الحج: ٤١
“Wale
ambao tukiwamakinisha (tukiwaweka uzuri) katika ardhi husimamisha Sala na wakatoa Zaka na wakaamrisha yaliyo
mema na wakakataza yalio mabaya.
Na marejeo ya mambo ni kwa Allah”
Aya 41 sura ya Al-Hajj
Utangulizi
Shukrani zote anastahiki Allah Subhanahu Wataala, Mola
wa walimwengu wote na Rehma zake na Amani zake zimwendee Mtume wake Muhammed
bin Abdillah bora wa Viumbe na Mitume. Basi kama ilivyotangulia hii jezuu ya
kumi inaendelea kuwa katika mtiririko wa “kujenga Uongofu katika nyoyo za
vijana” na tumechagua izungumzie jambo muhimu katika tarehe nalo ni “fikra kwa
ufupi juu ya Maimamu wa waislamu katika Omani na nchi nyenginezo iliyoenea
ndani yake madhehebu hii “ya Ahli Al-haq na Istiqama”. Amesema Allah SUBHANAHU
WATAALA :
يوسف: ١١١
“Bila
shaka katika hadithi zao hizo limo zingatio kwa wenye akili”
Na naapa kuwa visa hivyo ni fundisho kubwa kwa anaye
refusha fikira na maoni kwani nidhamu ya Uimamu katika Omani imekuja kuwa nguzo
ya kimsingi ya kuhifadhi Dini hii tukufu na kuieneza na kuikita mizizi yake.
Ijapokuwa pana tofauti baina ya majina mawili “Uimamu”
na “Ukhalifa” isipokuwa yanaonesha kitu kimoja (maana yake ni moja) kwani
nidhamu ya “Uimamu” imesimama juu ya msingi wa “Asshuraa” (kushauriana baina ya
waislamu) na dalili yake kuwa Imam hapati sharia ya kuhukumu na kuwa Khalifa
juu ya rayia isipokuwa baada ya kuchaguliwa (Siyo kwa urithi).
Amesema Sheikh Noor Addiin Assaalmiy -Allah Amrehemu-
katika “Madaarij Al-Kamaal”:
“Ni wajibu wamchague Imam wakipata uwezo
timamu nao ni kupatikana watu arubaini ambao hawakushughulishwa na baadhi ya
mambo kama utumwa, umaskini maradhi na hawakuhitilafiana, lao moja na kati yao
wapatikane watu sita wenye elimu (wanavyuoni), na wajiepushe na mambo ya haramu
na shubuha, wenye kutegemewa katika elimu na uaminifu na wenye hima kubwa.
Wametaraji ushindi katika kusimamisha Uimamu ndio wakaona wamchague aliye bora
wao ili awaongoze”
Na katika kitabu “Muqadimat Attawhiid” na sherehe yake
kilichotungwa na Mwanachuoni Abi Hafs Amru bin Jamii kuna maelezo juu ya
“Uimamu” ambao ameuita kwa jina la “Masaalik Addiin” yaani njia za Dini na
idadi yake ni nne:-
1) Adh-dhuhuur – Uimamu
wa kudhihiri.
2) Ad-difaa’ – Uimamu wa
kujihami (na adui).
3) Ash-shiraa – Uimamu wa
kujitolea mhanga.
4) Al-Kitmaan – Uimamu wa
kificho.
Amma Adh-dhuhuur huu ni kama wa Abi Bakar Assiddiq na
Omar bin Al-Khattab R.A. na Ad-difaa’ ni kama
wa Abdillah bin Wahab Arrasbiy. Na Ash-shiraa’ ni kama
Uimamu wa Abi Bilal Mirdaas bin Judere. Na Al-Kitmaan kama wa Abi Ubaidah bin
Abi Karimah na Abi Al-Sshaathaa Jabir bin Zeyd R.A.
Kwani hiyo ni wazi kuwa “Uimamu” unatafautiana njia
yake ya hukumu kutokana na hali ya mambo iliyouzunguka Umma wa Kiislamu na
unawajibika kuchagua msingi wa vitendo unaokabiliana nao.
Bila ya shaka mazungumzo ya “Uimamu” hakiwezi kitabu
cha muhtasari (ufupi) kama hichi kuchukua yote yanayohusikana nao isipokuwa
lengo ni kuwajulisha Maimamu muhimu na vipi wameeneza daawa yao na Allah ndio pekee mwenye kukusudia kitu
kikiwa na yeye ndie Anaeongoza katika njia iliyonyooka.
Imetolewa kuwa Mtume Mohammed
-rehema za Allah na amani zimshukie- amesema:
"يحمل هذا الدين من كل خلف عدوله ينفون
عنه تحريف الغالين وانتحال المبطلين وتأويل الجاهلين..."
“Wanaikamata Dini hii waadilifu miongoni mwa wafuatiao (kutoka
kwa waliotanguliya) waihami kutokana na upotofu wa wanaopindukia mipaka, na
uongo wa wanaojidai wameshika Dini na tafsiri ya wajinga…”
Basi kama hivyo waadilifu wa Ibadhi wameichukua Dini
hii na wakasimama katika haki yake kama
inavyowajibika, anaichukua afuatiaye kutokana na atanguliaye, na akataae hayo
basi akatae au akiri kwani haidhuru kitu mwenye kukataa wala haizidishii kitu
mwenye kukiri. Kwa hivyo waadilifu wa kila Karne wameichukua Dini hii kutoka
kwa waadilifu wa Karne iliyo kabla yao mpaka wakafikia kwa Mtume wa Allah
-rehema za Allah na amani zimshukie- ambaye ndiye chanzo cha asili ya dini hii
na ndiye Rehema ya Umma huu naye kaichukua kwa Jibriil Mwaminifu A.S kutoka
Allouh Al-Mahfoodh” kutoka kwa Mola Mwenye Nguvu Muabudiwa wa Viumbe na
inawatosha Maibadhi sharafu kubwa kuwa wanayo hii Sanadi tukufu (upokezi)
haitilii shaka yeyote mwenye akili. Twamuomba Allah Subhanahu Wataala atukinge
na upotofu.
Na kama ilivyo hivi
sasa tuko katika Karne ya kumi na tano (Hijiri) na wamo ndani yake wanavyuoni
wanaojulikana na mkubwa wao Mwanachuoni Mkubwa mujtahid Ahmed bin Hamad bin
Suleiman Al-Khaliliy ambaye amewaita wanavyuoni wa Dunia kuja kufanya mdahalo
naye (debate) katika maudhuu ya “Al-Aqida” na hakuna aliyeweza kunyanyua kichwa
chake kumjibu, Allah Subhanahu Wataala ambariki yeye pamoja na ndugu zake
wanavyuoni, wazee kwa vijana.
Basi hao wamechukuwa dini yao kwa waadilifu wa karne
ya kumi na nne na wao ni Noor Ad-diin Abdullah bin Hameid As-Saalmiy, na
Muhaqiq Amour bin Khamis Al-Maalkiy, Imam wa Waislamu Mohammed bin Abdallah
Al-Khaliliy, Imam na Mwanachuoni Mkubwa Majid bin Khamis Al-Abriy, sheikh wa
kuaminika Abdullah bin Mohammed Arriyaamiy, sheikh Esa bin Saleh Al-Harthiy na
wengineo.
Hao wamechukuwa dini yao kwa waadilifu wa karne ya
kumi na tatu na hao ni: sheikh Arrabani Saeed bin Khalfan Al-Khaliliy na sheikh
Saleh bin Ali Al-Harthiy, Mohammed bin Salim Al-Ghaarbiy, Nasser bin Jaaiid
Al-Kharusiy na Sultan bin Mohammed Al-Battashiy na wengineo.
Na hao wamechukuwa dini yao kwa waadilifu wa karne ya
kumi na mbili na hao ni: sheikh Saeed bin Bashiir Assubhiy, sheikh Jaaid bin
Khamis Al-Kharusiy, sheikh Saeed bin Ahmed Al-Kindiy, sheikh Khalaf bin Sinan
Al-Ghaafriy, sheikh Nasser bin Suleiman na Mohammed bin Midaad.
Na hao wamechukuwa dini yao kwa waadilifu wa karne ya
kumi na mmoja na hao ni: Sheikh Khamiis bin Saeed Asshaqsiy, sheikh Masood bin
Ramadhan Annabhaniy, shiekh Khamiis bin Ruweishid Al-Majrafiy, Sheikh Saleh bin
Saeed Al-Zaamily na Sheikh Abdallah bin Mohammed bin Ghassan Al-Kindiy.
