Tuesday, 19 January 2016

Juzuu 1 Wajibu wa mwanzo wa Muislamu---Kujenga uongofu katika nyoyo za vijana-----


JEZUU YA KWANZA



Jua (ewe Muislamu) Allah akuongoze wewe pamoja nasi katika kumtii Subhanahu Wataala kuwa kitu cha mwanzo kinachomuwajibikia Muislamu kukijua ni kumjua Mola wake aliyemuumba na kumpa riziki, naye ni “Allah”. Allah ambaye ameumba kila kitu na hakuna kitu kilicho kama Yeye, wala haonekani Duniani wala Akhera; kwani angekuwa aonekana basi angefanana na viumbe vyake. Hana mshirika wala msaidizi, wala waziri wala mshauri. Yuhai siku zote na ni mwenye uwezo na ujuzi wa kila kitu.


Kasema Allah katika sura Al-An’aam, aya 59:


               ﯲﯳ             ﯸﯹ            ﯿ                                           الأنعام: ٥٩

"Na ziko kwake funguo za siri; hakuna azijuaye ila yeye tu. Na anajua yaliyomo katika bara na bahari. Na halianguki jani ila anajua; wala (haianguki) punje katika giza la ardhi (ila anajua), wala (hakianguki) kilicho kibichi wala kikavu (ila anajua). (Hapana chochote) ila kimo katika kitabu kinachobainisha (kila kitu)."


Kasema Allah katika sura Fatir, aya 11:


           ﯿ         ﰃﰄ                   ﰌﰍ                           ﰘﰙ                 فاطر: ١١

 “Na Allah Amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha akakufanyeni wanaume na wanawake. Na mwanamke ye yote hapati mimba wala hazai ila kwa kujua Yeye (Mola). Na mwenye kupewa umri hapewi umri (zaidi) wala hapunguziwi umri ila mambo hayo yamo katika kitabu (cha Mola). Bila shaka (kuyapitisha) haya ni sahali kwa Allah ”


Hayo ndiyo mambo ya mwanzo ambayo ni lazima Muislamu ayajue. Kisha inampasa amjue Mtume wake Muhammad Salallahu Alayhi Wasalam kuwa ndiye aliyeletwa na Allah Subhanahu Wataala ili awaongoze watu katika njia ya Haki na yeye ni mkweli kwa ayasemayo, na ni wajibu wa kila Muislamu kufuata ayasemayo Salallahu Alayhi Wasalam na ayatendayo. Na kuwa yeye Salallahu Alayhi Wasalam amezaliwa Makka na akapewa Utume na Ujumbe huko huko Makka, kisha akahamia Madina na kuanzia huko ikatangaa Dini ya Kiislamu. Alifia huko Madina na kaburi lake liko huko mpaka Siku ya Kiyama.

Baada ya haya ni juu yake kuyajua yafuatayo:-

  1. Dini yake na mambo yaliyo lazima kuyaamini.
  2. Mambo yaliyo lazima kuyafanya.
  3. Mambo yaliyo lazima kujitenga nayo.


La kwanza katika matatu hayo:

Itikadi - Ni lazima aamini kuwa aliyokuja nayo Mtume Salallahu Alayhi Wasalam ni haki, na kuwa mauti ni haki, na kufufuliwa Siku ya Kiyama ni haki, na kuhisabiwa ni haki, na kuwa Siraati ni haki (njia ya Allah anaewatakiya waja wake waifuate), na kuwa Mizani ni haki (sio mizani tunayo ijua iliyo na mikono miwili na kuwa mema yatiwa katika mkono mmoja na mabaya yatiwa katika mkono mwingine bali ni uadilifu na uwezo wa Allah Subhanahu Wataala wa kujua vitendo vya waja wake (vibaya na vizuri), na kuwa Pepo ni haki na Moto ni haki na kuwa aingiaye Peponi hatoki tena milele na humo Peponi kuna kila inachotamani nafsi na kila linachoona raha jicho kukitizama. Na aingiaye Motoni hatoki tena milele ataadhibiwa na kufungwa pingu humo, atan’gatwa na wadudu wake watambaao (wanaotisha), ataunguzwa na moto wake na atazamishwa katika Zamharir yake (wadi katika Jahannamu inayokata viwiliwili kwa ubaridi wake kama ukatavyo moto viwiliwili kwa joto lake) atatamani mauti yamjie lakini hayatomjia na atatamani kurudishwa Duniani ili apate kufanya mambo mema hatokubaliwa, atakuwa akihamishwa kutoka kwenye joto la moto kwenda kwenye baridi ya Zamharir. Allah Subhanahu Wataala ametayarisha adhabu kali hiyo kwa waliomuasi na hawakukubali kumtii wala kumtii Mtume wake. Allah atuepushe hayo sisi na nyinyi.


