanahu Wataala. Wakaifata njia yake hiyo
iliyo wazi masahaba wenye kuhishimiwa amewaridhia Allah wote kisha wakafata
njia hiyo baada yao maimamu wa waislamu ambao Allah Subhanahu Wataala amewapa tawfiiq ya kufuata
haki na akawaonyesha njia yake.
Jihadi ni miongoni mwa sunna
zake Allah katika viumbe vyake kwani amejaalia njia mbili za kuifanya haki
ikubaliwe na watu, njia ya kwanza kwa mafahamiano na njia ya pili kwa nguvu
kwani mwenye akili na insafu aikubali haki kwa kufahamiana. Ama aliye mjinga na
mbishi haikubali haki isipokuwa kwa njia ya nguvu, kwa hivyo amefaridhisha Subhanahu Wataala jihadi na ingekuwa bila yake
asingepwekeshwa Allah katika ardhi. Hapa ndipo lilipo ingia nguvu neno lake na kudhihiri dini yake. Na hii haipingani na
rehema uliyokuja nayo Uislamu wala uadilifu aliouamrisha Allah Subhanahu Wataala. Na anaepinga wito wa
kiislamu ni mbishani na mpingaji wa haki na muenezaji wa batili ni wajibu
kukandamizwa na kudhalilishwa kwa kutumia nguvu kwani hatarajiwi kuikubali haki
na kuiwacha batili isipokuwa kwa nguvu (kwa kupigana nae jihadi). Imewekwa
sharia ya jihadi kwa ajili ya kuzuia dhulma na fasadi katika ardhi na kuhami
mwito wa haki, na kuiwezesha dini ya
Kiislamu ienee katika ardhi na kuzuia shari ya makafiri juu ya Waumini,
wanaotaka kuwayumbisha wale waliokuwa imani zao dhaifu kabla ya kutamakani
uongofu katika nyoyo zao na kujaribu vilevile kuwapoteza walio na imani thabiti
kwa kuwatumilia njia (fitina) mbali mbali kama wafanyavyo leo maadui wa
kiislamu kwa njia zao za udanganyifu. Na wote bali wengi katika wanao mpwekesha
Allah Subhanahu Wataala wameathirika na
njia zao hizi kwa sababu ya ghafla yao kutokana na njia ya Mola Subhanahu Wataala kwa hiyo imewekwa jihadi sio
kwa ajili ya mapendekezo ya nafsi ya kutaka kumwaga damu au kuhifadhi vyeo (vya
dunia) bali imewekwa kwa ajili ya kuihami dini na kutia nguvu na kujikinga na
uadui (wa makafiri) kwa hiyo jihadi ni rehema kwa waja. Anasema Allah Subhanahu Wataala:
البقرة:
١٧٩
“Mtakuwa nao uhai (mzuri) katika kulipiza kisasi enyi wenye
akili”.
Na dalili zilizoko katika
sunna ya Mtume -rehema za Allah na amani zimshukie- zinazoonesha kuwajibika kwa
jihadi ni vile vita ambavyo amepigana na kuviongoza mwenyewe -rehema za Allah
na amani zimshukie- kama Badr, Uhud na Al Khandaq na kadhalika vile alivyovitayarisha
akawapeleka masahaba zake kuwa viongozi wake Allah Subhanahu Wataala awaridhie wote. Kama vile vilivyoongozwa na ammi yake Sahaba mkubwa Simba
wa Allah na bwana wa mashahidi Hamza bin Abdul Muttalib kwenda kwa Seif Al Bahr
nayo ni madh-har ya kwanza katika kuonesha nguvu ya Kiislamu. Navyo ni vita vya
kwanza ambavyo amevituma Mtume -rehema za Allah na amani zimshukie- baada ya
kufika katika mji wa Hijra yake na kunusuriwa kwake (Madina Al-Munawwara) kwa
miezi saba. Na kauli yake -rehema za Allah na amani zimshukie: “Nimeamrishwa
nipigane na watu mpaka washahadie kuwa hakuna Mungu isipokuwa Allah na kuwa
Muhammad Mtume wa Allah basi wakisema neno hilo wamekwisha jikinga na mimi damu
zao na mali zao isipokuwa kwa haki yake
na hisabu yao iko kwa Allah Subhanahu
Wataala". Hadithi na kauli yake Mtume -rehema za Allah
na amani zimshukie:- "Kichwa(Asili) cha jambo hili ni Uislamu na
aliyesilimu amesalimika, na nguzo yake (hilo jambo) ni Sala na kilele cha nundu
yake ni jihadi, haipati (hiyo jihadi) isipokuwa aliye bora wao". Na kauli
yake -rehema za Allah na amani zimshukie- kumjibu yule aliyemuuliza vitendo
gani vilivyokuwa bora akasema "Imani ya Allah na Mtume wake",
akaulizwa kisha nini akasema "Jihadi katika njia ya Allah" akaulizwa
kisha nini akasema "Hija mabroor (iliyokubaliwa)" akaulizwa kisha
nini akasema "kuwafanyia mema wazee wawili". Na kutokana na Abi Musa
kuwa Mbeduwi amemjia Mtume -rehema za Allah na amani zimshukie- akasema “Ewe
mjumbe wa Mungu mtu apigana kwa kutaka apate mali ngawira (wanyama) na mtu
mwingine apigana ili apate kutajwa na mtu apigana ili apate kuonekana mahala
pake nani katika hawa apigana kwa ajili ya Allah? Akasema (kujibu) Mtume wa
Allah -rehema za Allah na amani zimshukie: "Anaepigana ili neno la Allah lipate kuwa juu (kuwa
na nguvu) basi huyu ndie anayepigana kwa ajili ya Allah".
Fadhila ya wapiganao jihadi
kubwa. Anasema Allah Subhanahu
Wataala:
النساء:
٩٥
“Lakini Allah amewafadhilisha wale wapiganao kuliko wakaao kwa
ujira mkuu”.