Na hao wamechukua dini yao kwa waadilifu wa
karne ya kumi nao ni Mohammed bin Abdulbaqiy mwanachuoni mkubwa kabisa na
sheikh Abdallah bin Omar bin Ziyad Al-Shaqsiy na Mohammed bin Ahmed bin
Ghasan na mwanachuoni mkubwa Ahmed bin Midaad na sheikh Mohammed bin Abdallah
bin Midaad . Na hao wamechukua dini yao kwa waadilifu wa karne ya tisa nao ni
Ali bin Abdulbaqiy na Sheikh Ahmed bin Saleh bin Mufarraj na sheikh Saleh bin
Wadhaah, na Sheikh Suleiman bin Ahmed bin Mufarraj na Sheikh Abu Alhassan bin
Khamis bin Amour. Nao wamechukua dini yao kwa waadilifu wa karne ya nane nao ni
Mwanachouni mkubwa Saeed bin Ahmed bin Mohammed bin Saleh, na Sheikh Abu
Al-Qassim bin Abu Shaaeq na ndugu yake Abdul Al-Rahman bin Abu Shaaeq, na Shekh
Suleiman bin Rashid bin Saqr Al-Adawiy na ndugu yake sheikh Dahman bin Rashid bin
Saqr basi hao wamechukua dini yao kwa waadilifu wa karne ya saba nao: Ahmed bin
Al-Nadhr bin Suleiman mwanachuoni aliekufa shahidi na aliuliwa na Khardala Al-Jabbar, na sheikh
mkubwa Abu Omar Al-Nakhliy, na sheikh Saeed bin Ahmed bin Mahmood , na Abu Al-Miikaal
Musa bin Kahlaan , na sheikh Abu Othman bin Abu Abdallah ajulikanae kwa " Al-Assam" Allah Subhanahu
Wataala Amrehemu. Hao wamechukua dini
yao kwa waadilifu wa karne ya sita nao ni mwanachuoni mkubwa Al-Khudhr bin
Suleiman babu wa Ahmed bin Al-Nadhr alietangulia kutajwa, sheikh Ahmed bin
Abdallah bin Musa, na Sheikh Mohammed bin Ibrahim bin Musa na mtoto wa ami yao
Mohammed bin Musa Al-Kindiy na Sheikh Abu Mohammed Abdallah bin Mohammed bin
Ibrahiim As-Samailiy basi wao wamechukua dini yao kwa waadilifu wa karne ya
tano nao ni mwanachuoni mkubwa Abu Ali Al-Hassan bin Saeed bin Quraysh, na
mwanachuoni mkubwa Salama bin Muslim Al-Utabiy As-Sohariy, na mwanachuoni
mkubwa Mohammed bin Abdallah bin Al-Mufadda Al-Kindiy, na Al-Qadhiy Abu
Abdallah Mohammed bin Essa , na Al-Qadhiy Abu Ali Al-Hassan bin Ahmed
Al-Hajaariy na Mwanachuoni mkubwa Abu Al-Hassan Al-Bisyawiy na hao wamechukua
dini yao kwa waadilifu wa karne ya nne nao ni Imam wa madhebu Abu Saeed bin
Muhammed bin Saeed Al-Kadamiy Al-Naabiy, na Sheikh Al-usuuliy Abu Muhammed bin
Barakah, na Mwanachuoni Mkubwa Abu Muhammed Al-Hawaariy bin Othman na
Mwanachuoni Mkubwa Abu Mohammed bin Abdallah bin Mohammed bin Abi Al-Muathir na
hao wamechukua dini yao kwa waadilifu wa karne ya tatu nao ni: Mwanachuoni
Mkubwa Musa bin Ali, na Mwanachuoni Mkubwa Mohammed bin Mahboob bin Al-ruheil,
na Mwanachuoni Mkubwa Abu Almuathir As-Salt bin Khamis, na Mwanachuoni Mkubwa
Abu jaabir Mohammed bin Jaafar, na Mwanachuoni Mkubwa Basheer bin Mohammed bin
Mahboob na Mwanachuoni Mkubwa Al-Mualliy bin Muniir na hao wamechukua dini yao
kwa waadilifu wa karne ya pili nao ni Al-Rabii bin Habib mwenye kitabu
“Al-Musnad As-Sahiih” ndio marejeo ya madhehebu ya Ibadhi katika hadithi .Na
wachukuaji wa elimu walioichukua kuipeleka Oman nao ni watano mashuhuri nao ni
Mahboob bin Al-Ruheil bin Saif bin Hubeira na Saif babu yake mpiganaji katika
wapiganaji wa Mtume wa Allah -rehema za Allah na amani zimshukie, na Al-Munir
bin Nayer Al-Jaalaaniy Al-Riyamiy, na Mohammed bin Al-Maaliy Al-Kindiy, na Bashiir bin Al-Mundhir An-Nizwaniy, na Musa
bin Abiy Jabir Al-Azkaaniy na mamia wa wanavyuouni wakubwa kama mfano wa hao
waliotajwa : Kahlan bin Attia Qadhi wa Imam Al-Julandiy bin Masood na
wale waliokufa mashahidi pamoja na Imam hapo Galfar. Basi ni za Allah hizo
nafsi zilizosafika ambazo haziwezi kutiliwa shaka katika ukweli na uikhlasi
wake. Allah Azirehemu roho Hizo na Azikirimu kwa kuzipa fadhila zake na daraja
kubwa.
Na kadhalika hao wamechukua ilimu yao
kutokana na waliowatangulia waliokuwa wenye heshima, waadilifu wa karne ya
kwanza ambayo ni bora ya karne zote nao ni: Jabir bin Zayd “Abu As-Shaathaa”
katika Matabiin wanaotegemeka kabisa rafiki wa Al-Hassan Al-Basriy na Mazin
bin Ghudhuba As-Saadiy As-Samailiy naye ndie alichukua habari za bishara njema
za Utume wa nabii Muhammed -rehema za Allah na amani zimshukie- kuwafikishia
watu wa Oman, na Saif bin Habiira Mpiganaji wa mtume Muhammed -rehema za Allah
na amani zimshukie, na Abd na Jeyfar watoto wa Al-Julanda Wafalme wa Oman, na
Jaafar bin khathm Al-Atkiy na Abu Safra Saarif bin Dhaalim, na Sohar bin
Al-Abbas Al-Abdiy, na Al-Qaadhiy Ka’ab bin Suur. Na wale waliochukua elimu
katika karne hii ambao watu wa Oman wamechukua kutoka kwao ni Abu Obaidah
Muslim bin Abi Karima Al-Tamimiy, na Abdallah bin Abadh ambaye kutokana naye
imepewa jina Madhebu hii ya maridhiya ya “Ibaadhi” na huyu Abdallah bin Abadh
ni Imam wa siyasa wa kiibadhi sio Imam wa elimu ndio maana hukuti athari yake
yoyote ya kutunga vitabu. Anasema Sheikh wetu Noor Addiin As-Saalmiy, Allah Subhanahu
Wataala Amrehemu, katika shairi na yafuatayo ni maana ya hilo shairi:
“Sisi Maibadhi
hakutuwekea madhehebu hii mwana wa Ibaadh tuifuate ndio maana hukuti katika
vitabu vyetu masala yake hata moja imeandikwa. Basi sisi katika Asili na katika
matawi tuko katika njia iliokuwa juu kabisa ya salafu (Masahaba). Kwa hiyo
twachukua haki pale tunapoiona hata kama kaileta mtu tunaemchukia na baatili
twairudisha hata kama imeletwa na rafiki
anaependwa kwetu. Na tunaokhalifiana nao (katika medhebu nyingine) wao ndio
waliotwita jina hili la Ibadhi na sisi tumeridhika nalo (hatukulipinga)”.
Na wa kwanza katika hao waliokwisha kutajwa
ambao Maibadhi wamewategemea katika utowaji wa hadithi ni Jabir bin Zayd. Kwa
ajili ya uaminifu wake ametegemewa na hatiliwi shaka katika utowaji wake wa
habari na yoyote yule akiwa ni Muibadhi
au sio Muibadhi, na wamemsifu wengi katika waliotunga vitabu na kama
walivyomhusudu wengi wamejua uadilifu wake lakini juu ya hivyo hawamtaji katika
vitabu vyao kama ilivyokuja katika mithali “Twakuona na wewe si chochote”. Na
Imam Jabir kama alivyokuwa mashuhuri katika vitabu vya sira kuwa amewawahi
(amewakuta) Masahaba Sabini waliopigana katika vita vya “Badr” basi inatutosha
kuwa masahaba wengine aliowakuta walikuwa wengi sana . Katika mashekhe wake wakubwa
(aliochukua elimu kwao) ni Abdallah bin Abbas na Bibi Aisha Mama wa waumini
Radhi za Allah ziwe juu yao .