Kasema Allah Subhanahu Wataala katika sura Annisa’a, aya 13 na 14:


                          ﯥﯦ                                          النساء: ١٣ – ١٤

[Na anayemtii Mola na Mtume wake, yeye (Mola) atamuingiza katika Bustani zipitazo mito mbele yake; wakae humo milele. Na huko ndiko kufaulu kukubwa. Na anayemuasi Mola na Mtume wake na kuikiuka mipaka yake (Mola) atamtia Motoni, humo atakaa milele na atapata adhabu zifedheheshazo.]


Vile vile ni wajibu wake aamini kuwa anaemtii Allah Subhanahu Wataala na Mtume wake Salallahu Alayhi Wasalam na akafanya kwa mujibu wa amri zao na akafa katika hali hiyo basi Allah atamtia Peponi na anawajibika kupendwa (na Waislamu) na mapenzi hayo huitwa “Al-Walaya”  (الولاية)  na anaemuasi Mola na Mtume wake na akafanya kinyume na amri zao na akafa katika hali hiyo (ya uasi) Allah atamtia Motoni na anawajibika kuchukiwa (na Waislamu) na huko kunaitwa Al-Baraa (البراءة).


Pia aamini kuwa anaekufa katika maasi hataombewa na Mtume Salallahu Alayhi Wasalam (kwa Allah Subhanahu Wataala) yaani   الشفاعة .

Kasema Allah katika sura Ghafir, aya 18:


               غافر: ١٨

 [Madhalimu hawatakuwa na rafiki wala muombezi atakayesikilizwa.]


Kasema Allah katika sura Al-Anbiya, 28:


          الأنبياء: ٢٨

 [Na (Hao Malaika) hawamuombei (ye yote) ila yule aliyemridhia (Allah).]


Mwenye kuasi hawezi kuwa mwenye kuridhiwa na Mola mpaka aombe maghufira na atubu.

Na Muislamu lazima aamini kuwa sifa za Mola ni Dhati yake Subhanahu Wataala (Yeye Mwenyewe) na wala hapana tafauti baina ya Dhati yake na sifa zake, na maana yake ni kuwa Allah ni mwenye elimu yaani katika sifa zake Subhanahu Wataala ni elimu, na elimu yake si elimu ya kupatikana kama ipatikanavyo elimu ya viumbe; kwani kiumbe huzaliwa mjinga kisha akasoma na kupata elimu wakati sivyo hivyo hali ya Mola Subhanahu Wataala, maana elimu yake sio ya ya kupatikana bali ni dhati yake. Na upime katika msingi huo sifa zake zote.


Vitendo - Inamlazimikia Muislamu afanye yale aliyoamrishwa na Allah kuyafanya  kama kusali, kutoa Zaka, kufunga Ramadhani, kuhiji, kusitiri utupu wake, kuwa na tabia njema, kuwatii na kuwafanyia wema wazee wake wawili, kuwasiliana na jamaa zake (kwa kuwatembelea au kuwaandikia au kuwapigia simu au kuwapelekea zawadi au salamu), kuwaliwaza majirani (katika misiba) na kutowaudhi na kustahamili kero lao, kuwa na maingiliano mazuri na watu, kutekeleza haki za Mola na za watu, kuwapenda (na kuwahurumia) wenye kuamini, kuwachukia na kuwaepuka makafiri, kuwatembelea wagonjwa, kushindikiza (au kufuata) majeneza ya Waislamu, kuwapenda mafakiri na kuwaliwaza, kutoa nasaha kwa ajili ya Allah Subhanahu Wataala, Mtume wake Salallahu Alayhi Wasalam na Waislamu kwa ujumla, kupatanisha waliogombana, kwenda kutekeleza haja za Waislamu, kutubia, kutekeleza ahadi, kusubiri katika shida, kuyategemesha kwa Allah Subhanahu Wataala mambo yake yote na kutawakali kwake, kujisafisha na najisi za mwili, nguo na mwahala pa kusalia, kuoga janaba na kuridhika na aliyogawa Mola katika mali na vyeo.