Na katika hadithi iliyotoka
kwa Ibni Abbas radhi ya Allah iwe juu yake yeye na baba yake amesema:-
Nimemsikia Mtume wa Allah -rehema za Allah na amani zimshukie- akisema:-
"Macho mawili moto (wa jahannam) hauyagusi, jicho limelia kwa khofu ya
Allah Subhanahu Wataala na jicho limekesha
lalinda kwa ajili ya Allah". Na imetolewa kutokana na Sahal Ibn Saad kuwa
Mtume -rehema za Allah na amani zimshukie- amesema: "Kujifunga siku moja
(kwa kulinda adui) katika njia ya Allah Subhanahu Wataala ni bora kuliko dunia na vilivyo
kuwemo ndani yake. Na pahala pa fimbo (pasimamishwapo fimbo ambapo ni padogo sana ) pa mmoja wenu huko
Peponi ni bora kuliko dunia na vilivyo kuwemo ndani yake. Na mwendo wa mchana
anaokwenda mja katika njia ya Allah na mwendo wa asubuhi mapema ni bora kuliko
dunia na vilivokuwemo ndani yake".
Kuwacha jihadi kumewekewa
kitisho kikubwa cha adhabu ya Allah na mabalaa ya kudhalilishwa Waislamu na
maadui zao kwa kuacha Jihadi na vile vile kusababisha katika kupotezwa katika
dini yao .
Amesema Allah Subhanahu Wataala :
الأنفال: ٢٥
“Na iogopeni adhabu (Allah ya
hapa duniani) ambayo haitawasibu peke yao wale waliodhulumu nafsi zao miongoni
mwenu (bali itawasibu hata walio nyamaza wasiwakataze bali na wengineo pia)”.
Katika hadithi inayosema:-
"Hawakuacha watu jihadi (kupigania dini) isipokuwa Allah awateremshia adhabu wote". Kutokana na Abi Huraira
radhi za Allah ziwe juu yake anasema:- Amesema Mtume wa Allah: "Aliyekufa
bila ya nafsi yake kumsemesha kupigana jihadi (kupigania dini ya Mungu) amekufa
juu ya tawi katika matawi ya unafiki".
Na adabu za jihadi (taratibu
zake) zina daraja kubwa zimetajwa katika hadithi tukufu iliyotolewa kutoka
kwake -rehema za Allah na amani zimshukie- kuwa wakati akituma jeshi husema:-
"Kwa jina la Allah
na kwa Allah na katika njia ya Allah na katika mila ya Mtume wa Allah
msipindukie mipaka wala msivunje ahadi, wala msiwakate kate viungo mnaopigana
nao, msiuwe mtoto mdogo wala mwanamke wala mzee". Na katika adabu zake
isiwe jihadi itokayo nje ya kufuata (taa) amri za Allah na kufarikiana na jamaa
na anayekhalifu kisha akafa basi hufa kifo cha jahiliya. Na anaepigana chini ya
bendera ya upofu inayoita kwenye kupendeleana kwa ajili ya Ukabila, Ujamaa,
Urafiki (sio kupigana kwa kunyanyua dini ya Allah Subhanahu Wataala) au anayeghadhibika juu ya
kasumba hiyo basi akiuliwa basi kifo chake cha jahiliya (yaani hakufa katika
Uislamu) Allah Subhanahu
Wataala
atuepushe na kufa kifo kama hicho. Na vile
vile katika adabu zake kutokimbia wakati wa vita vimeshika (yaani vikosi viwili
vimepambana), na anayekimbia ni asi wa Allah kafiri kufuru ya neema kwani hiyo
ni katika madhambi makubwa kwa kauli yake Subhanahu Wataala:
الأنفال: ١٥ – ١٦
“Enyi Mlioamini! Mkutanapo vitani na wale
waliokufuru basi msiwageuzie mgongo (mkakimbia) (15) Na atakaewageuzia mgongo
wake siku hiyo isipokuwa amegeuka kwa kushambulia au amegeuka akaungane na
sehemu nyengine za jeshi hilo hilo la Waislamu (ikiwa si hivyo) atastahiki ghadhabu ya
Allah na mahali pake ni Jahannam. Napo ni
mahali pabaya pa kurudia (mtu)(16)”.
Amesema Mtume wa Allah Subhanahu Wataala: “Mambo matatu hayafai pamoja
nayo amali (vitendo):- Kumshirikisha Allah na kuwaasi wazazi wawili na kukimbia
kutoka vitani”. Na juu yake anaepigana jihadi awe na hadhari na awe macho na
kuwa amejitayarisha matayarisho makubwa na afuata kauli ya Allah Subhanahu Wataala:
الأنفال: ٦٠
“Basi waandalieni (wawekeeni tayari) nguvu
mziwezao (silaha), na mafarasi yaliyofungwa (kufuga) tayari tayari (mipakani),
ili kwazo (nguvu hizi) muogopeshe maadui wa Allah na maadui zenu, (mnaowajua)
na pia (maadui zenu) wengineo wasiokuwa wao, msiowajua nyinyi”.
Vile vile huyo
anaepigana(mujaahid) achukue hadhari kwa kutegemea khadaa ya adui na kuwa adui
apeleleza ghafla yake (mujaahid) hata katika wakati wa ibada na haisihi kwa
mujaahid aweke chini silaha yake isipokuwa kama kutakuwa cha kumkinga kama
alivyotunabihisha Allah Subhanahu
Wataala
katika kitabu chake kutukufu pale aliposema:-
النساء: ١٠٢
“Na unapokuwa pamoja nao
(Waislamu katika vita) ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame
pamoja nawe (wanasali) na washike silaha zao. Na watakapomaliza sijida zao
(kusali) basi nawende nyuma yenu (kwa kulinda) na lije kundi jingine ambalo
halijasali na lisali pamoja nawe nao washike hadhari yao na silaha zao (humo ndani ya sala, maana)
wale waliokufuru wanataka mghafilike na silaha zenu na vitu vyenu ili
wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa
sababu ya mvua au mnao ugonjwa, kuondoa silaha zenu. Na mshike hadhari yenu.