Inasemekana kuwa si chini ya masahaba khamsini alichukuwa elimu kwao baina yao
Anas bin Malik, Abu Ayoub, Abu Hurairah na wengineo wengi. Na hapana shaka
yoyote kuwa alichukua elimu kutoka kwa Masahaba Radhi za Allah ziwe juu yao yaani amechukua katika chanzo kilichokua safi kabisa bila ya
wasiwasi wala shaka yoyote. Basi pima ewe uliokuwa na akili wapi penye haki
zaidi kuchukua penye chombo safi
kilichokuwa hakikuchafuliwa au penye chombo kilichopita katika mikono mingi na
kurambwa na ndimi na kikaingiliwa na wale wenye uwezo wanaofuata mapendekezo ya
nafsi zao baada ya kitambo cha wakati? Basi insaaf (kupima mambo kwa haki) ni tabia ambayo Allah
Subhanahu Wataala huipenda kwa hivyo ukitumia Insaaf utaona kile chombo cha
kwanza ndicho moyo unapotumaini na nafsi kuridhia. Basi baadhi ya wana historia
wasema: “Maibadhi madhehebu yao katika ukweli na uaminifu ni madhehebu ya Abu
Bakr Al-Siddiq, na madhehebu yao katika mkazo na uongofu ni madhehebu ya Omar
bin Al-Khattab na Akida yao ni Akida ya Mtume wao Muhammed -rehema za Allah na
amani zimshukie- hawako tayari kubadili dini yao kwa ajili ya dunia wala
hawawafanyii uadui waislamu wala hawajibagui (wawa pamoja nao) na Waislamu na
humsifu Allah Subhanahu Wataala kwa sifa zake zilizokamilika na zilizo bainika
(zilizokuwa wazi ambazo hazipingani na utukufu wake Subhanahu Wataala).
Wamtukuza Allah Subhanahu Wataala na kumyanyua kutokana na kila aina ya
upungufu na aibu. Msingi wa dini yao ni kitabu (Qur’ani) na Sunna ya Mtume
-rehema za Allah na amani zimshukie- na utegemeo wao kwa vitu hivi viwili ni
wenye nguvu kabisa bila ya kulainika kisha vile vile wanategemea Ijmaa na kutenda
kwa mujibu wake kisha wachukulia rai katika mambo waliyokhtilafiyana nayo
Waislamu na hawamridhii mtu yoyote yule atakapo pinga njia ya Waislamu basi
hata akiwa yeye nani au daraja yake iko vipi.
Kuelezea kwa ufupi juu ya Maimamu wa Oman
Hazikufanikiwa madhehebu nyingine za
kiislamu kutawala katika msingi wa kitabu (Qur’ani) na Sunna kwa njia ya
Makhalifa walioongoka kama walivyofanikiwa
Maibadhi. Akitaka mwenye kupenda haki na Insaf basi asome tarekhe na ataona
ukweli wa haya tuliyoyasema. Ndio wao wanao watawala wamewaita “Maimamu” basi
twamshukuru Allah Subhanahu Wataala kwa mafanikio yake.
1)
Imam Al-Julanda bin Masood bin Muawala bin Shams:
Huyu ni Imam wa kwanza aliochaguliwa Oman
katika mwaka 132 H na alikuwa katika wafalme wa Oman baada ya watoto wa Malik
bin Fahm na alikuwa amezungukwa na wanavyuoni wakubwa na hautoshi ufupi wa
maelezo haya kuwataja hao wanavyuoni, na huyu Imam ametawala muda wa miaka
miwili na mwezi mmoja na amekufa shahidi yeye pamoja na maaskari wake elfu kumi
wameuliwa na maaskari wa mmwagaji damu wa utawala wa Ki-Abbasi ambaye Allah Subhanahu
Wataala kamsaliti na maradhi ya ndui akafa huko Al-Anbar.
2)
Imam Al-Warith bin Kaab Al-Kharusiy naye anatoka
Al-Hijaar, Wadi Baniy Kharus:
Siku moja kasikia sauti haijui itokapo wala
nani mwenyewe yamwambia asimamishe uadilifu (atawale kwa sharia ya kiislamu
kutumia kitabu na Sunna). Basi akachaguliwa na waislamu kutawala na kipindi
chake kimechukua miaka kumi na mbili na miezi fulani, kwani alichaguliwa mwaka
179 H na akafa mwaka 192 H na sababu ya kifo chake alizama katika ‘Wadi Kelbuu’
huko Nizwa iliosabibishwa na mvua na vile vile walikufa pamoja na yeye masahibu
zake sabini wakati alipoona mkondo wa maji unawaendea wafungwa, kwani jela ilikuwa
kando ya wadi, akasema hawa ni amana yangu na mimi nitaulizwa kesho juu yao
basi akajitupa katika wadi ili kuwaokoa yakawashinda nguvu maji yeye pamoja na
wenzake Rehma za Allah Subhanahu Wataala ziwe juu yake.
3)
Imam Ghassan bin Abdallah Al-Yahmadiy kutoka Al-Fajah:
Amechukua Uimamu baada ya kufa kwa Imam
Warith moja kwa moja bila ya kuchelewa katika mwaka 192 H naye ni wa kwanza
aliyohami bahari kutokana na maharamia wa bahari wa kihindi waliokuwa
wakiwatisha na kuwatia khofu watu katika bahari. Basi akawapelekea askari wake
wakawashinda kwa hivyo ikawa ndio mwisho wa uharibifu wao baharini. Jeshi la
bahari la Omani
liliokuwa na Idadi kubwa ya manuwari lilikaa macho kila linaposikia kuna
maharamia baharini linakwenda kuwahujumu na hatimaye wakawafukuza kabisa kutoka
pwani ya bahari ya Oman .
Katika wakati wa Imam huyu ndipo yalipohamishwa makao makuu ya serikali kutoka
Sohar kwenda Nizwa baada ya kukubaliana wanavyuoni waliona maslaha juu ya
kitendo hicho. Naye ni wa kwanza aliyekata mkono kwa kosa la kuiba huko Sohar. Alitawala miaka
kumi na tano na miezi saba kwa uadilifu. Aliumwa siku ya Jumatano tarehe 22
Dhil-Qe’edah na akafariki usubuhi wa Jumapili katika mwezi huo huo kabla ya
kumalizika mwaka 207H kwa siku nne. Allah Subhanahu Wataala amrehemu.
4)
Imam Abdil Malik bin Humaid katokana na Bani Ali bin Sawda bin Ali bin Omar bin Aamer
Al-Alawiy Al-Uzdiy:
Amechaguliwa kuwa Imam mwaka mmoja baada ya
kufa aliyomtangulia katika Shawwal mwaka 208 H. amechaguliwa katika msingi ule
ule aliyochaguliwa Ghassan na kabla yake Al-Warith na Al-Julanda na kabla yao
makhalifa walioongoka na msingi wenyewe ni kuamrishana mema na kukatazana
mabaya na kuiuza nafsi kwa ajili ya Allah Subhanahu Wataala na kupigana na
waasi wa Imam (yaani waliotoka nje ya utiifu wake). Amesema Imam Noor Ad-diin:
“Iligeuka Oman katika wakati wa Imam huyu ikawa bora kuliko nchi zote za Allah Subhanahu
Wataala Wakati alipozeeka Imam waislamu wakaigopea nchi yao kupotea basi hapo
ndipo alipochukuwa hatuwa Musa bin Ali ambaye ndiye aliyekuwa marejeo ya
wanavyuoni wakati huo ya kumsaidia mpaka alipokufa siku ya Ijumaa katika mwezi
wa Rajab mwaka 226H Allah Subhanahu Wataala Amrehemu. Ulidumu uimamu wake miaka
18 na siku saba.
5)
Imam Al-Mohanna bin Jeifar Al-Yahmadiy:
Imam mkubwa kuliko maimam wote wa jamii hii
ya Al-Yahmad, ukubwa wa dini na dunia. Alikuwa akiitwa mwenye nabu (magego)
kwani alikuwa akikasirika hutokeza meno yake na huenda baadhi ya walio karibu
yake wakafa kwa heiba yake. Kachaguliwa siku ile ile aliokufa yule Imam
aliyomtangulia nayo ni siku ya Ijumaa tarehe 3 mwezi wa Rajab mwaka 226H. Na
alikuwa haingii mtu yoyote kwake isipokuwa ana silaha na hakuwa mtu yeyote
akizungumza katika majlis yake. Alikuwa amekusanya baina ya nguvu ya bara na ya
bahari na ikafikia nguvu hii kiwango kikubwa sana . Zilifika manuwari mia tatu za vita,
ngamia mia saba na farasi mia sita. Nguvu hii ilipatikana bila ya kuchelewa
katika mwito wa mwanzo wa vita. Alifariki Imam huyu Allah Subhanahu Wataala
amrehemu siku ya Ijumaa tarehe 16 mwezi wa Rabii Athaniy mwaka 237H, baada ya
kutawala miaka kumi na moja kasoro miezi michache. Na alikufa kabla yake sheikh
wa kiislamu Musa bin Ali katika Rabii Al-Awwal mwaka 230H na aliathirika sana Imam kwa kifo chake,
Allah Subhanahu Wataala awerehemu wote.