Kasema Allah katika sura Fussilat aya 46:


       ﰑﰒ      ﰕﰖ          فصلت: ٤٦

 [Anayefanya mema anajifanyia mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda ubaya ni juu ya nafsi yake (vile vile), na Mola wako si dhalimu (hata kidogo) kwa watumwa wake.]


Kasema Allah katika sura ya Israa aya 7:


      ﮰﮱ      الإسراء: ٧

 [Basi mkifanya wema, mnajifanyia wenyewe nafsi zenu; na mkifanya ubaya, mnajifanyia nafsi zenu wenyewe.]


Kujitenga: - Inamlazimu Muislamu ajitenge na mambo aliyoyakataza Allah Subhanahu Wataala na Mtume wake Salallahu Alayhi Wasalam nayo ni kama yafuatayo:-  Kuzini, kula Riba na maingiliano yoyote yanayohusu Riba (haifai kuchukua mkopo Benki wa Riba hata ikiwa imebadilishwa jina ikaitwa “interest” yaani faida), kuangalia utupu na kuuonyesha, kukojoa wima, kufanya liwati , kula nyama ya maiti, kuua nafsi (iliyokatazwa kuuliwa), kula nyama ya nguruwe, kuvuta sigara, kunywa pombe, kula mali ya watu bila ya ridha yao, kunyoa ndevu (hata kuzikata), kula nyama isiyochinjwa kihalali na kwa ajili ya Allah (kama ya muhanga au uganga au shetani), kuwatupa wazee wawili (kuwaasi au kutowatazama), kusema uwongo, kusengenya na kufitinisha  watu (kugombanisha), kusema maneno yaliyo batili kama mazungumzo yasiyopendeza, matusi na kutaja aibu za watu na kutaja tupu zao. Asijiweke Muislamu katika hali ya kutiliwa shaka na kutuhumiwa kwa mfano kwenda sinema, kusimama na mwanamke ajnabi (asiye Mahram kwake) au kumtizama, kucheka nae au kumkonyeza kwa jicho au nyusi, vile vile kukonyezana na mtu kwa kumdharau Muislamu mwenzao, kuwafanyia watu masikhara na asimsumbulie Allah Subhanahu Wataala kwa ajili ya vitendo vyake vizuri (Allah Subhanahu Wataala hana haja ya ibada yake, bali faida ya vitendo vyake inarudi kwake mwenyewe) kwani vitendo vya mja hata vikafika vinavyofika kwa uwingi na uzuri havifikii neema moja katika neema nyingi zisizohisabika alizopewa na Allah Subhanahu Wataala. Mja hakuvifanya hivyo vitendo vizuri isipokuwa kwa Tawfiiq ya Allah Subhanahu Wataala basi tena uko wapi uhodari wa mja?

Kasema Allah katika sura Fatir:


            ﮪﮫ                                                         فاطر: ١٥ – ١٧

 [Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Allah na Allah ndiye Mwenye kujitosheleza na Mwenye kusifiwa (kwa neema zake). Akitaka atakuondoeni na ataleta viumbe wapya. Na hilo kwa Allah kamwe si gumu.]



            Tena ni juu ya Muislamu ajifunze kujitia tohara – kujitoharisha mkojo na choo kikubwa, ambavyo vinaitwa “Al-hadathi Al-Asghari” (hadathi ndogo). Na kujitoharisha janaba, ambalo linaitwa “Al-hadathi Al-Akbari” (hadathi kubwa). Na ajifunze kufanya mambo haya.



Hadathi Ndogo:

Akitaka kukojoa ni lazima asitiri utupu wake asionekane wala asifunue nguo yake mpaka achutame, wala asikojoe pahala pagumu (kama juu ya saruji au mawe) kwa sababu chembe za mkojo zitamrukia nguoni mwake au mwilini. Akimaliza kukojoa asifanye haraka ya kuinuka kabla ya kufanya “istibraa”, nako ni kuikamua dhakari yake kutoka shinani (upande wa duburi) kuelekea upande wa kutokea mkojo kisha aikun`gute, afanye hivyo mara tatu mpaka ahakikishapo kuwa hakukubakia kitu ajipanguse pale panapotokea mkojo kwa kitu kigumu kinachofyonza kama jiwe au karatasi ya “tissue” (badala ya jiwe unaweza kutumia hizi karatasi “tissue paper”), kisha ajioshe kwa maji pamoja na sehemu zilizo kando yake. Na kadhalika choo kikubwa ajisafishe hivyo hivyo kwanza kwa karatasi halafu kwa maji. Na haitoshi kabisa kujisafisha kwa karatasi tu bila kufuatilia na maji, kwani akifanya hivyo Sala yake atakayoisali itakuwa batili. Na kikomo cha kujiosha ni kutumaini kuwa hakuna najisi iliyobakia. Na hii “Istibraa”, iliyokwisha zungumziwa, ni “Sunna” hapana budi kuifanya; ama kujiosha kwa maji ni faradhi anayeiwacha amekufuru (“Kufr neema”).


