JEZUU YA PILI
Kasema
Allah katika sura Al-Hashr aya ya 7
ﭽ ﮠ ﮡ
ﮢ ﮣ ﮤ
ﮥ ﮦ ﮧ ﭼ الحشر:
٧
“Na
anayokupeni Mtume basi pokeeni na anayokukatazeni jiepusheni nayo”
Kupunguza
Sala zenye rakaa 4 – Adhuhuri, Al-Asiri na AI-Isha.
Ni
wajibu kwa msafiri kupunguza Sala hizi wala si ruhusa (khiari) kama hali ilivyo katika funga ya Ramadhani kwani msafiri
amepewa ruhusa ya kufungua (ikiwa atapata mashaka katika safari) kwa mujibu wa
kauli ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na kitendo chake. Ama kauli yake
amesema:-
فرضت الصلاة ركعتين ركعتين فأقرت في السفر وزيد في الحضر
أربعاً ) (
"Imefaridhishwa
Sala rakaa mbili mbili, ikathibitishwa katika safari na ikaongezwa kuwa rakaa
nne katika watani. (Ni lazima Muislamu kuchukua watani – mahala anapotulia na
kuishi ndani yake yaani anakuwa sio katika hali ya safari.)"
Vile
vile amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:-
(
على المقيم سبع عشر ركعة وعلى المسافر إحدى عشرة ركعة )
"Mkaazi
(katika watani wake) ni wajibu asali rakaa kumi na saba na ni wajibu wa msafiri
kusali rakaa kumi na moja."
Amma
kwa mujibu wa kitendo chake katika kupunguza Sala, ametoa hadithi Ibn Abbas
kuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam alikaa Makka katika mwaka wa Al-Fat-h
(mwaka iliyofunguliwa Makka) siku kumi na tano anapunguza Sala naye hana niya
ya kukaa ndani yake. Ikaendelea hali hii ya kupunguza Sala katika wakati wa
Makhalifa waliokwenda mwendo mzuri (Arrashidiin).
Mtume
Salallahu Alayhi Wasalam alitoka siku moja baada ya kusali Adhuhuri huko Madina
rakaa nne, na akaelekea Dhul - Huleifa akasali huko Al-Asiri rakaa mbili
kisha akarejea. (Hii Dhul-Huleifa iko mwendo wa farsakhi mbili kutoka Madina
(kilo meter 12 ndio mwendo ambao baada yake inapunguzwa Sala) na akasema
Salallahu Alayhi Wasalam: Nimekuja ili niwafundishe Sala ya kupunguza
(Inayosaliwa safarini).
Kwa
hivyo ni wajibu kupunguza Sala baada ya kusafiri kwa masafa (mwendo) ya
farsakhi mbili (sawa na kilometer 12). Na waliotutangulia walikuwa wakichukua
hima kubwa kuyapima haya masafa, na walikuwa wakipanda punda au ngamia na huku
wakiburuza kamba yenye urefu ujulikanao na huku wakitia alama hivyo hivyo mpaka
utakapokamilika mwendo wa kupunguza Sala. Na anayesali katika safari zile Sala
za rakaa nne (Adhuhuri, Al-Asiri, Al-Ishaa) akazisali hivyo hivyo rakaa nne
(bila ya kuzipunguza) ni sawa na aliyesali rakaa mbili katika watani wake
(akiwa kwao) yaani Sala yake haitimii. Baadhi ya waliokuwa hawajui husema:-
Ziada ni bora kuliko kupunguza yaani kusali rakaa nne ni bora kuliko rakaa
mbili na huu ni ujinga mkubwa unaonesha kutofahamu sharia ya Dini. Wengine
wasema nchi za kiarabu zote ni watani, maneno haya si kweli wala hayana msingi
wowote katika Dini. Wengine wasema: Hawachoki katika safari na kupunguza Sala
imeletwa kwa ajili ya taabu kama ilivyokuwa
safari juu ya punda na wanyama wengine, hii inaonesha upungufu wa maarifa. “Na
hakiwi kinachozidi kuliko Qur'ani isipokuwa upungufu.”
Na
Mtume Salallahu Alayhi Wasalam hakufa ila baada ya kuteremka kauli yake Allah Subhanahu
Wataala:
ﭽ ﭻ ﭼ
ﭽ ﭾ ﭼ المائدة:
٣
“Leo nimekukamilishieni Dini
yenu”
Na yeye
Mtume Salallahu Alayhi Wasalam ndiye aliyetuletea faridha ya Sala kutokana na
amri ya Allah Subhanahu Wataala kwa hivyo aliyotuamrisha ndiyo tunayoyafuata na
wala haitufalii kuongeza kitu chochote kwa uzushi wetu wenyewe kwani akili zetu
hazifikii kiwango hichi. Basi tusimame katika mpaka wetu tulioekewa na sharia
yetu ikiwa twataka mafanikio yetu.