6)
Imam Assalt bin Malik bin Balarab Al-Kharusiy:
Amechaguliwa katika siku ile ile aliyokufa
aliyekuwa kabla yake siku ya Ijumaa 16 Rabee Al-Aakher mwaka 237H. Miongoni mwa
wanavyuoni wakubwa waliomchaguwa ni
Mohammed bin Mahboob. Katika maimamu wote hakuna aliyeishi muda mrefu zaidi
katika utawala kama Imam Assalt, alitawala mpaka akazeeka wakachoka nae raia
zake na ukweli athari ya uzee wake ilionyesha katika miguu yake lakini maskio
yake, macho yake, akili yake na ulimi wake vyote hivi havikupata upungufu
wowote. Imam huyu ndiye yule mwenye ile karama wakati mwanamke fulani huko Socatra
alikuwa akiomba msaada kwake akaandika barua kisha akaitia ndani ya kipande cha
bomba akakitumbukiza baharini basi ikahifadhika na kwenda masafa marefu katika
bahari mpaka ikamfikia Imam huko Sohar. Mwanamke huyu kabila yake ni Jahdhamiy
katika watu wa Samad Asshaan, alikuwa huko Socatra wakati lilipotokea lile
tukio maarufu katika historia ambalo lilisababisha watu wa Oman kufarikiana katika makundi
matatu (rejea siira) akatoka Imam kutoka nyumba ya Uimam katika tarehe 3 Dhil
Hijja mwaka 272H baada ya kutawala miaka thalathini na tano na miezi saba.
7)
Imam Rashid bin Annadhar Al-Yahmadiy:
Naye ndiye aliyesimama pamoja na Musa bin
Musa na wenzao wengineo kumtoa Imam Assalt kutoka katika Uimamu.
Walipomwingilia Imam Assalt akatoka kuiwacha nyumba ya Uimamu bila ya kugoma au
kufanya upinzani wowote, baada ya kutoka tu huku nyuma wakafanya uchaguzi wa
Imam mwingine na ndio alipochaguliwa huyu Imam Rashid na ilikuwa katika siku ya
Alkhamiis tarehe 3 Dhil Hijja mwaka 272H. na katika kipindi chake hichi cha
utawala kulitokea fitna nyingi sana na wakauliwa watu wengi sana hata mwisho
ikabidi waivamie nyumba ya Uimamu
wakamkamata na kumtoa humo baada ya kupita miaka minne na siku khamsini
na nane katika utawala na wengi katika watu wa Oman walikuwa hawako radhi nae
na kukhitilafiana kulikuwa kwingi sana Allah Subhanahu Wataala pekee anajua
ukweli na haki iko wapi. Na kwa sababu ya fitna hizi wakagawanyika watu wa Oman
makundi mawili. Kundi la
Nizwaniyah likiongozwa na Imam Abu Saeed Al-Kadamiy na Kundi la Rustaqiyah likiongozwa
na Imam Abu Mohammed ibn Barakah na juu ya tukiyo hili ametunga Imam Abu Saeed
kitab “Al-Istiqamah”.
8)
Imam Azzan bin Tameem Al-Kharusiy:
Amechaguliwa kuwa Imam siku ya Jumatano
tarehe 3 mwezi wa Safar mwaka 277H. na katika wakati alipotawala vimetokea vita
vingi vya kupigana Wa-Omani wenyewe kwa wenyewe. Katika hivi ni vile vita vya
Izki ambavyo aliuliwa Musa bin Musa na vile vile vita vya Alqaa katika Sohar
ambavyo waliuliwa wengi katika watu mashuhuri Oman . Na asili ya vita hivi vyote
ni watu wa “Jarnan” mpaka ikawa inasemwa (Haitokei fitna Oman isipokuwa asili yake ni Jarnan) .Na
vikasababisha vita kuingiza shari Oman
na watu kukimbia kwenda Bahrain
na huko kuna yule mtu anaeitwa Mohammed bin Noor (wakaipindua watu wa Omani
badala ya Noor wakamwita Boor). Wakaweza kumchota kwa maneno yao matamu na
akawakubalia kuwasaidia hapo akenda na jeshi lake Oman lililokuwa na wapiganaji
25,000 na farasi 3,000 na akaleta uharibifu mkubwa Oman kwani aliua maelfu na
kufukia mito ya maji, akaunguza vitabu, akakata mikono, akasababisha masikio
yapate uziwi na macho yapate upofu, mwishowe akauliwa Imam Azzan bin Tameem
huko Samad As-Shaan mwaka 270H. ukawa umedumu Uimamu wake miaka mitatu.
Baada ya Imam Azzan wakateuliwa Oman maimam wanane ambao haikujulikana vizuri
tarehe yao baadhi yao wamejiuzulu wenyewe na
baadhi yao wametolewa na wengine wameuliwa na
kadhalika ikaendelea hali hiyo ya kivita Oman na kutokuwa na utulivu mpaka
Allah Subhanahu Wataala aliekuwa kareem akaleta neema yake kwa kumleta:
17) Imam Saeed bin Abdallah bi Mohammed bin
Mahboob Al-Ruheiliy Al-Qurashiy:
Na familiya hii ya Al-Ruheiliy ilikuwa na
mahala pakubwa baina ya wanavyouni wa Kiislamu. Familia iliyobarikiwa inafuatia
Istiqama kutoka kwa waliopita nyuma (wazee) kwenda kwa vizazi vyao na babu yao
ni Seif bin Hubeira mpiganaji wa Mtume Mohammed -rehema za Allah na amani
zimshukie- na kuchaguliwa kwa Imam Saeed kulikuwa katika mwaka 320H. naye ni
katika wale waliokubaliana waislamu katika Uimamu wake na kutawala kwake kwani
hakuna aliempinga au kumtolea kasoro yoyote ile hata wakasema baadhi ya
wanavyuoni wa siku zake kuwa hatujui imamu yoyote katika maimamu wa waislamu
waliotawala hapa Oman
aliekuwa bora kuliko Saeed bin Abdallah isipokuwa Al-Julanda bin Masood.
Amesema Imam Noor Ad-diin: “Simweki sawa
Imam yoyote Oman
na Imam Al-Julanda kwani yeye amejumuisha sifa tatu nazo ni elimu, uadilifu na
shahada (kufa shaheed). Na kwa Imam huyu (Saeed bin Abdallah) Allah Subhanahu
Wataala amemdhalilisha Yousuf bin Wajeeh na wasaidizi wake wa dola ya
Al-Abassiya nao ndio waliobakia katika askari wa Ibn Boor basi wakatoka Oman hali
ni dhalil na wala waislamu hawakuhalalisha kitu katika mali zao wakati wa
kufukuzwa kwao hata pete ya reza ya mlango ilipotea basi Imam akawaadhibu wale
walioichukua na wakairudisha kwa wenyewe. Tizama huu uzuri na ukarimu kwa ajili
ya Allah Subhanahu Wataala” Alikufa Imam shaheed katika mwaka 328H. na ulikuwa
Uimamu wake miaka minane rehema na ridha za Allah Subhanahu Wataala ziwe juu
yake.
18) Imam Rashid bin Al-waleed Al-Kindiy:
Alikuwa katika upande wenye nguvu wa uchaji
Mungu na mahala pa juu pa uongofu. Amemsifu Imam Abu Saeed huyu Imam Rashid kwa
sifa nzuri na za ajabu. Amesema Imam Noor Ad-diin : Inakutosha kujua hali nzuri
ya yule mtu anaesifiwa na Abu Saeed sifa kama
hizi. Na watu ni mashahidi wa Allah Subhanahu Wataala katika ardhi yake. Kisha
akawaingilia fattan wa Iraq na jeshi lake kubwa akaiteka Oman kwa msaada wa
watu wake na kwa ubaya wao kwa Imam wao basi akajitenga Imam kwenda mahala
palipo magharibi ya Jabal Akhdhar, akaishi huko kama alivyojaliwa kuishi mpaka
kufa kwake naye yu katika hali ya kusifiwa. Tarehe ya kufa kwake haijulikani
isipokuwa imeandikwa katika “Bayaan Asshara” kuwa Oman
iligeuka kuwa nchi ya Ukafiri na Unafik katika mwaka 342H na wakti huu ndio
hapo ilipotekwa Oman .