Hadathi Kubwa:

Nayo ni  janaba. Janaba hupatikana kwa kutoka manii katika utupu wa mtu (mwanamme au mwanamke) au kukutana ncha mbili za utupu  hata ikiwa chini ya kizuizi kama nguo. Pia hiyo “Hadathi Kubwa”ni  hedhi au nifasi” (ujusi).


Kuoga Janaba:

Inampasa aogae janaba kwanza akojoe ili yatoke manii yaliyobakia katika utupu wake; kisha aisafishe hiyo najisi kwenye utupu wake na pembezoni mwake; kisha ajioshe kutoka magotini mpaka kitovuni; kisha atawadhe udhu kama wa Sala. Kisha aoshe kichwa chake akitia vidole vyake nyweleni, kisha aoshe kifuani na tumboni na ahakikishe kuwa maji yafika katika zile sehemu zilizokuwa tabu maji kufika (kama baina ya vidole, kwapa na sehemu nyingine zilizo finyu), kisha aoge mgongo na kwapa na pande zote mbili za mwili, kisha aoshe kutoka magotini mpaka kwenye ncha za vidole na akishafanya hivyo anaweza akasali (bila ya kutawadha) ikiwa hakugusa utupu wake. Vile vile “Wadii” na “Madhii” vinatoka katika utupu wa mwanamme lakini haimuwajibikii mtu kuoga kama yakitoka manii, bali yamtosha tu kuosha zile sehemu zilizofikiwa na najisi hizi kama vile anavyojiosha mkojo. Kama tulivyoeleza kuwa manii ni najisi ioshwe katika kiwiliwili na nguo, na inawapasa wote wawili kuoga janaba mwanamme na mwanamke. Na kujihifadhi na najisi ni ibada kwa sababu ibada (kama kusali na Saumu) haitimii ila kwa kujitoharisha na najisi.



Wakati wa Sala ukifika anatakiwa Muislamu kwanza atawadhe. Na atawadhe kama ifuatavyo:

Aoshe viganja vyake huku akisema “Bismillah” na atie niya katika moyo wake kuwa anatawadha kwa kusali faradhi ya Adhuhuri au Al-Asiri au Al-Maghribi au Al-Isha au Al-Fajiri na aendelee kuihudhurisha niya hiyo moyoni mwake mpaka amalize kutawadha, kisha asukutue mara tatu akiyafikisha maji mpaka kooni isipokuwa akiwa amefunga asifikishe maji kooni, kisha ayatie maji puani huku avuta pumzi ndani ili maji yaingie vizuri, mara tatu, kisha aoshe uso mara tatu kuanzia mwanzo wa nywele kipajini mpaka mwisho wa kidevu na mapana kutoka sikio mpaka sikio, na ajioshe vizuri baina ya masikio na mashavu, kisha aoshe mkono wa kulia mara tatu kutoka kwenye kibwiko mpaka vidole na apenyeze maji baina ya vidole, afanye hivyo hivyo kwa mkono wa kushoto, kisha apanguse kichwani aanze mbele ya kichwa kwenda nyuma, apanguse mara moja, halafu apanguse masikio mara moja nje na ndani na huku atie vidole vyake ndani ya matundu ya masikio, kisha aoshe mguu wake wa kulia mara tatu kuanzia juu ya kisigino mpaka ncha za vidole na apenyeze maji baina ya vidole na ahakikishe kuwa kisigino kimerowa maji na wayo vile vile na afikishe maji kwenye mvungu wa mguu wake ausugue vizuri, halafu aoshe mguu wake wa kushoto hivyo hivyo kama wa kulia. Mpaka hapa udhu wake umetimia basi amuombe Allah Subhanahu Wataala ampe tawfiiq kwa kufanya faridha yake vizuri na amuombe Allah Subhanahu Wataala ampokelee amali yake.