Hakika Allah amewaandalia makafiri adhabu itakayo wadhalilisha”.
Na Allah kawausia wapiganao
katika njia ya Allah kushikana pamoja.
Amesema Mola:-
الصف:
٤
“Kwa
yakini Allah anawapenda wale wanaopigana katika njia yake, safu safu (mkono
mmoja), kama kwamba wao ni jengo lililokamatana barabara”.
Na
akawahimiza kushikamana na kuunganisha rai yao , amesema Allah Subhanahu Wataala:
الأنفال:
٤٦
“Na mtiini Allah na Mtume
wake wala msizozane (msigombane), msije mkaharibikiwa na kupotea nguvu”.
Kukhitalifiana
rai ni upungufu (pengo) ambao adui bila shaka autumia ili kuwashinda waislamu,
na dalili kubwa ya jambo hili wakati washirikina waliposhindwa katika vita vya
Uhud waliweza kutambua mara tu wale waislamu, walioamrishwa wasiondoke kutoka
Jabali Uhud, walipoanza kuteremka na kuvunja amri ya Mtume -rehema za Allah na
amani zimshukie.
Na
Jihadi ina tunda katika dunia, nalo ni furaha, amani, neema na matumaini na
tunda lake katika Akhera ni furaha ya milele watakaotiwa humo ndani (Janna)
bila ya kutolewa. Na Mujahid alieuliwa kwa sababu ya kutaka kunyanyua Neno la Allah au kumzuia adui
dhalimu asiingie katika nchi (watani) yake au kukinga heshima yake (nafsi yake
na watu wake) au kupigania mali
yake basi anayeuliwa katika sehemu hizi yeye ni shahidi na daraja yake katika
Al-Janna yu pamoja na Manabii na Masaddiqqiin. Amesema Allah Subhanahu Wataala:
النساء:
٦٩
“Na
wenye kumtii Allah na Mtume wake, basi hao watakuwa pamoja na aliowaneemesha
Allah: Manabii na Masadiki na Mashahidi na Masalih (watu wema). Na uzuri ulioje
(kwa mtu) watu hao kuwa rafiki (zake)”.
Wapiganaji
Jihadi ni aina mbili. Aina ya kwanza ni wale wanaopigana na Washirikina. Na
aina ya pili ni wale wanaopigana na waliokiuka mipaka ya Allah Subhanahu Wataala.
Washirikina hapa wamekusudiwa Mayahudi, Manasara, wanaoabudu moto, Wasabai na
wanaoabudu masanamu katika waarabu na wengineo waliokuwa hawana dini. Na
amewataja Mola katika kitabu chake:-
الحج:
١٧
“Na
ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na wale washirikishao”.
Basi
ndio hivyo inabidi kupigana na Mayahudi, Manasara na waliokuwa mfano wao
wapigwe mpaka waingie Uislamu au walipe jizya (kodi) kwa hiari yao hali wametii kwa
dalili ya kauli ya Mola Subhanahu
Wataala:
التوبة:
٢٩
“Piganeni
na wale wasiomuamini Allah wala siku ya mwisho wala hawaharimishi alivyo
viharimisha Allah na Mtume wake, wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa wale
waliopewa Kitabu (piganeni nao) mpaka watoe kodi kwa hiari yao , hali wametii”.
Amma
wanaoabudu masanamu na wale waliortadi (wametoka kwenye Uislamu baada ya kuwa
waislamu) hawa wapigwa vita mpaka waingie Uislamu wala hawakubaliwi kutoa kodi
na mali
zao halali kuchukuliwa na hawana hiari nyingine isipokuwa kuingia kwenye
Uislamu na kuurudia Uislamu (kwa wale waliortadi) au sivyo upanga (yaani
wapigwe vita).
Na
vikundi vyote vilivyotajwa katika kitabu cha Allah kitukufu ambavyo vimekwisha
tajwa hapo nyuma vina hukumu katika sharia. Wakijichagulia nafsi zao upanga
basi zitekelezwe juu yao hukumu za Allah Subhanahu Wataala na
zachukuliwa mali
zao na wachukuliwa mateka wanawake wao na vizazi vyao na hao amewaita Mola Subhanahu Wataala
kinachomilikiwa na mkono wa kuume (milki al yamiin).
Amesema
Allah Subhanahu Wataala:
الأحزاب:
٥٠
“Na (wanawake) uliowatamalaki kwa mkono wako wa
kulia katika wale aliokupa Allah”
Amesema
Allah Subhanahu Wataala naye mkamilifu wa ukweli:-
البقرة:
١٧٧
“Sio wema (tu huo peke yake)
kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi katika kusali. (Yako na mema mengine). Bali wema (khasa) ni (wa wale) wanaomuamini
Allah, na siku ya mwisho na malaika na kitabu na manabii na wanawapa mali – juu
ya kuwa wanayapenda – jamaa na mayatima na masikini na wasafiri
(walioharibikiwa) na waombao na katika (kuwakomboa) watumwa”.
Vile
vile imekuja katika pahala pengine (katika Qur’ani) kwa lafdhi ya upweke
(mufrad):
البلد: ١٣
“(Kuukata mlima huo) ni kumpa mtumwa uhuru”.