Msaada wote ni kutoka kwake Allah Subhanahu Wataala Amesema Sheikh Salim bin
Hmood Assiyabiy: “Imepita karne hii nayo Imetandwa na mawingu ya dhulma na
ufisadi kutokana na hawa wasaliti wa Bani Abbas juu ya Umma wa kiislamu na
walikuwa kama waliowatangulia yaani Bani Umayya balaa na shari kubwa kwa Umma
wa kiislamu. Allah Subhanahu Wataala ndio mtoshelezaji wao na wetu (waislamu).
19) Imam Al-Khalil bin Shadhaan bin Salt
bin Malik Al-Khrusiy:
Kwake ndio
limenasibishwa kabila la
Al-Khaliliy katika Oman
nalo ni kabila muhimu sana katika Oman , mtiririko unaofatana kama
mtiririko wa kabila la
Ar-Ruheiliy. Ilibakia Oman na watu wake yachezewa na watu
majabari mpaka Allah Subhanahu Wataala akajalia kuja huyu Imam Al-Khalil ambaye
alichaguliwa kuongoza katika mwaka 444H. akenda baina yao mwendo mzuri na kuwalinda kutokana na
majabari na kwa uadilifu wake ikawa amani katika nchi na wakastarehe katika
utawala wake waja. Alifikiwa na Imam Abu Is-haq Al-Hadhramiy kutoka Hadhramaut
kwa kumuomba msaada amsaidie kupigana na watu wa Yemen
na Hadhramaut katika wale waliotoka katika utiifu wake basi akamsaidia kwa mali
na watu mpaka akaweza kuweka Imara nguzo za uimamu na akamsifu Imam Abu Is-haq
Imam Al-Khalil katika kasida zake zilizomo katika Diwani yake maarufu.
Yakatokea mambo makubwa katika wakati wake pamoja na kuhujumiwa na maadui
lakini alifanikiwa kuwashinda na kuleta hali nzuri mpaka Allah Subhanahu
Wataala alipomchukuwa katika rehma yake na radhi zake katika mwaka 462H baada
ya kuongoza miaka 18.
20) Imam Rashid bin Saeed Al-Yahmadiy:
Amechaguliwa kuwa Imam baada ya Imam
Al-Khalil naye vile vile amemsaidia Imam Al-Hadhramiy (Imam wa Yemen na Hadhramaut) kwa mali na kwa watu kama
alivyofanya aliyekuwa kabla yake Imam Al-Khalil. Na ameandika (Imam
Al-Hadhramiy) juu yake (Imam Rashid) kasida za kumsifu katika diwani yake.
Akawakusanya wanavyuoni katika wakati wake wakaweka kikomo cha mushkila wa
Assalt na Musa na hapo ndipo walipokubaliana kuwa yeyote aliesikia juu ya kosa
lililofanyika na kumjua alietenda hilo kosa ni juu yake kumkata au kuachana
naye (kumchukia kwa ajili ya Allah Subhanahu Wataala na kutomwombea Rehema na
Maghufira) na ikiwa haelewi hukumu ya kosa hilo juu yake kuuliza na akishaeleweshwa hukumu yake basi ni wajibu
wake kumkata huyo mkosa na anayetilia shaka hukumu hiyo huyo amehiliki.
Akabakia Imam huyu maridhiwa hata kufa kwake huko Nizwa. Rehma za Allah Subhanahu
Wataala juu yake.
21) Imam Hafs bin Rashid bin Saeed
Al-Yahmadiy:
Alibakia katika uimamu muda mrefu lakini
haikupatikana tarekhe yake kujulikana lini amechaguliwa na lini amekufa. Kila
ajali imeandikwa na Allah Subhanahu Wataala.
22) Imam Rashid bin Aliy Al-Kharusiy.
Amesema Imam Noor
Ad-Diin: “Hatukupata kujua tarehe ya kuchaguliwa kwake lakini kinachojulikana
kuwa alikuwa Imam mwema wamemshukuru raia zake na umma wa Kiislamu kumhimidi
kwani alikuwa mnara wa uadilifu na amekufa mwaka 513H.
23) Imam Amir bin Rashid bin Al-Waleed
Al-Kharusiy:
Alikuwa mtu mwenye elimu na alikuwa zaahid
(hakuchukuwa katika dunia isipokuwa cha dharura) mwenye akili na maarifa anawatendea
mema raia zake na alikuwa Imam aliyeuza Dunia yake kwa ajili ya Allah Subhanahu
Wataala (Imam As-Shari) naye ni katika maimamu wa Bani Kharus wa As-Shari wa
mwisho na akasimamiya haki mpaka mwisho wake. Rehema za Allah Subhanahu Wataala
ziwe juu yake. Amechaguliwa kuwa Imam
katika mwaka 576H. Wakati wa kufa kwake haukuhifadhiwa wala wa kubakia
kwake katika uimamu kama ilivyokuwa haikuhifadhiwa tarehe ya Imam wa kumi na
tano Mohammed bin Ghassan bin Abdallah Al-Kharusiy na alikuwa Imam wa difaa na
alikuwa katika uimamu wake muadilifu hakumkosoa kitu mtu yeyote katika wakati
wake wala kupinga katika hukumu zake mpaka Allah Subhanahu Wataala kumchukuwa
kwake. Rehema za Mola Subhanahu Wataala ziwe juu yake.
24) Imam Al-Khalil bin Abdallah bin Omar
Al-Khaliliy:
Katika watoto wa Salt bin Malik na
hakutolewa makosa katika uwongozi wake mpaka Allah Subhanahu Wataala akamfisha
naye yu hali ya kunyooka katika njia ya haki. Naye ni katika maimamu waliokuwa
tarehe zao hazijulikani. Utawala wa kiabbasi ulikwisha kwa kumalizika karne ya
sita Hijri na hapo ndio ilipotoweka dola yao na
ikapumzika ardhi kutokana nao na wala mbingu haikuwalilia (kwa mambo yao yalivyokuwa mabaya). Oman
nayo ikapumua kwa kupumzika na dhulma zao. Sifa zote na shukrani azistahiki
Allah Subhanahu Wataala Lakini kwa ajili ya maovu ya wale watu wabaya wa Oman na kupigana kwao wenyewe kwa weneywe na
kugawanyika, Allah Subhanahu Wataala akawasaliti juu yao
madhalimu wengine kutokana na wao wenyewe wakawaonjesha adhabu iumizayo kwani kama vile mlivyo ndivyo mnavyotawaliwa. Tazama hikma ya
Mola Subhanahu Wataala kwani Bani Abbas walitawala muda wa miaka mia tano kesha
wakadhalilishwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala baada yake. Kama ilivyokuja
zamu ya Al-Yaariba baada ya miaka mia tano mingine wakawan’goa majabari
kutokana na dhulma yao wakaijaza Oman uadilifu kama
ilivyokuwa imejazwa udhalimu na katika kipindi hichi akachaguliwa Imam:
25) Imam Al-Hawari bin Malik.
Amechaguliwa mwaka 809H na akasimama katika
wajibu wa sharia na akafanya kwa uwezo wa nafsi yake kuleta uadilifu. Alifariki
mwaka 833H baada ya kutawala kwa miaka ishirini na tatu. Na wakamchagua:-
26) Imam Malik bin Al-Hawari.
Alikuwa mwenye kushukuriwa kwa mwendo wake
mzuri lakini hakudumu zaidi ya mwaka mmoja katika uimamu wake kisha
akachaguliwa Imam:-
27) Abu Al-Hassan bin Khamis bin Aamer:
Katika mwezi wa
Ramadhani mwaka 839H. na akadumu katika uimamu mwaka mmoja basi kisha Allah Subhanahu
Wataala akaleta kwa fadhli zake mtu shujaa mwenye nguvu akawa imara mbele ya
watu waovu. Na huyo ni:
28) Imam Omar bin Al-Khattab:
Namna alivyowahujumu madhalimu mfano wake
ni kama Simba anaehujumu, basi Allah Subhanahu Wataala akampa ushindi juu yao na akamrithisha ardhi yao
na nyumba zao akatoa amri zichukuliwe mali zao na Bait al Maal.
Amechaguliwa Imam mwaka 885H kisha wakatawala kiasi maimam watano katika
kipindi hichi lakini walikuwa madhaifu na wakaonewa na watu majabari mpaka
alipokuja kutawala mtu mwenye ushujaa na uadilifu:
29) Imam Mohammed bin Ismaeel Al-Haadhriy:
Ametokana na Qudhaa bin Malik bin Himyar.