Mkaazi
katika mji kwa ajili ya kazi na akawa hakutia nia ya kuishi katika mji huo bali
ikimalizika kazi yake arejea katika watani wake basi huyu asikamilishe Sala
zake (zile za rakaa nne asali rakaa mbili) isipokuwa ni bora asali kila Sala
kwa wakati wake yaani asichanganye baina ya Sala mbili. Asali Adhuhuri katika
wakati wake rakaa mbili, Al-Asiri rakaa mbili na Al-Ishaa rakaa mbili,
isipokuwa akisali nyuma ya Imamu ambaye ni mkaaji wa mji huo basi asali kwa
mujibu wa Sala ya Imamu (yaani akamilishe).
Kusali (kwa
msafiri) kila Sala kwa wakati wake na kuchanganya (Sala mbili pamoja) yote mawili
ni sunna, lakini ni bora kwa anayeishi ugenini kusali kila Sala kwa wakati wake
na kwa aliye mbioni safarini kuchanganya. Hivi ndivyo alivyokuwa Mtume
Salallahu Alayhi Wasalam akifanya (Adhuhuri na Al-Asiri akizisali pamoja, na Al-Maghrib na Al-Ishaa akizisali
pamoja, na Al- Fajiri husaliwa peke yake). Asiyekuwa na kwao (watani) huwa hana
Sala kwa hiyo ni lazima kila mtu awe na watani wake. Na katika masharti ya
watani ni kuwa huondoki humo isipokuwa kwa dharura.
Ni wajibu
wa kila anaeingia msikitini akakuta Sala ya jamaa yasaliwa kujiunga nayo, siyo
kusubiri mpaka ikamalizika au kusali peke yake wakati bado Sala ya jamaa
imesimama; hivi haijuzu.
Akishaifikia
safu atasoma tawjihi (na huku ametia nia moyoni ya kusali Sala Fulani ile
anayotaka kuisali).
( سبحانك اللهم وبحمدك تبارك
اسمك وتعالى جدك ولا إله غيرك إني وجهت وجهي للذي فطر السموات والأرض حنيفا وما
أنا من المشركين )
Kisha
atapiga Takbira Al Ihram. Ikiwa Imamu asoma Al Hamdu naye vile vile asome Al
Hamdu. Na ikiwa Imamu asoma sura (baada ya Al-Hamdu) yeye asikilize asisome
kitu kisha ailipe Al Hamdu (kwa kuisoma baada ya Imamu kutoa Salamu yeye
anyanyuke na aisome). Akiwa Imamu yuko katika Rukuu naye arukuu na akimkuta
katika Sujuud naye asujudu, akimkuta katika Tahiyaatu ya mwanzo naye akae asome
Tahiyaatu, lakini akimkuta katika Tahiyaatu ya mwisho amngojee mpaka atoe
Salamu kisha asali peke yake.
Vile vile
afanye ikiwa kaingia msikitini akaikuta jamaa na Imamu yuko katika rakaa ya
pili kwa mfano, yaani asome Tawjih kisha apige Takbirat Al Ihram asome Audhu na
asome Al-fatiha kisha arukuu pamoja na Imamu na amfuate mpaka atakapotoa
Salamu. Akitoa Salamu Imamu asimame aliyeunga Sala bila ya kutoa Salamu kisha
asome Al-Hamdu ikiwa Sala ya mchana na Al Hamdu na sura ikiwa Sala ya usiku,
kisha arukuu halafu asujudu sijda mbili kisha asimame kwa takbira mpaka atulie
katika kisimamo chake bila kusoma kitu; hapa ndipo mahala alipojiunga na Imamu.
Basi hapo akae na atoe Salamu. Na hivyo hivyo afanye akiingia katika Sala ya
jamaa katika rakaa ya tatu au ya nne. Aijalie mwisho wa Sala yake mwisho wa
Sala ya Imamu kisha alipe kilichompita yaani tokea mwanzo wa Sala mpaka pale
alipojiunga na Imamu.
Vile vile
ikiwa amejiunga na Imamu katika rakaa ya kwanza kwa mfano katika rukuu ya
kwanza asome Tawajiih kisha apige Takbira ya Al-Ihram na arukuu pamoja na Imamu
na amfuate mpaka atoe Salamu lakini yeye asitoe Salamu bali asimame na asome
Audhubillahi mina shaitani arrajim kisha asome Al Fatiha katika Sala ya mchana
na Al Fatiha na sura katika Sala ya usiku kisha akae (kikao cha Attahiyatu)
halafu atoe Salamu. Na akimkuta (akajiunga na) Imam katika mwanzo wa rakaa ya
pili au ya tatu au ya nne basi baada ya kutoa Salamu Imamu lazima asimame (bila
ya kutoa Salamu) ainuke ule muinuko uliompita kisha akae kama
tulivyoeleza kwani kuulipa ule mwinuko ndio kukamilisha Sala, bila yake
haitimii, lazima azingatie kitu hichi.
Na akikuta
safu imejaa (mstari wa watu wanaosali nyuma ya Imamu) hapana wasaa wa yeye
kuingia ndani yake basi na asimame nyuma ya safu asome Tawjiih na kabla ya
kupiga Takbira ya Al-Ihram amvute mmoja katika wanaosali safu ya mbele na
akishakuwa amesimama kando yake basi apige Takbira ya Al-Ihram na asipige kabla
hajasimama kando yake kwa sababu baada ya Takbira haimjuzii kufanya kitendo
chochote na asicheleweshe kupiga Takbira baada ya kufika sahibu yake kando yake
kwani itamharibia Sala yake. Azingatie mambo haya.