Kuchukuwa
(kupata) mali yao na kuteka wanawake zao na vizazi vyao haya yote thabiti kwa
dalili ya Qur’ani na Sunna. Ama katika Qur’ani amesema Allah :-
الأنفال:
٤١
“Na jueni ya kwamba chochote
mnachokiteka (mnachokipata ngawira) basi sehemu yake ya tano (moja katika
tano)ni kwa ajili ya Allah na Mtume na jamaa (zake mtume) na mayatima na
masikini na wasafiri (walioharibikiwa) ikiwa nyinyi mumemuamini Allah na
tuliyoyateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuzi, siku (inayowafikiana na
siku) yalipokutana majeshi mawili (siku ya vita Badri, jeshi la waislamu na
jeshi la makafiri)”.
Basi
ndio hivyo yagaiwa mapato (ya nchi zilizofunguliwa na waislamu na ya vita) kama alivyobainisha Allah Subhanahu Wataala na akaweka wazi katika aya nyenginezo:-
الحشر:
٧
“Mali
aliyoleta Allah kwa mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji (vilivyo karibu
na Madina) ni kwa ajili ya Allah (basi yatatumika kwa ajili ya dini ya Allah)
na kwa ajili ya mtume (wake basi atachukuwa mwenyewe) na jamaa (zake) na
mayatima na masikini na msafiri aliyeharibikiwa”.
Na
katika rehema zake Allah Subhanahu
Wataala na uadilifu baina ya waja wake na kuwaweka wote wawe sawa
baina yao ni kutunabahisha tuikandamize nafsi
yenye kuamrisha kufanya maovu na kujiona bora kuliko mwenzake, basi tusiiwache kama inavyotaka bali tuiteremshe mbele ya mwenzake.
Anasema
Allah Subhanahu Wataala :-
الحجرات:
١٣
“Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele
ya Allah ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi”.
Kisha
baada ya hivyo akapanga Mola Subhanahu
Wataala hukumu za kuitowa ile nafsi iliyofungwa na pingu ya
utumwa kwa kuirejeshea uhuru wake na kuibandua(kuipapatua) kutokana na hukumu
za kutekwa, akajaaliya ukombozi wa mtumwa katika vitendo vyenye thawabu kubwa
sana ambapo akifanya kitendo hichi (kukomboa mtumwa) mwenye madhambi kinakuwa
sababu ya kumuokoa na kumuepusha (na adhabu ya Allah) kwa upungufu na makosa
aliyoyafanya katika haki ya Allah kama kuacha fardhi au kuua nafsi kwa makosa
au wenye kuapa kuwa watajitenga na wake zao au wale wawaitao wake zao mama zao
basi hawa wakitaka kutubu na kurejea kwa Allah Subhanahu Wataala
basi ni juu yao kukomboa mtumwa anayeashiriwa katika kauli yake Subhanahu Wataala:-
الأحزاب:
٥٠
“Na (wanawake) uliowatamalaki kwa mkono wako wa
kulia”.
Hekima
kubwa (haina shaka yoyote) ya Aliyetakasika na upungufu wowote, Mwenye Hekima,
Mwenye Elimu, Mpole kwa waja wake hawezi kukosa kuifahamu(hiyo hekima)
isipokuwa yule aliye mpumbavu na asi wa Muumbaji wake. Ajabu kubwa kusikia wale
maadui wa Uislamu wawatia fikra mbaya wale Waislamu wenye imani dhaifu kwa
kuwambia vipi inaruhusiwa katika Uislamu mtu kummiliki binaadamu mwenzake (ili
hali wanaona wazi kuwa Uislamu ndio unaohimiza kukomboa watumwa kwa kumlipa
anaefanya hivyo thawabu kubwa) lakini waleta fikra hizo mbaya ili kuhudumu
maslaha yao (ya
kuuchukiza Uislamu). Wao wameghafilika na mafundisho ya Muumbaji Mwenye Hekima
ambaye katika mikono yake kuna funguo za Mbingu na Ardhi kama
kwamba wao wako mbele (ya Allah Subhanahu
Wataala) katika kujua maslahi ya binaadamu na
kuwashughulikia. Waita mwito uliokuwa si wa kweli kabisa eti twataka haki za
binaadamu (na wao ndio wa kwanza wanaowateketeza binaadamu kwa kila njia
waiwezayo, khasa Waislamu).
البقرة:
١٥٦
"Hakika sisi ni wa
Allah, na kwake Yeye tutarejea(atatupa jaza yake)"
Amesema
Allah Subhanahu Wataala:
النساء: ٨٩
“Wanataka
(makafiri) lau mngekufuru kama walivyokufuru wao ili muwe sawa sawa”.
Basi
tahadhari ewe ndugu yangu wa Imani kutokana na neno hilo :-
الفرقان:
٢٨
“Eee Ole wangu (adhabu yangu)!
Laiti nisingalimfanya Fulani kuwa rafiki”.
Allah
Subhanahu Wataala atuhidi sote kwenye njia iliyonyooka.
Aina
ya pili: Waliopindukia mipaka nao ni katika
watu wenye kutamka Tawheed ambao husali na hufunga lakini wametakabari juu ya
viumbe na wakatoka nje ya utiifu wa hukumu wafanya hivyo katika msingi wa
kupindukia mipaka na kufanya uadui. Hawa wapasa kupigwa vita baada ya
kusimamishiwa hoja juu yao kuwa wamepotea njia ili warudi chini ya Utawala wa
Uadilifu na wafate hukumu zake na anaekufa miongoni mwao katika vita basi
huingizwa motoni, Allah atuepushe nao. Aina hii haichukuliwi mali yao wala
kutekwa vizazi vyao bali haihalalishiwi mali yao walau kitu kidogo kwa sababu
mali ya watu wa Qibla ni haramu kwa kauli ya Mtume -rehema za Allah na amani
zimshukie- amesema:-
(من قال لا إله إلا الله محمد رسول الله فقد أحرزوا مني أموالهم ودماءهم إلا بحقها
وحسابهم على الله)
“Wanaotamka ‘Lailaha illa Llah, Muhamadan
Rasulullah’ basi wamejikinga na mimi (kuwa siwachukulii) mali zao na damu zao isipokuwa kwa haki yake na
hisabu yao iko
kwa Allah."