Allah Subhanahu Wataala kaujaza moyo wake Imani na akautia nguvu na akampa
msaada kwa ushindi kutoka kwake Mola Subhanahu Wataala na akagharikisha mali
za wale waliowasaidia majabari. Amechaguliwa Imam mwaka 906H na akabakia katika
hali hiyo mpaka mwaka 942H kwa hivyo umedumu uimamu wake miaka thalathini na
sita kisha akachaguliwa mtoto wake baadaye:
30) Imam Barakat bin Mohammed bin Ismaeel:
Amechaguliwa baada ya kufa kwa baba yake na
akafata njia yake hata alipokufa mwaka 964H baada ya kutawala miaka ishirini na
mbili. Na ulikuwa uimamu wa maimamu wawili hawa kitenganisho baina ya vipindi
viwili vya utawala wa dhulma na ukandamizaji ambao baada ya kuweko utawala
mbaya hapo mwanzo ulikuja tena baada ya hawa maimamu wawili waadilifu. Hawa
watawala waliohukumu kwa dhulma ni Bani Nabhan. Katika kipindi hichi cha
utawala mbaya walitokea maimamu waliotawala lakini hawakudumu sana kwani
hawakuweza kuvumilia dhulma iliyoenea wakti huo. Basi Bani Nabhani walitawala
na utawala wao ulikuwa wa ukandamizaji, vitisho na kufanya maafa makubwa kwa
viumbe vya Allah Subhanahu Wataala na mwishowe wakapigana wenyewe kwa wenyewe
na wakati wao umefunikwa na vumbi la dhulma mpaka Allah Subhanahu Wataala
akajaalia kumleta Oman:
31) Imam kiongozi Nasser
bin Murshid Al-Yarubiy:
Akarudisha tena sira ya watu wema waliopita
katika Oman. Akaleta upya mwendo mzuri wa kinabii ukiwa umevikwa taji ya Imani,
mwendo ambao ulitoweka kabisa kwa sababu ya udhalimu uliokuwa hapo nyuma. Ikawa
Oman kwa kuja kwa Imam huyu kama kwamba imezaliwa upya na, Allah Subhanahu
Wataala akamsaidia kwa kumuwekea watu
wazuri mfano wake(huyo Imam) katika kutenda mema, uchaji Mungu, wivu
katika dini na maarifa. Naye alifanikiwa kufanya mengi mazuri, ambayo
hawakufanya wenzake kwani aliwatoa Wareno (wa-Portugizi) Oman na akaisafisha kutokana nao.
Na watu waovu na maasi wa Oman wenyewe wakajaribu kumpiga vita lakini
aliwashinda basi yakanyooka mambo na akafariki - Allah Subhanahu Wataala
amrehemu - katika hali Waisilamu wako
radhi nae na umri wake zaidi ya miaka arubaini. Ametawala kutoka mwaka
1024-1050H. kwa hiyo umedumu uimamu wake miaka 26 kisha akachaguliwa mtoto wa
Ammi yake:
32) Sultan bin Saif wa kwanza:
Amechaguliwa katika siku ile ile aliokufa
Imam Nasser naye alikuwa askari kiongozi wa Imam Nasser na alikuwa chini yake
na katika wakati wake aliwafukuza Wareno na akafungua mji wa Sur na vile vile
nchi nyingi zilizokuwa zimemilikiwa na India . Kadhalika aliwafukuza hawo
Wareno kutoka Mombasa , Kilwa, Zanzibar , Yemen
na nchi nynginezo zilizokuwa zimefunguliwa. Akaishi na hali raia wako radhi nae
mpaka kufariki kwake siku ya kumi na sita ya Dhil-Qeeda 1091H. ulidumu uimamu wake miaka arubaini na
moja. Basi ni ya Allah Subhanahu Wataala miaka hii nini ukubwa wa baraka zake
na nini wingi wa harakati zake katika mashariki ya dunia na magharibi yake na
kusini kwake …… na kama hivyo. Naye ndiye aliyejenga ngome ya Nizwa
iliyonyanyuliwa juu, na yenye msingi wenye nguvu na iliokuwa tabu kupatikana na
maadui. Kisha akachaguliwa Imam:
33) Balarab bin Sultan bin Seif
Alikuwa amepambwa na tabia nzuri na fadhila
za kupendeza na vitendo vizuri (vyema). Aliona kuwa Oman imejaa mambo mengi mazuri
isipokuwa ilipungua katika upande wa kufundisha sharia basi akajenga ngome ya
Jibriin ilio na mandhari ya ajabu, iwe madrasa watoke wanavyouni humo ambao
watajaza hizo sehemu zilizokuwa tupu zinahitajia watu wasomi. Ameijenga kwa
mamilioni ya pesa kitu kinachoonesha utajiri mkubwa uliokuwapo wakati huo.
Kadhalika alihifadhi humo ndani pesa zilizofika kiwango kama hicho ambazo
zilikuwa zitumiwe wakati wa haja. Uhodari uliotumika katika ujengaji wa ngome
hii ni wa kustajaabisha na ingalipo mpaka leo. Limerudishiwa kutengezwa katika wakati
huu kwa amri ya Sultan Qaboos. Amechaguliwa Balarab kuwa Imam mwaka 1091H na
akatawala hadi mwaka 1104H kwa hivyo alidumu katika uimamu miaka 13.
34) Imam Seif bin Sultan bin Seif.
Ameitwa kwa jina la “pingu ya ardhi”
amesema Sheikh Salim bin Humood: “Usifikirie kuwa hili jina la pingu ya ardhi
amepewa bure bila ya sababu nalo ni jina kubwa alilopewa kwani ametikisa upeo
wa mashariki mpaka sehemu za mbali za Afrika n.k.”. Ameunda majeshi kwa
kujiweka tayari kwa vita, hata ikiwa katika mgutio wa mwanzo wa vita farasi
elfu tisini na sita 96,000 wako kando yake tayari. Akaingia na jeshi hili India na kuichukua pwani yake kisha akaingia
katika ‘Rasi ya Matarajio Mema’ (Cape of Good Hope) hapa ni pale inapokutana
bahari kubwa ya Atlantic na bahari ya India . Ametengeza mifereji mingi
Oman. Naye amechaguliwa siku ile ile aliekufa ndugu yake mwaka 1104H na
akatawala muda wa miaka 19 na kifo chake kilikuwa tarehe 3 Ramadhani mwaka
1123H siku ya Ijumaa. Nasema: “Maimamu hawa wanne wamekamilisha miaka mia wakaijaza
nuru Oman
na kuitengeza kwa uadilifu (usawa) na kwa majengo wakaifanya kuwa pepo ya dunia
Allah Subhanahu Wataala awalipe kila la kheri na Pepo zilizokuwa upana wake ni
Mbingu na ardhi”.
35) Imam Sultan bin Seif bin Sultan.
Ajulikana kwa Sultan bin Seif wa pili.
Amekuja Oman
na hamu yake aigeuze iwe kama mabustani mawili
ya “maarib” naye ndiye mwenye kauli mashuhuri: “Akiniweka Allah Subhanahu
Wataala hakika nitamfanya msafiri wa Al-Hajji atoke bila ya kuchukuwa zaad
(chakula na mahitajio mengine).” Nikasema: wakati huo alioutamani ni huu wakati
wetu wa karne ya kumi na tano. Amechaguliwa kuwa Imam siku aliokufa baba yake
mwezi wa Ramadhani mwaka 1123H na akafariki siku ya Jumatano tarehe tano Jumadi
Al-Akhera mwaka 1131H na umedumu uimamu wake miaka saba na miezi tisa na kwa
kufa kwake ikaingia shari Oman na wakahuisha ujahiliya na wakataka kuufanya
utawala wa nchi mirathi ya kurithiana.
36) Imam Mohanna bin Sultan bin Majid
Al-Yaarubiy:
Naye ni katika watoto wa Ammi wa maimamu
waliopita na amemwoa bint wa Imam Seif bin Sultan, na wamemuona waislamu afaa
kuwa Imam wakamchagua katika siku aliokufa alie kabla yake Imam Sultan mwaka
1133H baada ya kutawala miaka miwili.
37) Imam Yaareb bin Balarab bin Sultan bin
Seif:
Katika watoto wa maimamu waliopita
amechaguliwa mwaka 1134H na katika wakti huu wakagawika wa Omani vikundi
viwili: Malghafiriy na Mahinawiy. Walipigana Mohammed bin Nasser Al-Ghafriy na
Khalaf bin Mubarak Al-Hinaaiy. Waliomfuata Al-Ghafriy katika makabila wakawa
Maghafriy na waliomfuata Al-Hinay wakawa Mahinawiy mgawanyiko wa kishetani
uliokuwa na mafanikio makubwa sana
bila ya mfano. Wakapigana kwa ajili ya hayo wakafa maelfu ya wa Omani. Basi kwa
msiba huu mkubwa hakuna isipokuwa tuseme Inna lillah wa Inna Ilaihi raajiuun.