Sala ya
Jamaa ni faradhi kwa kila Muislamu kutokana na Aya za Qurani na Hadithi za
Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na juu ya hayo ni nuru kwa Muislamu. Sala moja
ya jamaa ni sawa sawa na Sala ishirini na saba ya kusali mtu peke yake.
Walikuwa
baadhi ya watu wema wakilia zikiwapita Sala za jamaa, na baadhi yao wazigharimu
nafsi zao kwa kuisali Sala hiyo hiyo mara ishirini na saba wakipitwa na Sala ya
jamaa, yaani katika hizi Sala moja ni faridha na zilizobakia ishirini na sita
ni “naafila”, na juu ya hivyo kajiona katika ndoto yuko nyuma na wenzake
(waliosali jamaa) wamemtangulia. Vile vile mwenye kuacha Sala ya jamaa bila
udhuru hukataliwa na Waislamu wala haikubaliwi shahada yake wala hapewi “walaa”
(kupendwa na Waislamu, kuhurumiwa na kuombewa Dua ya maghufira na ya kuingizwa
Peponi, akiwa hayi na akifa)
Kwa hivyo
anaepoteza Sala ya Jamaa kwa kazi yake au mchezo wake kama kushughulishwa na
biashara yake, kuendesha gari yake, kutizama mpira (football), upuuzi wa T.V au
mengineyo kama kujiona nafsi yake bora hawezi
kuchanganyika na watu wengine, hao wako katika hasara kubwa na ya uwazi
watakuja Siku ya Kiyama wana majuto makubwa siku iliyokuwa hayafai majuto.
Na tunatoa
mfano wa hayo:-
Kikundi cha
watu kimesafiri na kila mmoja katika wao kachukua katika safari yake hiyo
chakula na anachokihitajia ndani yake isipokuwa mmoja wao hakuchukua kitu. Je
mtu huyu hataona haya wakati wakimsaidia kumpa chakula chao? Na ikiwa
hawakumsaidia atashikwa na njaa.
Sala za
sunna ambazo hazina budi kusaliwa kuna zilizotiliwa nguvu (سنن مؤكدة) na kuna zisizotiliwa
nguvu (سنن غير مؤكدة).
Zilizotiliwa
nguvu:
Zilizotiliwa
nguvu ni zile ambazo Mtume Salallahu Alayhi Wasalam alizisali bila ya kuziacha
popote alipokuwa - safarini au kwake. Hizi ni sunna ya Al-Fajiri rakaa mbili
kabla ya faradhi, Salaa ya witri ambayo husaliwa baina ya Sala ya Al-Ishaa na
ya Al-Fajiri, na sunna ya Magharibi kwa
aliyeko kwake ( siyo kwa aliyeko safarini ) rakaa mbili baada ya faridha .
Sala za Idd
husaliwa rakaa mbili; hupigwa takbira tano baada ya Takbira Al-Ihram kisha
husomwa Al Hamdu na sura, katika rakaa ya pili husomwa Al Hamdu na sura halafu
hupigwa Takbira tano kisha kurukuu na baada ya kuinuka kwenye rukuu kabla ya
kusujudu hupigwa takbira tatu na kwa hizo hutimia takbira kumi na tatu (za
ziada). Kisha Imamu atatoa hotuba ifaayo.
Husaliwa
maiti kwa Takbira nne bila kurukuu wala kusujudu. Kwanza hupigwa Takbira
Al-Ihram baada ya Tawjiih kisha inasomwa Al-Hamdu halafu Takbira ya pili kisha
yasomwa Al-Hamdu halafu hupigwa Takbira ya tatu na baada yake husomwa Dua ya
ujumla kwa huyo maiti kama kauli yake Mola Subhanahu
Wataala:
ﭽ
ﯞ ﯟ
ﯠ ﯡ ﯢ
ﯣ ﯤ ﯥ
ﯦ ﯧ ﯨ
ﯩ ﯪ ﯫ
ﯬ ﭑ
ﭒ ﭓ ﭔ
ﭕ ﭖ ﭗ
ﭘ ﭙ ﭚ
ﭛ ﭜﭝ ﭞ
ﭟ ﭠ ﭡ
ﭢ ﭣ ﭤﭥ
ﭦ ﭧ ﭨ
ﭩ ﭪ ﭫﭬ
ﭭ ﭮ ﭯ
ﭰ ﭱ ﭼ غافر: ٧ - ٩
Ataongeza
kwa muombea maiti aliekuwa katika “Walaa” (Anaependwa na kuridhiwa na Waislamu
kwa msimamo wake mzuri katika Dini mpaka kufa kwake) kwa kumuombea Pepo na
radhi ya Allah Subhanahu Wataala kisha ajiombee nafsi yake na Wazee wake wawili
kisha hupigwa Takbira ya nne halafu husaliwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam
kisha hutolewa Salamu hafifu (kwa sauti ndogo).
