Tuesday, 19 January 2016

Juzuu 3 Haki---Kujenga Uongofu katika nyoyo za Vijana-




{ بسم الله الرحمن الرحيم }

            ﮜﮝ                                         ﮯﮰ                   النساء: ٣٦

"Muabuduni Allah wala msimshirikishe na chochote, na wafanyieni wema (Ihsani) wazazi wawili (Baba na Mama), na jamaa na mayatima na masikini majirani walio karibu na majirani walio mbali, na marafiki walio ubavuni (mwenu) na msafiri aliyeharibikiwa na wale iliyowamiliki mikono yenu ya kulia (kuume). Bila shaka Allah hawapendi wenye kiburi wajivunao."



Haki ni aina mbili:

1- Haki baina ya mja na Mola wake.

2- Haki baina ya Mtu na Wenzake (Jamii).


1- Haki iliyo baina ya mja na Mola wake ni kumuabudu Allah Subhanahu Wataala na kumpwekesha na kumtii na kutomshirikisha na cho chote.

2- Haki iliyo baina ya mja na wenzake ni haki zinazo wahusu viumbe baina yao wenyewe kwa wenyewe ili ihsani ienee baina ya binaadamu katika kila mambo ya maisha.


Na hizi haki ziko zilizo maalumu, za watu wote, za lazima (wajibu) na za kupendelewa.


Haki Maalumu


- Haki za jamaa waliohusu:

Yatuwajibikia kuwasiliana nao kwa kuwazuru na kuwafanyia ihsani, na hii ndio daraja ya juu kabisa ya mawasiliano, au kuwafanyia ihsani kwa mali bila ya kuwazuru, au kuwatembelea bila ya kuwafanyia ihsani ya mali. Na ikiwa hawezi kwenda wala kumsaidia kwa pesa basi kwa kumtumia salamu, na hii ndio daraja ya chini kabisa ya kuwasiliana. Wala asitie niya ya kuwakata jamaa zake kwani anaewakata huyo amelaaniwa, kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam.

Allah Subhanahu Wataala Amemegua jina la “Rahim” (jamaa waliomhusu mtu) kutokana na jina lake “Arrahiim” basi mwenye kuwasiliana nao Allah Subhanahu Wataala Atawasiliana nae na mwenye kuwakata (kuwapiga pande) na Allah Subhanahu Wataala Atamkata.



Hizi vile vile ni katika haki maalumu. Ni wajibu wa mtoto kuwatii wazazi wake wawili na awafanyie wema kama iwezekanavyo hata wakiwa waovu. Mtoto awatii wazazi wake katika mambo yaliyokuwa si ya maasi kwasababu:

( لا طاعة لمخلوق في معصية الخالق )

“Haifai kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba.”


 Na anyenyekee kwao na awatekelezee haja zao kwa kupenda na kutarajia malipo kwa Allah Subhanahu Wataala na wala asiwatazame mtazamo wa kukereka au kuchoshwa nao au kuwadharau, na wakimwita asiwaitike na huku amekaa  bali awaitike na huku anawakimbilia.

Hadithi inasema: Mwenye kuamka asubuhi na hali wazazi wake wawili wako radhi na yeye basi huamka na hali amefunguliwa mlango wa Peponi, na anayeamka na hali amewakasirisha wazazi wake wawili basi huamka na hali amefunguliwa mlango wa Motoni.


Inamlazimikia baada ya kufa kwao arudie kutubu na awatembelee marafiki zao na awafanyie wema kwa heshima ya wazazi wake. Ami na kaka mkubwa ni kama baba, na mjomba na mama mdogo (ndugu ya mama) ni kama mama inapokuwa baba na mama wamekufa; ni juu yake kuwahishimu hao na vile vile wazee wa Waislamu.



Imepokewa kutoka kwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:-

 (رحم الله والدا لم يحمل ولده على شاق يعصى بتركه)

“Allah Amrehemu baba ambaye hakumlazimisha mwanawe jambo gumu ambalo huasi kwa kuliwacha”.