Wao ni aina mbili:-
Aina ya kwanza huwa wanapo mahala
pa kukimbilia na wanaye kiongozi wa kumrejelea kwa mambo yao. Na aina hii
wakishindwa huuliwa majruhi wao (aliyejurihiwa) na hufatwa anaekimbia kati yao mpaka auliwe na mfano
wake vita vya Aliy bin Abi Talib katika Safein alipopigana na Muawiya bin Abi
Sufyan kwa sababu Muawiya ni marejeo kwa wanaoshindwa.
Aina ya pili – Hawana kituo
wala kiongozi wa kurejea kwake basi hao hauliwi majruhi wao wala hafatwi
anaekimbia kati yao na mfano huu ni vita vya Aliy bin Abi Talib vile vile siku
ya Al Jamal alivyopigana na Talha, Azzubeir na Aisha, basi alieshindwa kati yao
hauliwi wala hafatwi aliekimbia kwa sababu viongozi wawili Talha na Azzubeir
waliuliwa katika mapambano hayo na Aisha amerejea kutubu (Allah amridhie na
amghufirie makosa yake). Na Aliy bin Abi Talib katika vita vyote viwili hivi
yeye ni Imam wa haki kwa makubaliano ya Masahaba na ili kujua urefu wa matukio
haya arejee atakae vitabu vya tarehe na haiwezekani kujua ukweli au uhakika
isipokuwa yule anaeutafuta na kuufuata kwa insaaf. Amma utelezi au upotevu
hausemwi. Asije akasema Muislamu kama walivyosema wengine bila ya kujali ikiwa
jambo hilo analolisema
ni sawa sawa au kosa. Kwani wengi katika waandishi wa tarehe waliopita
wameipotoa tarehe ya vita vya Masahaba wakaiandika sio kama vile ilivyotokea na
waliokuja baada yao
wakawafuata bila ya kujitaabisha kuutafuta ukweli.
ولا حول ولا قوة إلا بالله Na
hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Allah.
Kutaja sifa za
wapiganaji katika njia ya Allah Subhanahu Wataala (Mujahidiin).
Twataja
sifa za Maimamu na wanavyuoni katika mujahideen wa Ahli Al-Istiqama na
twatosheka kwa aliyoyasema Mwana shairi (Mwana chuoni) wa wakati huo Sheikh Abu
Muslim Nassir bin Salim Arrawahiy wakati alipotaka kuwasifu watu wazuri hao
akatanguliza kuusifu mji wao (mji wa Nizwa) akasema kumwambia yule anayekusudia
huo mji. Katika shairi maana yake kama ifuatavyo:-
Fika,
teremka katika eneo lote lina utukufu, hapo ndipo haki ina nuru na matawi.
Teremka fika kwenye ardhi yenye nuru ambayo imewaweka Maimamu wa dini ya
uongozi juu ya mgongo wake na eneo lake
tambarare ambapo Malaika
wameingia katika sehemu zao. Kawaida kwa hao malaika kuingia na kuondoka katika
hizo sehemu (jinsi zilivyokuwa tahiri kwa hao Maimamu) Ardhi imetoharishwa,
imebarikiwa inayo nuru na hayo ni matunda ya elimu na imani kwa sababu ya
yakini yake (hiyo ardhi tahiri – Nizwa) na kufata kwake amri ya Allah Subhanahu Wataala
ameisaidia kwa kuipa ufunguzi, ushindi na kuayidiwa na Allah Subhanahu Wataala.
Umethibiti Uislamu hapo kutoka zama na zama ijapokuwa mara nyingine uadilifu
hujificha. Toka zamani sana yatajwa ardhi hii kwa kushika kwake dini toka
kuingia Tawhiid na Qur'ani. Basi ikasimama ngome ya Kiislamu mpaka maadui
wakanyenyekea na kuwa kituo cha kulinda uadilifu na uongofu. Mara ngapi Allah Subhanahu Wataala
amewapa ushindi (watu wa ardhi hii) dhidi ya watawala wa dhulma na shaitani.
Ameikhusisha Allah Subhanahu
Wataala kuwa ndipo pahala pa ushindi na ufunguzi kwa
Waislamu. Akaendelea kusema:-
Wakafuatana makhalifa wa Allah Subhanahu Wataala kuanzia Imam Al-Julanda na
kumalizia Imam Azzan. Maimamu hawa ndio waliohifadhi dini iliyotoka kwa Mola Subhanahu Wataala
toka siku iliyobadilika dini yake kuwa dini chungu nzima walikuwa wenye tabia
njema, makarimu na watu wa ibada, Simba (kwa ushujaa) wakataa dhulma, wao ni
kama majahazi ya kuokoa watu (kutokana na upotevu) viongozi wa watu nao ni kuta
zinazolinda Uislamu. Wakatenda yote yalioko katika Qur'ani katika siri yao na
dhahiri yao, Sunna ya Muhammad -rehema za Allah na amani zimshukie- (dini yake
safi aliyekuja nayo) ndiyo sira yao kwa kufanya hivyo wataka kuwa na Imani
sahihi na Ihsani. Wamefata sira ya Makhalifa wawili (Abu Bakar R.A na Omar
R.A.)