Kasema Allah katika sura ya Al-Ankabut aya 69:


         ﮤﮥ          العنكبوت: ٦٩

 [Na wale wanaojitahidi kwa ajili yetu, kwa yakini tutawaongoza katika njia zetu. Na bila shaka Allah yu pamoja na wafanyao mema.]



Akimaliza kujitia udhu atakwenda kusali na ataelekea Qibla na kutia niya moyoni kuwa anasali faradhi fulani, kwa mfano atasema:

(  أتقرب إلى الله بأداء فريضة الظهر (أًو العصر أو المغرب أو العشاء أو الفجر )


Halafu atakimu kama ifuatavyo:

( الله أكبر الله أكبر الله أكبر الله أكبر، أشهد أن لا إله إلا الله أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمداً رسول الله أشهد أن محمداً رسول الله، حي على الصلاة حي على الصلاة، حي على الفلاح حي على الفلاح، قد قامت الصلاة قد قامت الصلاة، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله )


Adhana huwa kama hivi isipokuwa قد قامت الصلاة  haisemwi. Wala asiseme katika adhana ya Sala ya Al-Fajir: الصلاة خير من النوم . Na ni sharti kuisema “Ikama” upesi upesi sio kuisema polepole na kuivuta. Kisha atasoma Tawjih:

( سبحانك اللهم وبحمدك تبارك اسمك وتعالى جدك ولا إله غيرك إني وجهت وجهي للذي فطر السموات والأرض حنيفا وما أنا من المشركين )

Kisha atapiga Takbirat Al-Ihram, bila ya kusita baina ya Tawjih na hiyo Takbirat Al-Ihram, katika hali ya unyenyekevu na kuhudhurisha niya moyoni kuwa anahirimia Sala ya faradhi fulani (mambo yaliyokuwa halali kabla yanakuwa haramu baada ya takbirat Al-Ihram kama kuzungumza, kugeukageuka, kutizama watu, kula, kunywa na kadhalika). Wanavyuoni wanasema ikiwa hakuihudhurisha niya kwenye Takbirat Al-Ihram basi Sala yake inaharibika. Kisha atasoma: أعوذ بالله من الشيطان الرجيم kwa siri, halafu atasoma sura ya Al-Fatiha peke yake katika Sala ya Adhuhuri na Al-Asiri na katika rakaa ya tatu ya Al-Maghribi na rakaa ya tatu na ya nne ya Al-Ishaa. Na atasoma Al-Fatiha na sura au aya tatu kwa uchache katika rakaa mbili za mwanzo za Al-Maghrib na Al-Isha na Al-fajir. Kisha atarukuu na atasema katika rukuu: سبحان ربي العظيم mara tatu kisha atasimama na atasema katika kunyanyuka kwake: سمع الله لمن حمد na akishakuwa amesimama wima atasema: ربنا ولك الحمد . Halafu atasujudu na atasema humo: سبحان ربي الأعلى mara tatu kisha atakaa mpaka atulie katika kikao chake hicho, kisha atasujudu tena afanye kama mwanzo halafu asimame na kusoma kisha arukuu kisha asimame halafu asujudu halafu akae na kusujudu tena kisha akae kikao cha Tahiyatu cha mwanzo aseme:

التحيات المباركات لله والصلوات الطيبات، السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته، السلام علينا وعلى عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له وأشهد أن محمداً عبده ورسوله


Kisha asimame, asome, arukuu, asujudu kama mwanzo. Kisha asimame tena, arukuu, asimame na asujudu kama hapo mwanzo. Kisha akae kikao cha pili cha Tahiyatu na asome kama alivyosoma mwanzo na akifika عبده ورسوله  aongeze:

( صلى الله عليه وسلم أرسله بالهدى ودين الحق ليظهره على الدين كله ولو كره المشركون ربنا آتنا في الدنيا حسنة وفي الآخرة حسنة وقنا عذاب النار )


Na akitaka kuongeza kusoma dua ni vizuri akiwa peke yake lakini akiwa Imamu asiwacheleweshe jamaa. Akiomba dua bora ziwe dua za (kuomba) Akhera, katika dua ilizotuelekeza Qurani na Sunna kuzisoma. Na atahadhari asikae juu ya visigino vyake (katika Tahiyatu) akasimamisha nyayo zake au kujibweteka chini au kukaa kitako akasimamisha magoti yake kwani mikao hii yote inabatilisha sala. Kisha atoe salamu ageuke kulia na kusema السلام عليكم kisha kushoto na kusema: ورحمة الله  .