Vile vile mtoto awaombee wazazi wake wawili rehema baada ya kufariki kwao kama alivyoamuru Allah Subhanahu Wataala:


                     الإسراء: ٢٤

"Sema: Ee Mola! Warehemu (wazazi wangu) kama wao walivyonilea na mimi ni bado mdogo."


Imesemwa kuwa mtoto ni (kama) uwa lenye harufu nzuri (reyhana) katika miaka saba ya mwanzo ya umri wake, kisha katika miaka saba ifuatayo huwa mtumishi na halafu katika miaka saba mingine huwa mshirika kisha atakuwa adui au rafiki.


Katika haki za mtoto juu ya baba yake ni kumtafutia mama mwenye ukoo mzuri na Dini asije akadharauliwa kwa ajili ya hali ya mama yake.

Amesema Mshairi:-

Ihsani yangu ya mwanzo kwako (mwanangu) ni kukuchagulia mama mwenye nzuri asili na njema heshima


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 (  تخيروا لنطفكم فإن العرق دساس )

"Chagulieni vizazi vyenu (mama wazuri) kwani mzizi unaendelea chini kwa chini (asili ya mama na tabia zitadhihirika kwa mtoto)."


Na baada ya kuzaliwa ni juu ya wazazi wake kumchagulia jina lililo bora kama majina ya Mitume na watu wema na wamfanyie akika akitimia umri wa siku saba. Akika ni kumchinjia motto wa mbuzi au kondoo na kugaiwa nyama yake kwa jamaa na majirani. Vile vile wamhifadhi na vitendo vibaya, na wamfundishe kumjua Allah Subhanahu Wataala na Mtume wake na kuwajua watu wema. Na wapandikize katika moyo wake chuki ya maovu na wenye maovu, na wamfundishe Qur'ani na wamhifadhishe. Wamhifadhi asicheze mwahala mnamochukiza. Akifika miaka saba wamfundishe Sala na wamzoeshe kusali.


Katika wakati wetu huu wa sasa kuna mashule ya kinidhamu hapana ubaya akipelekwa mtoto kusoma humo lakini kwa sharti mzazi asiitegemee hiyo shule moja kwa moja bali amchunguze usiku na mchana. Amuulize nini amejifundisha, wapi amekwenda, vipi amekwenda hata ajue kuwa kuna masuala ya kuulizwa katika kila harakati yake na asizoee kutoeka nyumbani. Amfanye mwanawe tangu udogoni amuogope kwani kama hakumfanyia hivyo kwa kumuonea huruma basi atampoteza na itakuwa vigumu kwake kumgombeza akiwa mkubwa na atakulia kuwa  hana adabu. Katika maneno ya waliotangulia: Mwenye kumtia adabu mtoto wake yu ngali mdogo hufurahika naye akiwa mkubwa.


Nimemsikia mtu miongoni mwa wenye akili akisema:-

Ikiwa unampenda mtoto wako sehemu mia ya mapenzi, usimuonyeshe isipokuwa sehemu moja tu na umfichie sehemu tisini na tisa, utatengenekewa wewe na atatengenekewa yeye mwenyewe.


Na ampige kwa kuwacha Sala na kuipuuza baada ya kufika miaka kumi ili mwili wake uchanganyike na utiifu hata ikimfikia taklifu (ikamuwajibikia ibada) anakuwa tayari kishaijua  ladha ya kumtii Allah Subhanahu Wataala; kwani mtoto mdogo ni kama ardhi iliyo tupu (haijapandwa), cho chote utakachokipanda ndani yake kitaota, basi tazama kile cha kupanda (kiwe kizuri).