Nafsi
zao zafanya mkazo mkubwa katika kuinusuru dini ya Allah Subhanahu Wataala na
wajaalia nafsi zao fidaa katika kumnusuru Allah Subhanahu Wataala na
kufanya jihadi katika njia yake wakimbilia kufanya mambo ya kheri kwa vile
walivyokuwa mahodari na wajanja wamezikaribisha nafsi zao (wameziteremsha)
ndipo zilipokuwa na nguvu na kila ulipo uongofu utawakuta wapo hapo. Alama zao
ni nuru katika umbo lao na katika tabia
zao nao wanafata Sunna za Mtume Muhammad -rehema za Allah na amani zimshukie-
Hekima zao zipamoja na hukumu ya Allah Subhanahu Wataala na
hima zao. Wao ni wanaoiyona haki na kuisikia zaidi na katika batili wao ni
vipofu na viziwi hawapotezwi na mapambo ya dunia na udanganyifu wake kwani hima
yao ni kusimama katika njia ya Allah na radhi yake. Wameuza dunia yao ya kupita
kwa kutaka ridha ya Mola wao inayo baki kama kwamba ladha ya dunia hii haina
ukweli, hawakuwa mbali na njia ya Mukhtar katika mwendo wao wala azima yao
haikupindishwa na nafsi wala shetani basi wakapigana jihadi na kunyooka katika
njia yake mpaka ukawa utawala wao ni hukumu na sharia ya Allah Subhanahu Wataala.
Watu hao ndio mwangaza wangu nimeongoka kwa kuathirika nao na kufuata mfano wao
na malipo yake ni kuwapenda watu hao na kupata msamaha wa Allah na kughufuriwa
madhambi. Hao ni Maimamu (viongozi) wangu mabwana zangu, dalili yangu ndio
waokozi wangu kutokana na dhiki inayonipata. Allah Subhanahu Wataala
hakubali dini yoyote nyingine isipokuwa dini yao na hakuna uongofu mwingine
isipokuwa ule waliokuja nao, tokea zama za Badr na Uhud hawakuondoshwa kutoka
msimamo wa haki na fitina zilizopita na wala nyakati (wamebakia katika msimamo
ule ule).
Ikiwa
heshima ya watu duniani kwa mali na utajiri wao heshima ya watu hawa (Maimamu)
ni kwa yakini na Ikhlasi, kila wanachokifanya ni kwa ajili ya Allah Subhanahu Wataala tu.
Unawaona usiku wa manane wamesimama wasali na kusoma Qur'ani. Hao ni Maibadhi
wakarimu wenye daraja juu ya watu wengine kwa uwezo wa Allah Subhanahu Wataala.
Haujulikani uadilifu isipokuwa katika msimamo wao wa sawa na haikupewa mezani
haki yake na usawa isipokuwa kwao wao, kazi yao ni kujiweka mbali na yaliyo
haramishwa na Allah Subhanahu
Wataala sio kazi yao kuitaka dunia ni sawa sawa kwao
wakiipata au wakinyimwa (hiyo dunia) wameridhika na yale maisha waliyopewa na
juu ya hivyo wana wasi wasi kuwa labda wamechukua zaidi katika hayo maisha
kuliko wanavyostahiki. Alama za kutosheleka na maisha zaonesha katika sura zao kama kwamba ni matajiri, moyo umeshiba na tumbo lina
njaa. Njia ya wafalme(namna yao) na uongofu wa manabii katika tabia zao kama
kwamba ufakiri kwao ni ufalme, hao hawakudanganyika, na uhakika wa maisha ya
dunia kuwa ni hadaa. Wamevuka daraja (mtihani wa dunia) nao wamebeba mzigo
mwepesi wana khofu, subra, wamepuuza dunia na washukuru neema za Mola wao.
Wamefuzu wenye mizigo myepesi katika mahali hapa pa udanganyifu (dunia) hawana
hofu hao wala hawahuzuniki. Wamekwenda na athari yao na kumbusho lao ni nuru na
kuwataja ni rehema na malazi yao ni furaha na rehema. Wamefatilia Dola katika
athari ya Dola iliyopita yaani mfano ule ule mzuri kama Manabii aliyekuja
kaendeleza risala ya mtume aliyopita. Mpaka akasema (huyu mtoa shairi) mpaka
ikapambazuka nyota (Sayari) yenye mwangaza mkali na kumetameta na kwa mwangaza
wake ikadhihirika haki.
Na
akasema katika kumsifu Imam Salim bin Rashid Al-Kharusi katika Maimamu
waliochaguliwa kuongoza kwa sharia ya Qur'ani na Sunna mmoja kati yao alikuwa
amejaa imani katika kifua chake na hima yake ilikuwa kubwa sana na alikuwa
mwenye kuihifadhi nchi yake na kuitosheleza na mwenye uwezo wa kubeba dhamana
ya utawala. Umekuja uimamu wake na nchi imejaa dhulma na watu wako katika hali
ya fujo na madhalimu wafanya watakavyo basi akaweza kwa hekima kutengeza hali
hii na kueneza badala yake uadilifu na palipohitajia nguvu (jihadi) aliitumia,
kwani ushindi wa Allah Subhanahu
Wataala mwenza mwenzake ni jihadi (upanga), kwa sababu katika
hali kama hii ukitumia tabia nzuri na ukarimu haufai kitu lazima utumie nguvu.
Mtume wa Allah -rehema za Allah na amani zimshukie- wakati alipokuwa Makka
alifanyiwa maudhi na dhiki kubwa sana
lakini aliporudi kufungua Makka baada ya Al-Hijra amekuja katika hali ya nguvu
basi wale wale waliompa dhiki kabla wakamuangukia kumtaka radhi na msamaha.
Hapa
zatajwa aina za ukafiri.
(1)
Ukafiri wa shirki nao ni kumshirikisha Allah Subhanahu Wataala kwa
kuabudu mwengine pamoja na Yeye nayo inayojulikana kwa jina la Al-Musawaa yaani
kumfanya mwengine sawa sawa na Yeye Subhanahu Wataala. Au kukataa kuwa kuna Mungu
nayo inaitwa “Juhuud” au kukataa mmoja katika Manabii au Mitume wake au Malaika
wake au kukataa kitu katika Qur'ani Tukufu walau harufu moja au kukataa kitu
katika mambo ya faridha kama nguzo tano za kiislamu au kuhalalisha madhambi
makubwa na kuitaqidi kuwa sio haramu, na hizo ni zile kabair (Madhambi makubwa)
zilizotajwa katika Qur'ani au Sunna, au kurtadi kutokana na dini ya Kiislamu na
kuingia dini nyingine au kuufanya Uislamu sawa sawa na dini nyingine kama mtu
kusema:- Hapana kitu kwangu kufata dini yoyote katika hizi dini za Mbinguni
(Adyaan Samawiya) au dini za Allah Subhanahu Wataala.