Wakati Imamu anapotoa Salamu hutia niya ya kuwatolea wale wanaosali nyuma yake. Ama akiwa mtu anasali peke yake hutia niya ya kuwatolea Malaika. Na asiseme kitu baina ya Sijda mbili (kwenye kikao). Baada ya kutoka kwenye Sala aombe dua yoyote ile atakayojaaliwa na Allah. Na inapendelewa asome aya ya “Al-Kursiy” baada ya kutoa Salamu. Na aihifadhi Sala yake baina ya Takbirat Al-Ihram na kutoa Salamu, asigeukegeuke wala kucheka wala asicheze (yaani asisogeze viungo vyake ovyo ovyo kama kujikuna au kushika ndevu n.k.) asitazame juu, asijikohoze isipokuwa kwa kutengeneza kisomo chake, wala asinyanyue mikono yake mpaka masikioni (wakati wa kupiga Takbiratu Al-Ihram) wala asifunge mikono (kwa kuweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto hata kinyume chake) wakati wa kusimama, wala asinyooshe kidole chake au kukizungusha wakati wa Tahiyatu, wala asiseme “Aamin” baada ya kusoma suratul Al-Fatiha kwani haya yanabatilisha Sala. Wala asimfanyie mtu ishara kwa mkono au kwa jicho wala asifikirie jambo lolote katika mambo ya Dunia kwa hiari yake (yaani kwa kutaka mwenyewe. Ama akiwa amepotezwa akili na Iblis basi na ajaribu kwa uwezo wake kushindana naye arudi kwenye Sala asikubali kutolewa kwenye Sala moja kwa moja) kwa sababu yeye yuko katika kisimamo kitukufu mbele ya Mfalme Mkubwa sana ambaye hawezekani na yeyote katika Mbingu wala Ardhi (na wala hakiwi chochote isipokuwa anachotaka yeye Subhanahu Wataala) kwa hiyo anawajibika kusimama mbele yake kwa adabu. Sala ni nguzo ya Dini na mwenye kutengeza Sala yake basi ibada zake nyingine vile vile zitatengenea. Kasema Allah katika sura ya Israa aya 22 -39 

         

                                       ﮞﮟ                                                                                         ﯤﯥ                                                          ﯽﯾ  ﯿ                                                                                             ﭲﭳ                                    ﭾﭿ      ﮂﮃ                      ﮌﮍ                                     ﮛﮜ                         ﮧﮨ                                     ﯘﯙ    ﯛﯜ                                           ﯨﯩ                           ﯵﯶ                              ﯿ               ﰅﰆ                                                                ﭗﭘ                             الإسراء: ٢٢ - ٣٩