1- Sala ya
Tahiyatu Al Masjid rakaa mbili, nayo husaliwa akiingia mtu msikitini na asome
ndani yake (baada ya Takbira Al-Ihram) Al-Fatiha na sura katika rakaa zote
mbili. Akiingia msikitini na Sala ya Jamaa yasaliwa basi na ajiunge na hiyo
Sala ya faradhi na hiyo Tahiyatu Al Masjid haimpasi na vile vile haimpasi ikiwa
atasali faradhi peke yake.
2- Sala ya
sunna ya Adhuhuri rakaa 2 au 4 kabla ya Sala ya faradhi na rakaa 2 au 4 baada
ya faradhi.
3- Sunna ya
Al-Asiri rakaa 4 nne kabla ya faradhi.[1]
Haisihi
Sala (haifai) yoyote baada ya faradhi ya Al-Asiri mpaka ingie Sala ya Magharibi
isipokuwa ikiwa mtu amepitiwa na usingizi bila ya kusali faradhi au kaisahau
basi wakati akigutuka au akikumbuka wakati huo huo aisali kwa hivyo hali kama hii haikatazwi kusali baada Al-Asiri kwa hadithi:-
( من نام عن صلاة أو نسيها
فليصلها متى ذكرها فذلك وقتها )
“Aliyelala wakati wa Sala au aliyesahau basi naasali akumbukapo
tu, na huo utakuwa ndiyo wakati wake hiyo Sala.”
Vile vile
katika Sala ambazo zawezekana kusaliwa baada ya Al-Asiri (haziingii katika
katazo la kusali baada Al-Asiri) ni Sala ya maiti, Sala ya kupatwa kwa jua au
mwezi na Sala ya tawaaf; hizi haiwezekani kucheleweshwa.
4- Sunna ya
Ishaa nayo ni rakaa mbili baada faridha.
5- Sunna ya
Dhuha nayo ni rakaa mbili, nne au nane.
6- Sala ya
kupatwa kwa Jua au Mwezi. Husaliwa rakaa mbili na rakaa ya pili huwa fupi zaidi
kuliko ya mwanzo, sijda ya pili huwa fupi zaidi kuliko ya mwanzo, nayo
huingizwa rakaa nyengine katika kila rakaa na rakaa mbili zikawa nne. Wakati
anaposimama kutoka kurukuu katika rakaa ya mwanzo husoma tena kwa ufupi zaidi
kuliko mara ya mwanzo kisha arukuu mara ya pili halafu asujudu. Hufanya hivyo
hivyo katika rakaa ya pili.
Haya ndiyo
tuliyofundishwa na sunna kuyafanya wakati linapopatwa jua na unapopatwa mwezi,
sio kama wafanyavyo watu wengi kuadhini njiani, kuwapiga wanyama na watoto
mpaka walie, kupiga ngoma na kupiga makelele kwa sauti kubwa wanafikiria
wakifanya hivyo wanawapasha habari Malaika kuwa mji wao umejaa watu nao ni
Waislamu kwa hiyo wasizamishwe katika ardhi. Imani kama hii ni uzushi ulioletwa
na maadui wa Kiislamu. Twamuomba Allah Subhanahu Wataala salama!
7- Sala ya
haja nayo ni rakaa mbili.
8- Sala ya
Istikhara rakaa mbili.
9- Sala ya
Tarawehe katika mwezi wa Ramadhani.
10- Kusali
Qiyaam katika theluthi ya mwisho ya usiku ijapokuwa rakaa mbili na kusoma
Al-Fatiha na Aya ya Al-Kursiy katika rakaa ya kwanza na Al-Fatiha na
Qul-Huwa-Allah-Ahad mara tatu katika rakaa ya pili.
Hizi ndizo
Sala za muhimu ambazo zimetokana na Mtume Salallahu Alayhi Wasalam, na uongofu
wote wapatikana katika kufuata mwendo wake Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na
wala hapana kheri kwa asiyefuata mwendo huo na hali aweza.
Sijda ya
sahau ni katika mambo yaliyo wajibu kuyafanya ili kuziba makosa yaliyofanywa
katika Sala. Na jambo ambalo wajibu hautimii isipokuwa kwa kulifanya basi nalo
ni wajibu.
Mfano mtu
kasahau katika Sala yake akasimama badala ya kukaa au kinyume chake, au kitu
kinachofanana na hicho kisha akakumbuka na akarejea, au ametoa Salamu katika
rakaa ya pili badala ya tatu bila ya kuondoka katika mahala pake hapo, wala
hakuzungumza bali alipokumbuka akasimama na kukamilisha Sala yake, au vile vile
anaesali nyuma ya Imamu naye akasahau katika Sala yake yote (akili yake haikuwa hadhiri tokea
mwanzo wa Sala mpaka mwisho) na hakujua Imamu kasali rakaa ngapi basi husujudu
kwa kusahau kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam.
Ama akiwa asali peke yake na akasahau asijue rakaa ngapi kasali mpaka kamaliza
Sala yake huyu lazima airudie. Na kama ametia shaka wakati yuko katika rakaa ya
tatu je yuko katika rakaa ya pili au ya tatu basi na aijalie rakaa ya pili na
akamilishe Sala yake, na kama hivyo akitia
shaka katika rakaa ya nne je yupo katika rakaa ya tatu au ya nne basi aijalie
ya tatu kisha aikamilishe Sala yake halafu asujudu sijda ya sahau.