(2)
Ukafiri wa neema (kufr Nneema) nao ni kufanya madhambi makubwa makubwa sawa sawa
ikiwa madhambi haya ni ya kuonekana au ya ndani (siri) na ya kuonekana kama
zina, riba, kula maiti au damu au nyama ya nguruwe, kuuwa nafsi iliyoharamishwa
kuuliwa, kuwakatia watu njia ili kuwaibia, kuwadhulumu waja, kuiba, kuudhi
Waislamu na kuwatia khofu, kueneza ufisadi katika ardhi, kunusuru batili
(kinyume cha haki), kuikataa haki na kuwapinga watu wake (wa haki) kunywa pombe
na vileweshaji vyote, kuvaa dhahabu na mengineyo kama kunyoa ndevu, kusaidia
watu wabaya na kueneza maasia katika magazeti, kuipamba batili, kutangaza mambo
ya washirikina kama kutangazia mavazi yao n.k. Haya yote ni katika madhambi
makubwa makubwa yanayoitwa kufr nneema kwa msingi wa Qur'ani na Sunna na Ijmaa
ya
Umma, miongoni mwa dalili zilizoko katika Qurani kauli yake
Mola:-
آل عمران: ٩٧
“Na
Allah Amewawajibishia watu wafanye Hija katika Nyumba hiyo yule awezaye kwenda
huko na atakayekanusha basi Allah si mhitaji kuwahitajia walimwengu”.
Na
kauli yake:-
الروم: ٤٤
“Anayekufuru
(madhara ya) kufuru yake ni juu yake (mwenyewe) na wafanyao wema (hao)
wanazitengenezea nafsi zao”.
Na
akaijaalia kufuru mukabili wake imani. Na kauli yake akizungumzia juu ya Nabii
Suleiman A.S.:-
النمل: ٤٠
"(Basi
alipokiona kimewekwa mbele yake) alinena:
'Haya
ni kwa fadhila za Mola wangu ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru (nitakuwa
mwizi wa fadhila)'."
Hapa
Allah Subhanahu Wataala ameijaalia kufuru mukaabili wake shukrani na kauli yake Mola Subhanahu Wataala:-
البقرة:
١٥٢
“Basi nikumbukeni (kwa
kunishukuru kwa hii neema niliyokuneemesheni ya kukuleteeni Mtume) (Nami)
nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru”.
Na
dalili katika Sunna ni kauli yake Mtume -rehema za Allah na amani zimshukie- kama
alivyoitowa Ibn Abbas R.A.:
(من قال
لأخيه يا كافر, فقال أنت الكافر فقد باء بالكفر أحدهما والبادي أظلم)
"Anaemwambia ndugu yake (mwenzake) ewe
kafiri akamjibu kumwambia wewe ndie kafiri basi amejitia katika ukafiri mmoja
wao na aliye dhalimu zaidi alieanza"
(من ترك قتل الحية خوف الثأر
فقد كفر)
"Anayewacha kumua nyoka
kwa kuogopa kumn’gata basi amekufuru"
Na
riwaya iliyotolewa na Ibn Abbas R.A.:
(من أتى الرجال شهوة دون النساء , أو أتى النساء
في أعجازهن فقد كفر)
‘Anaewaingilia wanaume badala ya wanawake au
kuwaingilia wanawake kwa nyuma basi amekufuru’.
Na
katika riwaya nyingine:
( ليس بين العبد والكفر إلا
تركه الصلاة)
‘Hakuna baina ya mja na
ukafiri isipokuwa kuacha Sala’.
Na katika riwaya nyingine:-
(العهد الذي بيننا وبينهم
الصلاة فمن تركها فقد كفر)
‘Ahadi iliyo baina yetu
(Waislamu) na baina yao
(Makafiri) ni Sala basi anayeiwacha (asisali) amekufuru’
Na
riwaya nyengine:-
(سباب المسلم فسوق , وقتاله كفر)
‘Kumtukana Muislamu ni ufasiki na kupigana naye
ni ukafiri’
Na
riwaya nyengine:-
(لا ترجعوا بعدي كفارا يضرب بعضكم رقاب بعض)
‘Msirejee baada yangu kuwa
makafiri mnakatana shingo wenyewe kwa wenyewe’.
Na
maasi yaliyofichika (yasiyoonekana) ni
kama yafuatayo:- Nayo ni kujiona nafsi yake kuwa hakuna kama yeye, kiburi,
hasadi, kufanya riyaa (kujionesha kwa watu unapofanya ibada yako ili wakusifu),
ghishi, khiyana na yote yale ambayo
tabia mbaya ndio huwa matokeo yake. Na sifa ya kujiona (ujbu) ni kuikuza
mtu ile neema aliokuwa nayo na kupendezewa nayo wakati anawacha kufikiri kuwa
amepewa neema hiyo na Allah Subhanahu
Wataala na kuwa ameipata kwa nguvu zake na uhodari wake na
ajiona kuwa ana hadhi. Inakuwa kujiona katika kila kitu katika sifa au mali au
uzuri au ukoo au elimu au ushujaa na mengineyo katika yanayo mpendeza mtu, na
anayosifiwa kwayo au apenda asifiwe kwa hayo mambo basi Muislamu akisibiwa na
ugonjwa huu basi ajiwahi nafsi yake upesi kuwa ajue kuwa Allah Subhanahu Wataala
ndiye mwenye fadhila juu yake kwa yale aliyoneemeshwa nayo na kupewa. Na kuwa
yeye mwenyewe hana uwezo wowote katika hayo aliyopewa. Kama
alivyosema Qaruni na Allah Subhanahu
Wataala amemuelezea katika kitabu chake kitukufu kwa kusema :-
القصص: ٧٨
Akasema: “Hakika nimepewa haya
kwa sababu ya elimu niliyonayo”. Je, hakujua ya kwamba Allah amewaangamiza
kabla yake watu waliokuwa wenye nguvu zaidi kuliko yeye na wenye mkusanyiko zaidi (kuliko wake
yeye)? Na wabaya hawataulizwa makosa yao. (Allah mwenyewe anayajua yote).