Na katika usia muhimu ninaokuusia ni kuwa yasikufanye mapenzi ya mwanao umwachie afanye atakalo kwani hayo si mapenzi ijapokuwa unayachukulia kuwa ni mapenzi. Na muombe Allah Subhanahu Wataala akuepushe nayo. Asema Mola Subhanahu Wataala:-


             التغابن: ١٤

"Kwa yakini baadhi ya wake zenu na watoto wenu ni maadui zenu; basi jihadharini nao"


Mohammed bin Jaafar alimwambia mwanawe:- Hakika Allah Subhanahu Wataala ameniridhia mimi kwa ajili yako ndiyo akanihadharisha na mtihani wako, na hajakuridhia wewe kwa ajili yangu ndiyo akakuusia kwangu (unitii na usiniasi). Ewe mwanangu mtoto bora ni yule ambaye hisani (ya wazazi wake kwake) haimpelekei kudharau haki yao wala upungufu wa hisani haumpelekei kuwaasi.


Vile vile wawatenge baina ya watoto wa kiume na wa kike katika malazi.

Azidishe baba mtu kumbusu mtoto wake wa kike mdogo kwa sababu ya ujira mzuri anaopata kwa kufanya hivyo na vile vile kumuepusha asimchukie kwa hivyo ailazimishe nafsi yake kumbusu binti yake kwani kuchukia watoto wa kike ni katika masaliyo ya ujinga wa “zama za kijahili”. Ni juu ya muumini kukubali kila kitokacho kwa Allah Subhanahu Wataala kwani ndicho chenye kheri na yeye. Mbedui mmoja alimkasirikia mke wake kwa kumzalia mtoto wa kike na akamhama. Akamtungia shairi kusema: “Ana nini baba yake Hamza haji kwetu abakia katika nyumba ya pili ameghadhibika kwa sababu hatuzai watoto wa kiume kwani jambo hilo haliko katika uwezo wetu, hakika sisi twachukuwa kile tunachopewa”.


Mimi nilikuwa nikiambiwa umepata mtoto wa kike huenda upesi kumbusu na kumuombea Allah Subhanahu Wataala amuongoze, nafanya hivyo kuupinga ujahili wa mwanzo (kabla ya Uislamu) na wala simfanyi bora kuliko mtoto wa kiume kama ilivyo katika ujahili wa sasa.




Haki za Mke na Mume

         ﮜﮝ       البقرة: ٢٢٨

“Nao (wanawake) wanayo haki kwa sharia (kufanyiwa na waume zao) kama ile haki iliyo juu yao kuwafanyia waume zao. Nao wanaume wana daraja zaidi kuliko wao”


                             ﭞﭟ               ﭦﭧ                    ﭯﭰ            ﭶﭷ                         النساء: ٣٤

 "Wanaume (wawe) ni walinzi wa wanawake kwa sababu Allah amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii, wanaojihifadhi (hata) wasipokuwapo (waume zao) kwa kuwa Allah amewaamrisha wajihifadhi. Na wanawake ambao mnaona uasi wao kwenu waonyeni na waacheni peke yao katika vitanda na wapigeni. Na kama wanakutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Allah ndie aliye juu na Mkuu".


Katika Aya hii tukufu wanawake wamegawiwa makundi mawili baada ya kupewa mwanamme umbele kwa ajili ya akili yake na uhodari wa kufanya mambo na uwezo wake wa kuchuma maisha na kutumia mali. Kikundi cha kwanza cha wanawake ni wale wanaokikubali hicho cheo alichopewa mwanamme na Allah Subhanahu Wataala wakawatii waume zao na kuwahifadhi wao na mali zao, na hao ndio wale wanawake wema wenye kutii, wanaojihifadhi hata wasipokuwepo waume zao. Kikundi cha pili ni wale wanawake wasiokikubali hicho cheo alichopewa mwanamme, waliotoka katika tabia zao, hao ndio waasi wanaotibiwa kwa kuonywa, kukimbiwa na kuachwa peke yao vitandani na kupigwa.