Sijda ya
sahau humghadhibisha sheitani, asema “Ole wangu nimeamrishwa kusujudu na
nimeasi na binaadamu kaamrishwa kusujudu na akatii.”
Sijda baada
ya Sala inajuzu bila ya kusahau ikiwa haikufanywa kuwa ni katika Sala.
Alikuwa
Arrabii Allah Subhanahu Wataala amrehemu asujudu sijida mbili bila ya kusahau
lakini husujudu kwa ajili ya mghafala au upungufu ambao unamtokea katika Sala
akaupa hukumu ya kusahau.
Asema Ibn
Abbas: (Ikiwa aweza mmoja wenu asisali isipokuwa asujudu baada yake sijida
mbili basi na afanye hivyo). Lakini kwa sharti asichukulie kuwa ni wajibu. Ndio
maana wanavyuoni wetu wa mwisho wameziacha kwa kuogopea watu wasiojua
kuchukulia kuwa ni faradhi.
Kugeuka geuka katika Sala
Wengi
miongoni mwa wasiojua hugeuka geuka katika Sala na kitu hichi kinaharibu Sala
moja kwa moja, wala hakuna asemaye kuwa yajuzu kugeuka katika Sala, na
madhehebu ya Ibadhi haijuzishi kitendo chochote katika Sala hata kikiwa kidogo
vipi. Sala inabatilika kwa kucheza cheza walau kidogo ikiwa sio kwa ajili ya
kuitengeneza hiyo Sala.
Miongoni
mwa watu (wema) wako wanapoingia katika Sala wanakuwa hawasikii kitu hata
wakipitiwa na wapigaji ngoma, wachezaji
na waimbaji. Na wapo katika Maibadhi miongoni mwa hawa wengi wengi -
Allah Subhanahu Wataala awaridhie na awajaalie wawe radhi nae.
Na wala
hazingatiwi mtu mjinga na vitendo vyake, kwani Dini haichukuliwi kutokana na
wajinga, wala haiwezekani kuwahukumu watu wote kwa mambo yanayofanywa na watu
wachache, wala haifai kuwazulia watu wema kitu kisichokuwa cha kweli. (Wako
wanaosema kuwa Maibadhi wanachezacheza katika sala na hali imejengwa hukumu
hiyo kwa kuwaona badhi ya watu wajinga wanaposali wakahukumiwa Maibadhi wote
pamoja na Wanavyuoni wao kuwa ndivyo wanavyosali. Huu ni uzushi mkubwa). Kuna
msemo: "Mwenye matusi zaidi katika watu ni yule anayewatukana walio kama yeye". Na Allah Subhanahu Wataala ni Mjuzi wa
kila alisemalo mtu, basi na aseme atakalo.
Katika
mambo yanayoharibu Sala vile vile:-
Kunyanyua
kichwa juu (kutizama juu); wengi katika wasiojua wafanya harakati hii
wanaponyanyuka baada ya kurukuu. Vile vile kuteremsha kidevu na kukibanisha na
kifua mpaka akawa anaangalia tumbo.
Msimamo
sahihi katika Sala ni ifuatavyo:-
Aangalie
mtu pale anaposujudu wala asipakiuke kuangalia mbali au karibu zaidi.
Asifumbe
macho wala asiyafumbue sana
kiasi ya kuwa atashughulika na waliokuwa karibu yake, bali ayajalie baina ya
kufungua na kufunga. Na katika kukaa (kikao cha Tahiyatu) asikalie visigino
kwani mkao huu wakatazwa na sharia. Na wala asidonoe katika sijida (kusujudu
upesi upesi kama jogoo anapodonoa
chakula ardhini), na asiseme سبحان
ربي الأعلى chini
ya mara tatu katika sijida. Na baina ya sijida mbili akae kwa kituo mpaka kila
kiungo kitulie mahala pake na wala asiseme chochote baina ya sijida mbili kwani
kauli yoyote hapa huharibu Sala. Na Allah Subhanahu Wataala ndie mwenye kutoa
taufiki.
Kuosha Maiti
Katika
sunna zilizotiliwa nguvu ni kuosha maiti.
Kumuweka
maiti kwenye ubao na astiriwe utupu wake na muoshaji avae kitambaa mkononi
mwake.
Ataanza
kumsafisha utupu wake kuanzia kitovu mpaka magotini na atie mkono wake chini ya
nguo iliyomstiri maiti na amuoshe utupu wake kisha amkalishe maiti na kukama
tumbo lake mara tatu na amuoshe ikiwa atatoka uchafu (najisi) wowote. Akisha
hakikisha kuwa hana tena najisi amuoshe kwa maji na majani ya mkunazi. Na
mwenye kuosha siku hizi kwa sabuni badala ya majani ya mkunazi hakosolewi kwani
sabuni yasafisha zaidi kuliko majani ya mkunazi, lakini kuosha kwa majani ya
mkunazi ni sunna.
Kisha amtie udhu wa Sala halafu amuogeshe kwa maji safi kama kuoga janaba, kisha amuogeshe kwa maji yenye
manukato kama kafuri au mfano huo. Kwa hiyo
itakuwa jumla amemuogesha mara tatu. Na hiyo ndiyo sunna. Kisha amfute maji na
amtie katika sanda.