"Usifanye mungu mwingine pamoja na Allah usije ukawa mwenye kulaumiwa (na) mwenye kukosa wa kukunusuru (22) Na Mola wako amehukumu kuwa msimuabudu yeyote ila yeye tu. Na (ameagiza) kuwafanyia wema (mkubwa) wazazi. Kama mmoja wao akifikia uzee, (naye yuko) pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie hata Ah! Wala usiwakemee na useme nao kwa msemo wa heshima (kabisa) (23) Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa (njia ya kuwaonea) huruma (kwa kuwaona wamekuwa wazee) na useme: Mola wangu! Warehemu (wazee wangu) kama walivyonilea katika utoto (24) Mola wenu anajua sana yaliyo nyoyoni mwenu. Kama mkiwa wema (kwa wazee wenu daima; lakini mara moja mbili hivi mkapotea, basi Allah Subhanahu Wataala atakusameheni) kwani yeye ni mwenye kuwaghufiria wenye kurejea (kwake) (25) Na umpe jamaa (yako) haki yake, na maskini na msafiri aliyeharibikiwa, wala usitawanye (mali yako) kwa ubadhirifu (26) Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashetani (wanamfuata mashetani). Na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake (27) Na kama unajipurukusha nao (sasa hivi kwa kuwa huna kitu) lakini unatafuta rehema ya Mola wako (riziki) unayoitumai, basi sema nao maneno laini (ya kuwapa waadi ya kuwa ukipata utawapa) (28) Wala usifanye mkono wako kama uliofungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote, utakuwa mwenye kulaumiwa (ukifanya hivyo) na kufilisika (ukiukunjua ovyo ovyo) (29) Hakika Mola wako humkunjulia riziki amtakaye na humdhikishia (atakaye). Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona; (anajua yupi anayestahiki utajiri na yupi anayestahiki ufakiri) (30) Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa umaskini. Sisi ndio tunaowaruzuku wao na nyinyi (pia). Kwa yakini kuwaua ni khatia kubwa (31) Wala msikaribie zina. Hakika hiyo ni uchafu (mkubwa) na ni njia mbaya (kabisa) (32) Wala msiue nafsi ambayo Allah amekataza (kuiua) isipokuwa kwa haki (Akahukumu Hakimu kuwa mtu huyo anastahiki kuuawa na akatoa amri ya kuuawa). Na mwenye kuuawa kwa kudhulumiwa, basi tumempa nguvu mrithi wake (juu ya muuaji huyo) akitaka ataomba kwa Hakimu kuwa amuue kama alivyomuua mtu wake na akitaka atamsamehe na akitaka atamtoza kitu). Basi (huyo   mrithi asifanye fujo katika kuua kwa ajili ya mtu wake aliyeuliwa). Hakika yeye atasaidiwa (na sharia maadam anayo haki (33) Wala msiyakaribie (msiyaguse) mali ya yatima, isipokuwa kwa njia iliyo bora (kwa hao mayatima) mpaka afike baleghe yake (huyo yatima akabidhiwe mwenyewe). Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itaulizwa (Siku ya Kiyama) (34) Na timizeni kipimo mpimapo, na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni wema kwenu na bora mwishoni (kwake) (35) Wala usifuate (ukipita ukiyasema au kuyafanya) usiyo na elimu (ujuzi) nayo. Hakika masikio na macho na moyo; hivyo vyote vitaulizwa (36) Wala usitembee (usende) katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala huwezi kufikia urefu wa mlima. (Basi unajivuna nini) (37) Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza mbele ya Mola wako. (38) Haya ni katika yale aliyekufunulia Mola wako katika hekima (zake). Wala usimueke pamoja na Allah, mungu mwingine, usije kutupwa katika Jahannam hali ya kuwa mwenye kulaumiwa (na) mwenye kufukuzwa (huku na huku) (39)."




Hii ndiyo madhehebu ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam ambayo ameteremka nayo Jibril A.S kutoka kwenye Al-Lawhi Al-Mahfoodh kutoka kwa Allah Mtukufu, Mwenye nguvu na sifa zote nzuri.

Walioko kwenye madhehebu hii wao ndio wenye haki pasi na shaka yoyote, na madhehebu nyingine zimetokana na madhehebu hii (kwani hii ndio asili na nyingine ni matawi yake). Jina hili (Ibaadhi) wamepewa kwa kunasibishwa na Abdullah bin Abaadh ambaye alikuwa mwenye heshima na mkali kwa ajili ya kufuata Dini. Na huku kunasibishwa madhehebu na yeye sio kwa kuwa yeye ndiye Imamu wa madhehebu hii kama walivyo Maimamu wa madhehebu nyingine, hapana, kwani Imamu wa Maibaadhi ni Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na Masahaba wake watukufu Radhi za Allah ziwe juu yao. Wao ndio waliochukua sheria ya Dini kutoka kwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kisha wakampa Muibaadhi muaminifu mwenye kutegemewa na  Mwanachuoni mkubwa alietoka Oman naye ni Jabir bin Zayd ambaye hakukosolewa katika uaminifu wake na ukweli wake sio na wafuasi wake tu bali hata na wapinzani wake.

Lakini sababu ya kunasibishwa Maibadhi na Abdullah bin Abaadh ni kuwa alikuwa anaihami na kuitetea Dini na alikuwa muongofu katika tabia yake na kuihami Dini katika wakati ulipogawanyika Umma ukawa madhehebu mbali mbali wakapata Waislamu mtihani mkubwa kwa mfarakano huu, jambo ambalo Allah Subhanahu Wataala hakuliamrisha lifanywe. Walikuwa Waislamu kama mwili mmoja na iwapo kiungo kimoja kitashtaki (katika mwili huo) basi viungo vyote vilivyobakia vitahisi maumivu hayo na homa hiyo (iliyosibu hicho kiungo kimoja). Kama alivyosema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na kutabiri kwa tukio hilo la kufarikiana Umma huu. Na kilichoandikwa na Allah hakina budi ila kutokea.