Na kiburi – ni kuwadharau
viumbe wenzake na kuirudisha haki (bila ya kuiamini na kuifuata) na sababu yake
ni kujiona kuwa ana utukufu na ana kitu na daraja wenzake hawana kama uraisi wa
nchi, uwaziri au umudiri au ukubwa juu ya
kikundi fulani cha watu, mambo haya yote yanamfanya mwenye kiburi
adanganyike navyo na ajione kuwa ana haki navyo vitu hivyo ndipo anapotakabari
juu ya wenziwe. Aliepata balaa hii ajitizame asili yake aliyoumbiwa nayo na wapi utakuwa mwisho
wake kama ilivyozungumzwa kutokana na Aliy bin
Abi Talib kuwa amesema: ‘Mwanadamu mwanzo wake ni manii iliyo chafu na mwisho
wake mzoga unaonuka naye baina ya mawili haya anabeba uchafu katika tumbo lake
(kinyesi)’. Imetolewa kutokana na Ibn Abbas: ‘Anaeikuza nafsi yake mbele ya
watu Allah humteremsha na yule anayeiteremsha nafsi kwa ajili ya Allah
humpandisha’ na imesemwa katika athari: ‘Hauingizi Al-Jannah uzito wa, chembe ya adesi, wa
kiburi na kiwango cha chini kabisa cha kiburi ni kuchukia mtu kueka mdomo wake
katika chombo pale alipoweka mdomo wake mnywaji kabla yake’.
Riyaa – ni kufanya
vitendo (amali) kwa ajili ya binaadamu (ili wamsifu) na inaitwa shirki ndogo
anaitwa kesho mtu kama huyu: Ewe muonyeshaji
ewe Fajir, ewe mvunjaji wa ahdi, ewe ulio khasirika jitihada yako ya bure na
amali yako imepotea. Anaepewa mtihani huu basi ni juu yake ajue kuwa viumbe
havimiliki kumfaa yeye au kumdhuru cho chote au chochote cha kumfaa au kumdhuru
bali anaefanya yote hayo ni Allah mmoja pekee ambae hakimshindi cho chote wala
hakimpiti cho chote.
Hasadi – ni kutamani
mwenzako aondokewe na neema aliopewa na Allah Subhanahu Wataala kama kusema katika nafsi yake
mtu huyu ana mali nyingi sana hastahiki kuwa nayo mali haya bora yangekuwa
yangu mimi nina haki zaidi nayo kuliko yeye. Dhambi hili ni katika madhambi
makubwa kabisa yaliyofichika nalo ni asli ya shari na kwa sababu yake fitina
zaenea na nafsi za watu zafisidika. Na mtu hasidi ni adui wa neema za Allah,
haridhiki na kadhaa ya Allah Subhanahu
Wataala
na kadari yake na juu ya yote hayo anakuwa mtu huyu anaghadhabu moyoni mwake
ambayo haimsaidii kitu, na moto ambao hauzimiki kwani yeye hawezi kuiondoa
neema aliopewa mwenzake kwani anaetoa na kunyima ni Allah Subhanahu Wataala.
Anasema mtungaji shairi:-
Kiumbe anaechukiwa kabisa na
Allah ni yule anaekesha amhusudu mwenzake wakati yuko katika kufurahika na
neema zake.
Imethibitika kuwa moyo wa
hasidi ni kama chumba kilichokuwa kina ngano
imebunguliwa na wadudu. Katika hadithi "Ukihusudu usipindukie mpaka
(usifanye uadui)". Inajuzu kutamani upate neema kama ya mwenzako bila ya
kutamani imuondokee na aina hii yaitwa “ghibta” na ya juzu kutamani iondoke
neema ya anaepiga vita Waislamu na kuwaudhi na kila aliekuwa neema yake ni
balaa kwa Waislamu.
Imetolewa kutokana na Ibn
Masood msije mkahusudu, mkafanya dhana na kufanya uadui (kupindukia mpaka)
kwani hana hadhi ya Uislamu anaefanya hivyo wala hadhi katika Uislamu anaefanya
jambo moja katika haya. Na kumdhania mtu vibaya inajuzu kwa yule anaejulikana
kwa ubaya kama ilivyopokelewa kutokana na Omar bin Khattab R.A.: ‘Tunaemjua ana
kheri twamsema kwa kheri na twamdhania vizuri na tunaemjua ana shari twamsema
kwa shari na twamdhania vibaya’. Mambo haya ni mifano ya maradhi yaliyo ndani
ya nafsi nayo yako mengi sana
katika hayo kuwadhania vibaya Waislamu na vile vile miongoni mwa hayo kukata
tamaa na Rehma ya Allah Subhanahu
Wataala.
Hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa kupewa na Allah Subhanahu Wataala. Tunamuomba Allah
asituharimishie shahada katika njia yake na atupe tawfiiq ya kupata ridha yake
na atujaalie tuwapende mawalii (wapenzi) wake na atujaalie tuwachukie maadui
zake. Hakika Yeye tu ndie Mwenye kutoa tawfiiq. Na Sala za Allah (Rehma) ziwe juu
ya Mtume wake Bwana wetu Muhammad pamoja na watu wake na Masahaba zake na
salamu vile vile ziwe juu yao .
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.