Zichukuliwe
nguo tatu nyeupe zilizo tahiri kwa mwanamme: kikoi, kanzu na kilemba. Na kwa
mwanamke nguo tano: suruwali, kanzu, ushungi na shuka mbili. Kwanza
zitandikwe nguo chini kisha ndio maiti awekwa juu yake na kabla hajafungwa na
hizo nguo azibwe kwa pamba katika kila uwazi wa mwili. Inapendelewa kutia
manukato katika pamba kisha atiwe machoni, puani, masikioni, mdomoni, na
huzibwa uso wake wote kwa pande la pamba. Pia awekewe kwenye shingo, kwapa,
kifua, kitovu, kwenye utupu, chini ya magoti na baina ya vidole vya mikono na
baina ya vidole vya miguu. Kisha azingirishwe sanda na ifungwe bila ya kukazwa sana .
Inapendelewa
akitiwa kaburini alegezwe fundo kwenye macho yake ili awaone Malaika wawili. Na
ni katika sunna kulifukiza jeneza kwa udi kwa kulizungushia kietezo mara tatu kisha ndio achukuliwe na
kupelekwa kaburini na awekwe mahala penye tohara na asaliwe halafu azikwe na
aachwe baina yake na Mola wake Mkarimu Mrehemevu.
ﭽ ﮇ ﮈ ﮉ
ﮊ ﮋ ﮌ ﮍ ﮎ
ﮏ ﮐ ﮑ
ﮒ ﮓ ﮔ ﭼ
الزلزلة: ٧ - ٨
[Basi
anayefanya wema hata wa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jaza yake. Na
anayefanya uovu hata wa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jaza yake]
Sala ya Kuomba Mvua ( صلاة
الاستسقاء )
Ni sunna
kusali Sala ya kuomba mvua kutakapoingia ukame na kukatika mvua. Husaliwa rakaa
mbili na husomwa katika kila rakaa Al-Hamdu na sura nyingine. Kisha husimama
Imamu na hutoa hotuba na kumuomba Mola Subhanahu Wataala kwa unyenyekevu na
kuogopa ili awaondolee balaa na awaletee mvua ili kuwarehemu waja wake, wanyama
na watoto. Na aipindue shuka yake aliyojifunika kama
ilivyokuja katika sunna. Na kuipindua shuka ni kuashiria matumainio mema ya
kubadilika wakati (kuja wakati mzuri).
Kuondosha
vilivyozidi katika mwili kama kukata kucha,
kunyonyoa nywele za kwapa na kunyoa nywele za kinena na kupunguza masharubu kwa
chini na pembeni mwake. Hayo yote ni katika sunna alizoamrishwa Muislamu
kuzifanya, nayo katika usafi yana sehemu isiyofichikana. Kwani vitu hivyo
vikiachiwa vizidi vitasababisha uchafu kujikusanya ndani yake. Makucha hukaa
vibaya yakitokeza na kuwa marefu, na masharubu yakiwa marefu yanambadilisha mtu
sura yake na kuchusha kama anavyochusha mwenye
kunyoa ndevu zake au mwenye kuzipunguza au kuzichezea.
Tizama
sharia ya Allah Subhanahu Wataala nini manufaa yake na ubora wake.
Hakutuamrisha kitu isipokuwa chapendeza na hakutukataza kitu isipokuwa
chachusha na kumfanya yule anachokitenda atishe kwa watu na ajihisi mwenyewe
yuko chini ya watu wengine, akikaa mbele ya watu wa heshima ajiona dhalili.
Angalia kwa
mfano mtu aoaye mke kwa halali huitangazia harusi yake na huwalisha watu
chakula na kulala mahala pazuri na godoro zuri katika raha na starehe. Lakini
amchukuaye mwanamke kwa haramu amficha watu wasimuone na hajali mahala gani
atampatia faragha hata kama kwenye zizi la
wanyama katika udhalilifu mkubwa. Hii ndiyo tofauti baina ya halali na haramu,
na utiifu na uasi. Ukisema lakini watu wengi hawajali kuyafanya mambo hayo
wayafanya nao wacheka bali wajisifu basi nitakujibu kuwa watu hao ni kama
wanyama, Allah Subhanahu Wataala ametoa heshima na sharafu katika nyoyo zao kwa
hivyo hayachukuliwi mafunzo kutokana na watu kama
hawa kwani wao ijapokuwa wengi lakini ni duni.
Ni karama
(heshima) aliyowakirimu Allah Subhanahu Wataala Umma wa Mtume Muhammad
Salallahu Alayhi Wasalam kwa ulimi wa Mtume wao. Imekuja karama hii katika
sunna tatu:- Kauli, Vitendo na akiwaona watu wanaonyoa au kupunguza basi
huwakataza. Na ameishi Mtume Salallahu Alayhi Wasalam mpaka kufa kwake bila ya
kuzigusa (kukata au kunyoa) ndevu zake na Masahaba wakafanya hivyo hivyo
wakafatiwa na Matabiina na waliokuja baada yao katika watu wema bali hata waovu (zamani
ilikuwa aibu kubwa kwa mwanamme kunyoa bali hata kukata ndevu).