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:-

  افترقت اليهود على إحدى وسبعين فرقة كلها هالكة إلا واحدة وافترقت النصارى على اثنين وسبعين فرقة كلها هالكة إلا واحدة وستفترق أمتي على ثلاث وسبعين فرقة كلها هالكة إلا واحدة قيل فمن الواحدة يا رسول الله قال : من كانت على ما أنا عليه أو كما قال رسول الله

“Wamefarikiana mayahudi katika makundi sabini na moja na yote yameangamia isipokuwa kikundi kimoja na wamefarikiana manasara makundi sabini na mbili yote yameangamia isipokuwa kikundi kimoja na utafarikiana Umma wangu makundi sabini na tatu yote yameangamia isipokuwa kikundi kimoja” akaulizwa ewe Mtume wa Allah: Nani hao wenye kikundi hicho kimoja. Akasema: Kikundi hicho ni wale watakaofuata yale ninayofanya mimi. Au kama alivyosema Mtume wa Allah Salallahu Alayhi Wasalam”.


(Wakati huo wa fitina hizo akatokea huyu Abdullah bin Abaadh aliyekuwa na wivu na Dini ya Allah na mshupavu akaita watu warudi katika njia ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na makhalifa wake waliofuata njia ya sawa (khulafaa Arrashidiin) na kuwapinga vikali sana viongozi wa Bani Umayya basi hao walioitikia mwito wake wakaitwa “Maibaadhi”).


Maibaadhi hawakubadilisha kitu katika Dini tokea kuujua kwao Uislamu, wao wanakubaliana na Umma wa Kiislamu katika mambo yote ya Dini isipokuwa katika baadhi ya mambo ya itikadi ambayo haiwezekani kuhitilafiana juu yake (kwani haki iko kwa mmoja tu) na tumeyataja yaliyo muhimu miongoni mwa hayo katika kijitabu hichi kifupi.

Na watungaji wa vitabu wa Kiibaadhi huchukua haki kwa Mwanachuoni ye yote yule akiwa katika wao au katika wapinzani wao na hulikataa jambo lolote linalopingana na haki likiwa limeletwa na mwanachuoni wao au mwingineo. Tena siyo kila Muibaadhi maridhiya kwao isipokuwa wanavyohukumu kuwa Muislamu yeyote afaye bila ya kutubu na yungali aendelea kufanya maasi makubwa wanaona kuwa ataingia Motoni iwapo Ibaadhi au mwengineo, kwani hakuna aliye karibu na Allah isipokuwa mcha Mungu na hakuna aliye mbali naye isipokuwa muovu.


                                 طه: ١٠٩

 “Siku hiyo hautamfaa uombezi wa yeyote ila wa yule anayemruhusu Mola na kuiridhia kauli yake”.


Anasema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam katika kuwasemeza baadhi ya watu wake:-

 ( يا فاطمة بنت محمد ويا صفية عمة محمد : اشتريا أنفسكما من الله فإني لا أغني عنكما من الله شيئا لا يأتينى الناس بأعمالهم و تأتوني بأنسابكم )

"Ewe Fatma bint Muhammad na ewe Safiya shangazi yake Muhammad zinunueni nafsi zenu kwa Allah, kwani mimi siwafai kitu kwa Allah, wasinijie watu na vitendo vyao nanyi mkanijia na nasabu zenu"

(Uhusiano wenu kwangu wa kidamu mkafikiria kuwa utawasaidia, la siku hiyo haimsaidii mtu isipokuwa amali yake aliyoifanya, hakuna “wasta” wala “influence”).


Na anasema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:-

من قصر به عمله لم يسرع  به نسبه

“Mwenye kupungukiwa na amali (vitendo vyake) haitamsaidia kitu nasaba yake (uhusiano wake kwangu)”.


Kwa hiyo anaetilia shaka madhehebu ya Kiibadhi atakuwa ameitilia shaka Dini yote na mwenye kuwatia makosani Maibadhi atakuwa amewatia makosani Masahaba wa Mtume wa Allah Salallahu Alayhi Wasalam na hakika Allah Subhanahu Wataala ni Mjuzi wa kila alitamkalo mtu basi na aseme alitakalo (atahisabiwa na Allah Subhanahu Wataala Siku ya Kiyama). Na mwenye kutatizwa na jambo lolote awaulize wenye elimu kwani elimu ndiyo ya kuulizwa.


Tunamuomba Allah Subhanahu Wataala atuongoze njia ya haki na atufahamishe Dini yetu kwani Anaemtakia kheri humpa hiyo (kheri). Na hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Allah Mtukufu na Rehema zake zimfikie Mtume wake mkarimu Salallahu Alayhi Wasalam na Masahaba zake wenye fadhila kubwa.

No comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.