38) Imam Mohammed bin Nasser
bin Aamer Al-Ghaafri:
Huyu ndiye aliyepigana vita na Khalaf bin
Mubarak kwani wanavyuoni wa Oman
waliona katika mtu huyu nguvu na ushujaa wakamchagua kuwa Imam wa Difaa
(Himaya). Amesema Imam Nuru Ad-Diin Assalmiy: “Waislamu waweza wakamchaguwa
Imam wa Difaa mtu asiyekuwa na walaya (Asiyependwa kwa ajili ya Allah Subhanahu
Wataala kwa sababu mwendo wake haukustaqim) ili apate kuwarudi watu wabaya
(wanaotaka kuleta fitna kwa nchi) wanaweza wakaendelea naye baada ya fitna hii
kutoweka ikiwa mwendo wake utastaqim au sivyo wamuondoe na wamchague Imam
mwingine. Amechaguliwa Imam huyu tarehe 7 Muharram mwaka 1137H lakini
hakustarehe kwa vita hata siku moja katika kipindi chake cha utawala. Siku moja
wakakutana yeye na mpinzani wake Khalaf mbele ya mlango wa ngome ya Sohar
wakauliwa wote wawili wakati mmoja. Basi ikapumzika Oman nao lakini haikupumzika na
mwito wao mbaya kwani kila damu inayomwagika kwa ajili ya mwito huu hata baada
ya kufa kwao wabeba wao sehemu ya madhanbi haya.
39) Imam Seif bin Sultan bin Seif:
Mtoto wa Imam wa thalathini na tano na
alikuwa mdogo wakati alipokufa baba yake, hapo ndipo alipochukulia sababu
Mohammed bin Nasser kupigana kwa kuwa huyu ni
Imam hata angali mdogo lazima atawale na asili ya kupigana kwake sababu yake ni
hii. Kisha akachaguliwa yeye mwenyewe badala ya huyo aliyempigania. Lakini
hakuachana nae muda wote aliokuwa akipigana. Baada ya kuuliwa Mohammed bin Nasser alikuwa Seif bin Sultan keshabaleghe basi
wakamchagua wanavyuoni wa zama zake kwa kuepusha mbali michafuko na akastaqim
mwanzo baadae akabadilika basi wakamtoa katika uimamu mwaka 1145H na wakamweka
mtoto wa ammi yake:
40) Imam Balarab bin Hamyar bin Sultan bin
Seif:
Kitu kilichomkasirisha Seif ndipo
alipoifata ile fikra ya watu inayosema: “Bora kukufuru kuliko kukubali
kushindwa” basi akasafiri kwenda Makraan akaja na Mabulushi wamsaidie. Lakini
walishindwa na akenda Iran akaja na Waajemu, wakateremsha jeshi lao Khorfakan
katika mwezi wa Dhul-Hijja mwaka 1149H akaja Imam Balarab kuwahujumu mwezi wa
Muharram mwaka 1150H vikatokea vita baina yao na kumalizika kwa kushindwa Imam
na wenzake na wakapata watu wa Oman mtihani mkubwa kwa hawa Maajemi jinsi
walivyoeneza ufisadi hata huyo aliyowaleta, yaani Seif hakuweza kuwamiliki basi
ikabakia Oman katika idhlali kubwa chini ya hawa Maajemi mpaka ukapepea upepo
wa Imani wakakusanyika wanavyuoni kutoka kila mahala katika mji wa Nakhal
wakawafikiana juu ya Imam:
41)
Sultan bin Murshid Al-Yaarubiy:
Amechaguliwa mwaka 1154H usiku wa kuamkia
Arafa. Akasimamisha haki na kuwa katika nguvu kwa idhini ya Allah Subhanahu
Wataala zikaanguka ngome chini ya utawala wake, akasimama dhidi yake Seif bin
Sultan kama alivyosimama dhidi ya aliye kabla
yake. Lakini alishindwa katika mapambano yote na huo ndio ukawa mwisho wake na
akafa na hali yuko chini ya zimamu ya Maajemi ambao wamefanya Oman vitendo viovu vilivyokuwa havikufanywa
kabla yao . Haya
ni matokeo ya vitendo vya watu wajinga ambao hawajali misiba gani watasababisha
kwa watani wao na nafsi zao. Akafa yeye na Imam Sultan bin Murshid katika
wakati mmoja na Waajemu wanaendelea na ufisadi wao mpaka Allah Subhanahu
Wataala akajaalia kuja kwa shujaa katika Mashujaa wa Oman mwenye nguvu, ushujaa na
mwenye kuwa macho:
42)
Imam Ahmed bin Saeed Al-Busaidiy:
Babu wa ukoo wa kifalme unaotawala sasa Oman .
Akawan’goa Waajemu na kuwafukuza Oman
na kuwafanyia ihsani watu wa Oman .
Kwa hivyo amepata Ahmed bin Saeed kwa wa Oman
mahala pa juu na ikawa daraja yake kubwa mbele yao na kuwa na sauti kwao mpaka akavikika
taji ya haiba ya wafalme. Hapo akamtokea yule Imam wa arbaini Balarab bin
Hamyar baada ya kuwa alijificha siku za nyuma kwa kuwahofu Waajemu, eti sasa
hivi ndio ataka kupigana na Ahmed yakatokea mapigano baina yao yakamalizika kwa kufa kwa Balarab mwaka
1167H. Wakaishi watu katika siku zake katika raha na starehe baada ya kupata
kila aina ya mitihani na balaa. Alichaguliwa kuwa Imam baada ya mchuano mkubwa
na waajemu na watu wa Oman ,
na huko kuchaguliwa kwake kulikuwa baada ya kuuliwa Balarab na akadumu katika
uimamu miaka ishirini na tisa mpaka kufa kwake mwaka 1196H. Baada ya hapo
waliendelea watoto wake kuhukumu mpaka alipochaguliwa:
43)
Imam Azzan bin Qais bin Ahmad:
Mjukuu wa Imam aliye kabla yake, naye
kachaguliwa katika mwaka 1285H siku ya Ijumaa, Ishirini na mbili mwezi wa
Jamaada Al-akhera. Amesema Imam Noor Ad-Diin: “Hakika uimamu wake ulikubaliwa
kwa ujumla (sauti kubwa)”. Akafanya yale yaliyomwajibikia katika kuinusuru
dini, kusimamisha haki, na kuwatia adabu madhalimu. Akaingia katika mapigano
mengi dhidi ya wa Omani na washambulizi wa Najd, akachukua mali za madhalimu na kuzitia katika
“Beit almaal” ya waislamu. Kafanya hivyo baada ya kukubaliana na wanavyuoni wa
zama zake. Akabakia Imam mpaka alipokufa shaheed katika usiku wa nane wa Dhil-Qeeda
mwaka 1287H baada ya kuhukumu miaka miwili na miezi minne na siku kumi na tano
Allah Subhanahu Wataala ampe radhi zake, amin. Alibakia baada kufa kwake muda
wa siku tatu hajazikwa na juu ya hivyo hakubadilika.
44)
Imam Salim bin Rashid bin Suleiman bin Aamer
Al-Kharusiy:
Amechaguliwa tarehe kumi na mbili katika
Jumaada Al-Akhera mwaka 1331H. Alikuwa madhubuti katika hukumu zake na alikuwa
haogopi kwa ajili ya Allah Subhanahu Wataala lawama za yoyote yule. Ameiwacha
dunia (Zaahid) inaonekana nuru katika kiwiliwili chake yungali yuhai. Akasimama
pamoja na haki kuamrisha mema na kukataza mabaya na kuwatia adabu wenye makosa
na ikaendelea Oman
katika wakti wake na ikazidi baraka. Kabakia katika Uimamu mpaka alipokufa
shaheed katika usiku wa tano wa Dhil-Qeeda mwaka 1338H. Ulikuwa uimamu wake
miaka saba na miezi minne na siku ishirini na mbili.
45)
Imam Mohammed bin Abdallah bin Saeed Al-Khaliliy:
Amechaguliwa baada ya kufa aliekuwa kabla
yake kwa siku saba katika Dhil-Qeeda 1338H. Alikuwa ana elimu zaidi kuliko watu
wote katika wakati wake, akatimiza masharti yote yanayotakiwa kwa msimamiaji wa
haki (Mtawala kwa sharia ya Kiislamu) akafanya waajibu wake kadri ya uwezo
wake, akapigana na wezi wa marabarani (wanaowakatia watu njia), akaleta amani
nchini na kusimamisha mipaka ya dini kama walivyosimamisha maimamu walio kabla
yake, na akaishi hali ya kuwa marejeo kwa watu wa Oman. Ametoa mali yake yote
katika kuitia nguvu nchi na alikuwa tajiri kwa kuachiwa urithi na baba yake na
akafa hamiliki kitu. Amekufa usubuhi wa siku ya Ishirini na tisa Shaaban mwaka
1373H na Uimamu wake ulidumu miaka thelathini na nne, miezi tisa na siku kumi
na saba na alimchagua kuongoza umma Imamu (kabla ya kufa kwake) kwa sababu ya
fujo na mizozo ilioko wakti huo.