Kukata
ndevu, wacha mbali kuzinyowa, ni haramu kwa mtu mwema na aibu kwa mtu muovu
mpaka ukatuingilia na kutupiga vita ukoloni na ukapandikiza ndani yetu mbegu za
udhalilifu na kutokuwa na sharafu aina mbali mbali. Na wakati wanapoondoka hao
wakoloni waacha nyuma yao utekaji wa kifikira
yaani zinakuwa fikira za watu wa hiyo nchi zimeathirika na hao wakoloni na
hufata mambo yao
mabaya. Inakutosha udanganyifu mkubwa waliouleta wa kumpa mwanamke wa Kiislamu
uhuru wake akabakia huyu maskini (mwanamke) kapotea hajui nini chakufanya yuko
baina ya kutaka huo uhuru wanaojidai nao na uhuru wa kweli ulioletwa na sheria
ya Kiislamu akawa kama kondoo anapelekwa na mchinjaji wake kwenda kumchinja
naye akimbia nyuma yake amfuata au ayaona malisho ataka kuyaendea kwenda kula
lakini huko angojewa na mbwa mwitu apate kumla kabakia yuko katikati hajui nini
la kufanya.
ﭽ ﭳ ﭴ
ﭵ ﭶ ﭷ
ﭼ البقرة: ١٥٦
"Hakika
sisi ni wa Allah, na kwake Yeye tutarejea (atatupa jaza yake)."
Nimemgombeza
mtu mmoja (Mu-Omani) kwa kunyoa ndevu zake akanijibu nimewaona wanavyuoni na
wazee wanyoa ndevu zao. Nikamwambia: Kama
ingekuwa kila Mwanachuoni na kila mzee astahiki kuigwa basi wa kwanza mwenye
haki ya kuigwa angelikuwa Ibliis. Yeye ni mkubwa wa wanavyuoni na mkubwa wa
wazee.
Na Allah Subhanahu Wataala
ndie Anayeongoza kwenye njia iliyonyooka.
Yamesemwa
maneno haya na Samahat Sheikh Ahmed bin Hamad Al-Khaliliy – Mufti Mkuu wa Oman :
Suali : Baadhi ya Waislamu waasi husema kuwa hakuna
katika Uislamu maelezo ya uwazi (katika Qurani na Sunna) ya kuharimisha ulevi
na sigara. Nini jawabu la mtu kama huyu.
Tafadhali kwa kutufahamisha.
Jawabu: Ni
neno kubwa hilo alilolisema huyu mzushi muongo na umekuwa uzushi mkubwa juu ya
Allah Subhanahu Wataala na Mtume wake Salallahu Alayhi Wasalam na Dini yake kwa
kuwa kuharimishwa kwa ulevi ni wazi na thabiti kwa Aya za Qurani ambazo hazina
shaka ambazo hazitilii shaka isipokuwa wale waliokuwa wameachwa hawapewi msaada
wala ushindi (na Allah Subhanahu Wataala na Mtume wake Salallahu Alayhi Wasalam
na Waumini) ambao wametiwa upofu na mapendekezo ya nafsi zao, zikiwapeleka
kwenye hilaki. Vipi mtu aweza akadai kitu hicho na Allah Subhanahu Wataala
amesema katika sura ya Al-Maida:
ﭽ
ﭑ ﭒ
ﭓ ﭔ ﭕ
ﭖ ﭗ ﭘ
ﭙ ﭚ ﭛ
ﭜ ﭝ ﭞ
ﭟ ﭠ ﭡ
ﭢ ﭣ ﭤ
ﭥ ﭦ ﭧ
ﭨ ﭩ ﭪ
ﭫ ﭬ ﭭ
ﭮ ﭯ ﭰ
ﭱﭲ ﭳ ﭴ
ﭵ ﭶ ﭼ المائدة: ٩٠ - ٩١
"Enyi
Mlioamini! Bila shaka ulevi na kamari na kuabudiwa (kuombwa) asiyekuwa Allah na
kutazamia kwa mishare ya kupiga ramli (na vinginevyo); (yote haya) ni uchafu
(ni) katika kazi za shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu
(kutengenekewa). Hakika shetani anataka kukutilieni uadui na bughudha baina
yenu kwa ajili ya ulevi na kamari; na anataka kukuzuieni kumkumbuka Allah na
(kukuzuieni) kusali. Basi je! Mtaacha mambo hayo?."
Basi
kuharimishwa kwa ulevi katika Aya mbili hizi (zilizotajwa juu) kuko wazi kabisa
katika pande kumi:-
Wa
kwanza: Umewekwa ulevi pamoja na kamari,
nayo ni kula mali
ya mwingine bila ya haki.
Wa
Pili: Umewekwa ulevi pamoja na kuabudiwa
asiyekuwa Allah na kutazamia kwa mishare ya kupiga ramli, na yote hayo ni
katika njia za ushirikina na amali za washirikina.
Wa
tatu: Kuhukumu kuwa huo (ulevi) ni
uchafu na uchafu hauwi halali.
Wa
nne: Kubainisha kuwa huo (ulevi) ni
katika vitendo vya shetani, na vitendo vyake si miongoni ya vilivyokuwa halali
katu.
Wa tano:
Kuamrishwa kuacha kuunywa, na amri (ya Allah) ni wajibu kuitekeleza ikiwa
hakuna kilichokuja kuivunja hiyo amri.
Wa
sita: Uokovu umeambatanishwa na kuacha
ulevi.
Wa
saba: Hakika ni katika sababu za uadui
na uchukivu. Na kinachosababisha uadui na kuchukiana baina watu basi ni haramu.
Wa nane:
Imebainishwa kuwa (ulevi) unazuia kumtaja Allah na kinachozuia kumtaja Allah
basi ni haramu.
Wa
tisa: Imebainishwa kuwa (ulevi) unazuia
kusali ambayo ndiyo kichwa cha ibada zote na mkusanyiko wa kumkumbuka (Allah)
na ndio inayojenga uongofu katika kheri.
Wa
kumi: Kusisitiza wajibu wa kuuacha
(ulevi) na kukoma kuunywa kwa maneno makali sana nayo ni maneno yake Allah Subhanahu
Wataala:
ﭽ ﭳ ﭴ
ﭵ ﭼ
المائدة: ٩١
“Basi jee! Mtaacha mambo hayo.”
Basi
laiti nijue kitu gani kimebakia (baada ya dalili zote hizo juu) kwa huyu
anaedai kuwa hakuna dalili katika Uislamu ya kuharimishwa ulevi. Na katika hadithi
sahihi kuna dalili zinazoshikamana kuonesha uharimisho wa ulevi.
Katika
hizo kauli yake Salallahu Alayhi Wasalam:
كل
مسكر خمر وكل خمر حرام )
)
‘Kila kinacholewesha ni
ulevi, na kila ulevi ni haramu’
Na kauli
yake Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:
ما
أسكر كثيره فقليله حرام ))
‘Kinacholewesha wingi wake
basi uchache wake ni haramu’
Na kauli
yake Salallahu Alayhi Wasalam:
( حرام قليله ما أسكر كثيره )
'Ni haramu uchache wake
kinacholewesha wingi wake’
Na kauli
yake Salallahu Alayhi Wasalam:
ما
أسكر الفرق منه فملء الكف منه حرام ) )
‘Kinacholewesha wingi wa
“Al-Faraq” (uzito wa ratili kumi na sita)
basi gao lake (mjazo wa kiganja) ni haramu.'
Na kauli
yake Salallahu Alayhi Wasalam:
لعن
الله الخمر و شاربها...)
)
"Allah Ameilaani pombe
na mwenye kuinywa…"
Hadithi
hizi zimeenea na zimekubaliwa na Umma kwa hiyo hakuna nafasi ya shaka.
Ama sigara
watu hawakuwa wakiitumia wakati ulipoteremshwa Ujumbe wa Uislamu bali imekuja
baada yake kwa makarne mingi. Kwa hivyo kukatazwa kwake kunaingia katika
misingi ya ujumla iliyowekwa na Uislamu ya halali na haramu, kwani Uislamu
unaharamisha moja kwa moja kila kinachodhuru akili, mwili, mali au heshima. Na madhara ya
kuvuta sigara yapatikana katika mambo yote hayo yaliyotajwa juu bila ya
kuhitaji maelezo zaidi. Kuwa sigara inasababisha maradhi mabaya yanayoua ya
kansa (Cancer) peke yake inatosha kuiharamisha. Tunamuomba Allah Subhanahu
Wataala atukinge nayo. Amin. Kwani (hiyo sigara) ni mshare uuao na nani ambaye
anayeruhusu kuiua nafsi yake licha ya harufu yake kuwa mbaya na Allah Subhanahu
Wataala anasema:
ﭽ ﮅ ﮆ
ﮇ ﮈ ﮉ
ﮊ ﭼ
الأعراف: ١٥٧
“Na anawahalalishia vizuri
na kuwaharamishia vibaya”.
Kwa hivyo
sigara ni haramu iliyo wazi kwa dalili hizo, na anaebisha basi huyo anaipinga
akili yake mwenyewe na anakataa uhakika wa mambo. Tunamuomba Allah Subhanahu Wataala
atuepushe na hali hiyo na yeye Mola ndiye Mjuzi wa kila kitu.
Na kutimia
kwa fatwa hii ndio kumalizika kwa makala hii. Namshukuru Allah Subhanahu
Wataala kwa taufiki yake. Na Rehema na Amani ziwe juu ya Mbora wa Mitume -
Mohammad na Jamaa zake na Masahaba zake wote. Hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa
kwa Allah Mtukufu Mkubwa.
[1] Hii ni kwa rai ya baadhi ya maulama; wengine wanasema
sala ya sunna kabla ya fardhi ya alasiri haikuthibiti, na hii ndiyo
aliyoisahihisha Alimu wa Hadithi Sheikh Said bin Mabrouk Al-Qannubi katika
kipindi cha Sual Ahli-'Dhikri cha TV ya Oman, kisha akasema lakini hakuna
dalili kuwa inakatazwa kusali nafla kabla ya fardhi ya alasiri kwa anayetaka,
kutokana na kauli ya Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- "Baina kila
adhana mbili (yaani adhana na iqama) kuna salaa".
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.