46)
Imam Ghalib bin Ali bin Hilal Al-Hinaaiy:
Ni pekee katika maimamu alichaguliwa na
Imam alie kabla yake (Imam Mohammed bin Abdallah bin Saeed Al-Khaliliy).
Akaingizwa katika uimamu kabla ya kuzikwa aliemtangulia. Alifanya wajibu wake
kwa umma isipokuwa kadari (hali ya mambo yaliotokea) haikumsaidia. Maafa
yaliyompata ni sawa sawa na yale yaliyompata Imam Assalt bin Malik. Naye
hakutawala isipokuwa miezi kumi na nane.
Maimamu hawa ndio
waliokubaliwa na wote (ijmaa). Amma wana
tarehe wa Kiomani wamehesabu maimamu sitini lakini hatukutaja hapa isipokuwa
wale mashuhuri.
Imeenea madhehebu ya Kiibadhi katika nchi
za magharibi za Kiarabu (Libya ,
Tunisia na Algeria ).
Tutataja hapa kwa kutoa mfano tu sio kwa
ajili ya kuzingatia majina ya wote hao waliochukua elimu kupeleka nchi za
magharibi:
Waliochukua elimu na dini kutokana na Imam
Abi Ubaidah Muslim bin Abi Kariimah ni:-
Abu Ubaidah Abd
Al-Hameed bin Mughteer Al-Janaawiniy, Imam Abu Al-Khattab Abd Al-Aaala bin
Assamh Al-Maafiriy naye ni Imam wa kwanza wa nchi hizi za magharibi.
Amechaguliwa kuwa Imam mwaka 140H na Imam Abd Arrahman bin Rustum Al-Faarsiy
(Tai wa Uajemu) amechaguliwa imamu mwaka 160H katika Taihert Algeria ambayo yalikuwa
ndio makao makuu ya Uimamu huu wa Kirustum katika kaskazini ya Afrika kisha
wakachaguliwa watoto na wajukuu zake kuwa maimamu kwa ajili ya elimu, fadhli na
uongofu wao. Kadhalika Abu Dawood Al-Qabaliy Annafzaawiy, Ismaaeel bin Draar
Al-Ghadaamsiy na Aasim Assaddraatiy na hao wote ni katika wale waliochukua
elimu kuipeleka nchi za Magharibi za kiarabu.
Kisha wakafuatia baada ya waliotajwa nyuma
wanavyuoni wakubwa tokea wakati huo mpake leo hii. Anachukua elimu ya dini yule
aliechelewa kutoka kwa yule alietangulia. Katika hao ni:-
Imam Abdilwahab bin Abdirrahman bin Rustum,
Imam Aflah bin Abdilwahab, Imam Mohammed bin Aflah bin Abdilwahab, Abu Mirdas
Mahasir Assidratiy, Abu Dhar Abaan bin Wasiim, Amroos bin Fath Almasaakniy, Abu
Khalil Addarkaliy, Abu Al-Muniib Mohammed bin Yaanis, Abu Al-Qaasim
Albaghtooriy, Abu Khirz Yaghlaa bin Zaltaaf, Abu Nooh Saeed bin Zangheel, Abu
Abdallah Mohammed bin Abi Bakr, Tabghuooriin bin Eeisa Almalshootiy, Abu
Arrabii Suleiman bin Yakhlef, Abu Ammarr Abd Al-Kaafiy, Abu Yaaqoob Yousuf bin
Ebrahim Al-Waarijalaaniy, Abu Nasser Fath bin Nooh Al-Malooshaaiy, Abu
Al-Qassim Al-Barraadiy, Ahmed bin Saeed Asshammaakhiy, Ahmed bin Saeed
Addirjiiniy, Yahya bin Sufyaan Al-laaloootiy, Abu Haaroon Al-Jalaalimiy, Abu
Arrabii Suleiman bin Haaroon, Abu Yahya Zakaria bin Ibrahim Albarooniy, Eesa
Attarmiisiy, Abu Saakin Aamer bin Aliy Asshahammakhiy, Abu Taahir Ismaaeel bin
Musa Al-Jaytaaliy, Dawood bin Ibrahiim Attalaatiy, Yaaqoob bin Ahmed
Al-Yafraniy, Abu Yahya Al-Janaawiniy, Mahdiy bin Esmaeel, Abdullah bin Mohammed
Al-Majdaliy, Abdul Aziz Atthamiiniy, Ibrahiim bin Yusuf Atfeysh. Mohammed bin
Yusuf Atfeysh (Qutb Al-Aimmah), Abdullah bin Yahya Al-Baarooniy, Abu
Al-Yaqdhaan Ibrahiim bin Issa, Ibrahiim bin Omar Bayyoodh, Abdallah Bakliy, Aliy
Yahya Muammar na wengineo wengi.
Wamesimamisha Maibadhi katika nchi za
Magharibi ya Uarabu uongozi wa uadilifu na Imam wa kwanza alikuwa Abu
Al-Khattab Al-Maafiriy kisha Imam Abu Haatim Al-Malzooziy halafu ukaja Uimamu
wa Kirustum ulikuwa mashuhuri. Nchi zilizopata hadhi ya kuwa chini ya uongozi
huu wa uadilifu ni Waarjalaam katika Algeria ,
Jarba katika Tunnis na Jabal Nafuusa katika Libya . Wakaunda nidhaamu ya
kutawala (Nidham Al-Azzaba) na ni mpango mzuri sana ndio uliohifadhi fardhi ya kuamrishana
mema na kukatazana na mabaya katika nchi hizi. Na mpango huu ulikuwa na athari
kubwa sana
katika kuhifadhi Istiqama katika nchi hizi.
Madhehbu hii kadhalika imeenea huko Yemen
na ikapata watu wakubwa waliopigiwa mifano mizuri katika elimu na vitendo.
Amesema juu yao Imam Mwanachuoni Mkubwa Waail bin Ayoub Al-Hadhramiy:
“Nimewawahi watu katika Hadhramaut kama
ingekuwa mmoja katika wao angepewa uongozi wa Ulimwengu mzima basi angelihimili
kufanya hivyo (Augeliweza kutawala bila ya tabu yo yote) kwa ukubwa wa akili,
elimu, busara na ucha Mungu wake”.
Katika hao Imam Taalib Al-Haqq Abdallah bin
Yahya Al-Kindiy Imam wa kwanza katika Yemen . Amechaguliwa mwaka 129H,
Abraha bin Assabaah Al-Hameiriy, Abdallah bin Saeed, Waaeel bin Ayoub, Abu
Almuarij Amrou bin Mohammed Assodousiy, Qais bin Suleiman na Imam Ibrahiim bin
Qais Al-Hadhramiy. Amesema Imam Noor Ad-Diin Assalmiy katika shairi: “Wa Omani,
Wa Magharibi na Wa Hadhramaut wana wengi katika viongozi wao, wanaofanana na
Omar wawili katika Uadilifu, kumkhofu Allah Subhanahu Wataala, uaminifu na
tabia nzuri. Wamepita katika njia ilio sawa basi wakapata sifa nzuri (Kusifiwa
na raia zao) pamoja na kupata radhi za mola wao Subhanahu Wataala
Ilikuwa madhehebu ya Ibaadhi imeenea huko
Khurasaan wakawa wanao wanavyouni, kadhalika Ghana, Magharibi ya Afrika. Bali kwa hakika Uislamu umeingia Afrika ya Magharibi kwa
njia ya Maibadhi na katika Afrika ya Mashariki. Kama ilivyokuwa Maibadhi wa Oman wao ndio waliopeleka Uislamu Mashariki ya
Asia, ndipo ulipoingia Uislamu huko Arkhabiil Al-Malayo (Malasia) katika mikono
yao .
Tuliyoyataja ni mukhtasari ili apate
msomaji kujua kuwa madhehebu hii ndio asili. Sio madhehebu ilio chaguliwa na
binadamu kwa mapendekezo ya nafsi zao la bali imechaguliwa na Allah Subhanahu
Wataala ……na mafinikio yangu hayawi isipokuwa kwa kutaka Mola Subhanahu Wataala.
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.