Kila awachaye tabia yake (katika wanawake) huwa ameasi hata akiridhiwa na mumewe, maana radhi ya mtu kama huyu haitiwi maanani kwani waume kama hawa ndio aliowataja Mtume Salallahu Alayhi  Wasalam katika kauli yake:

(كل ديوث في النار)

"Kila Dayyuuth (Asiyemuonea wivu mkewe) yuko Motoni (ataingia Motoni)."


Nimesema kuwa hawakuharibika wanawake ila baada ya kuharibika wanaume; waliposhuka wanaume chini ya daraja zao wakashuka wanawake vile vile chini ya daraja zao.


Vile vile katika haki za mume za kisheria zilizompasa mke ni kumhifadhi mumewe katika nafsi yake (asimfanyie khiyana) na mali yake na awe mpole kwake na amliwaze katika shida na amtumainishe na amfanye asihisi upweke. Ikiwa mke hana sifa hizi basi hautapatikana ule utulivu ambao yeye ameumbwa kwa ajili yake na ameolewa kwa ajili yake.

Amesema Allah Subhanahu Wataala:


                     الأعراف: ١٨٩

"Yeye ndie aliyekuumbeni katika nafsi moja na katika (nafsi) hiyo amewaumba wake wao, ili (kila mwanamme) apate utulivu kwake (mkewe)."


Na mume anahaki nyingi (kubwa) zinazompasa mke kuzitekeleza kwake. Sheria ya Kiislamu imezitanguliza kabla ya haki za wazazi wawili.

Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 (  لو أمرت أحدا بالسجود لأحد لأمرت المرأة أن تسجد لزوجها )

"Kama ningeliamrisha mtu kumsujudia mtu (mwingine) basi ningeliamrisha mke kumsujudia mumewe."


Na amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 ( لو لحسته من قرن لقدم قيحا، ما أدت حقه )

"Kama (mwanamke) angemramba (mumewe) usaha kutoka kichwani mpaka mguuni (angekuwa na majeraha yatoka usaha kutoka kichwani mpaka mguuni) bado angekuwa hakutekeleza haki yake."


Ikiwa mume atamkataza mke kufanya kitu lazima amtii hata kwa mfano akamkataza kufunga sunna au kusali sunna, je vipi akimkataza kufanya kitu kilichokuwa na maasi ya Allah Subhanahu Wataala, basi ikiwa atampinga, Malaika watamlaani mpaka atakaporejea na akifa katika hali hiyo ya kumuasi mumewe ataingizwa Motoni.


Na katika haki za mke zilizo juu ya mumewe awe mpole kwake na amuonee huruma.


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

( خيركم خيركم لأهله و أنا خيركم لأهلي)

“Mbora wenu ni yule aliye mbora wenu kwa ahli zake (mkewe, wanawe na watu wa nyumbani kwake) na mimi ni mbora wenu kwa ahli zangu”.


Ni wajibu wa mume kumstahmilia mkewe akikosea kwani hakuna binaadamu anaekosa upungufu isipokuwa mwenye kuletewa ujumbe Mtume muaminifu Salallahu Alayhi Wasalam. Mwanamme asimdhihirishie mkewe kuwa amchukia hata ikiwa amchukia.

Amesema Mola Subhanahu Wataala:


  ﯣﯤ                                  النساء: ١٩

“Na kaeni nao kwa wema; na kama mkiwachukia (basi msiwaache) kwani huenda mkakichukia kitu na Allah ametia kheri nyingi ndani yake”.


Na anasema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 ( لا يفرك مؤمن مؤمنة إن كره منها خلقا رضي منها آخر )

"Muumin (mume) asimchukie Muumin (mke) kwani akichukia moja katika tabia zake (bila shaka) huridhika na nyingine (katika tabia zake)."


Na juu ya mume kutomdhiki mkewe katika matumizi na amtimizie kila lililo wajibu wake katika haki (za mke).

Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 ( استوصوا بالنساء خيراً فإنكم أخذ تموهن بأمانة الله واستحللتم فروجهن بكلمة الله )

"Usianeni kuwafanyia wake zenu wema kwani mumewachukua kwa amana ya Allah na mmejihalalishia tupu zao kwa neno la Allah."


Na cha mwisho alichousia juu yake Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kabla ya kufariki ni mke na mtumwa.

Vile vile ni juu ya mume amfundishe mkewe mambo ya Dini yake ikiwa yeye ni mjuzi zaidi katika Dini khasa kujiosha janaba, hedhi na ujusi na kujihifadhi na najisi na mengineyo yaliyo lazima kuyajua.



Amesema Allah Subhanahu Wataala:


                التحريم: ٦

“Enyi Mlioamini, jiokoeni nafsi zenu na watu wenu na Moto”.


Mola amemsifu Mtume wake Ismaeel (A.S) kwa kusema:


                       مريم: ٥٥

“Na alikuwa akiwaamrisha watu wake Sala na Zaka na alikuwa mridhiwa mbele ya Mola wake”.


Na juu ya mke na mume, wasitoleane siri zao, wala wasimwambie mtu mambo wayafanyayo wanapoingiliana, kwa sababu afanyaye hivyo huwa ni kama aliyemuingilia mkewe mbele ya watu.



Kupiga ponyeto ni zinaa. Nako ni kujichezea mtu utupu wake mpaka ukatoka manii, na hilo licha ya kuharimishwa kwake pia linaleta madhara kwa alifanyaye, huleta maradhi na kuleta machofu, na huenda ikawa hawezi kujimiliki nafsi yake kila inapotikisika dhakari yake humtoka manii sawa akiwa amejitayarisha kwa hayo au hakujitayarisha. Watu wengi wamepatwa na magonjwa kama haya. Basi udhia huu anaoupata mtu kwa kufanya kitendo hichi unamtosha kukiacha kama kingekuwa halali,  vipi nacho ni haramu?


Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amewausia vijana wafunge Saumu na amesema:- “Enyi vijana! Mwenye uwezo kati yenu wa kuoa basi na aoe, na asiyeweza basi na afunge kwa sababu Saumu itamzuilia matamanio”.

Wako katika vijana waliotumia Saumu na wakafanikiwa. Basi vijana watahadhari na wafanye subira juu ya awali ya ujana hasa katika wakati wetu huu ambao mahari yamekuwa makubwa na ufisadi umezidi. Na mambo yote ni ya Allah tokea mwanzo mpaka mwisho na hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa Kwake Mola Subhanahu Wataala.



Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam: Hakuacha ndugu yangu Jibril (A.S) anisisitiza kuniusia juu ya jirani hata nikadhania kuwa atamrithisha (jirani amrithi jirani yake).


Majirani ni wa namna tatu:-

Jirani mwenye haki moja – huyo ni jirani mushrik anayo haki ya ujirani.

Jirani mwenye haki mbili – huyo ni Muislamu anayo haki ya ujirani na haki ya Uislamu.

Jirani mwenye haki tatu – huyu ni Muslamu aliye na uhusiano wa damu – anayo haki ya ujirani, haki ya Uislamu na haki ya uhusiano wa damu.

Namna zote tatu za majirani wana haki zao, nazo kuwa wasiudhiwe na kuwastahimilia maudhi yao, wanasihiwe pindi wakenda mwendo mbaya, wapewe hongera kwa furaha zao (mkono wa furaha) wapewe rambirambi kwa misiba yao (waaziwe), wagawiwe sehemu ya vitu tunu waliokuwa hawanavyo pindi wakipata habari ya kuweko (vitu hivi kwa jirani yake), kutopeleleza aibu zao na kutotowa siri zao, kuwatekelezea haja zao na kumsaidia muhitaji wao.


Inasemekana kuwa jirani atamshika jirani yake kesho na kushitaki akisema: “Ameninyima hisani yake”.



Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amesema:

 ( من كان يؤمن بالله و اليوم الآخر فليكرم ضيفه )

"Anayemuamini Allah Subhanahu Wataala na Siku ya mwisho (Kiyama) basi naamkirimu mgeni wake."


Katika haki za mgeni ni kumshughulikia, kumtengenezea mambo yake, kuwa mpole nae kumkirimu kwa chakula na kinywaji na mahali pa zuri pa kulala. Asifanye jambo mbele yake ambalo litamfanya awe mnyonge kama kumpiga mtoto wake au mfanyakazi wake au hata kuwagombeza. Amsindikize mpaka mlangoni wakati anapotoka nyumbani na amkaribishe kwa furaha na bashasha aingiapo nyumbani


 Anasema Tegemeo la Maimamu (Mohammed bin Yusuf Attfeish) Allah Amrehemu: “Wala hana haki mgeni wa kishetani”. Huyo ni yule aliyetoka kwake ili kufanya maasi au kuwakatia watu njia (kuwaibia), anayeitukana Dini ya Kiislamu, aupigae vita Uislamu, mzinifu, na aliepigwa pande na Waislamu. Basi hao wote hawana haki yoyote katika haki za wageni. Amaeongezea Sheikh Abu Is-haaq Attfeish juu ya kauli yake (Sheikh Mohammed bin Yusuf Attfeish) anaeitukana Dini ya Waislamu kwa kauli yake: Na wale wanaoonyesha aibu za Waislamu (jasusi) kwani hao wawili katika mtazamo wa Sheria ni sawasawa, bali aliekuwa mbaya zaidi ni huyu wa mwisho na khabithi wao na ana madhara makubwa zaidi kwa Umma wa Kiislamu na Dini, kwasababu yeye ni jicho la adui kila akiona kuwa Umma unapata nguvu ya mali au hali huwapa habari madhalimu ili wapige vita kila nguvu au maendeleo katika taifa dhaifu, na humpa habari mtawala wa kimabavu anaefanya uwezo wa juhudi yake kuwapiga vita wananchi duni hali ya kuwa wako katika ghafla ili ateketeze kila walichokuwa nacho kwa ajili ya maslaha yake na matamanio yake.


Basi khaini au jasusi ajidhuru zaidi yeye mwenyewe kuliko kitu kingine kwa sababu anapiga vita kile kinacholeta manufaa na furaha kwa Umma wake ambao yeye hufurahika kwa furaha yake (huo Umma) na hupata tabu kwa tabu yake (Umma). Anabomoa kila heshima anayostahiki kuipata yeye, watoto wake na wajukuu zake, basi ni adui wa nafsi yake na adui wa watu wake kwa hiyo ni wajibu kumnyima kila haki inayompasa. Kwani huyo hana heshima yoyote na Muislamu humtilia shaka mtu kama huyo kama anayo Imani yoyote, vinginevyo vipi aliye na imani hata chembe atakuwa ndio chombo cha kubomoa Dini yake na kuharibu nchi yake (watani wake). Hakika ni katika kuikhini ile amana aliyoibeba mja kutoka kwa Allah Subhanahu Wataala na khiyana ya Umma na kuwadhuru Waislamu kuwa mtu huwa pamoja na watu (Waislamu) kisha akageuka jasusi juu yao na kuifanya hiyo ndio kazi yake. Hii ni sifa mbaya iliyoje kuwa nayo mtu mbele ya watu.


Imedhihiri shari hii mnamo wengi katika wana wa Kiislamu wanaifanya kwa ladha kubwa na wao wajidai kuwa ni Waislamu na kumbe Uislamu wajiepusha nao (watabarraa nao).

Inamtosha mtu hasara anayoipata hapa Duniani ya kukosa tawfiiq ya Allah Subhanahu Wataala (yaani hamnusuru wala hampi msaada) hata ametokana na Dini na Waislamu kwa ajili ya kuwahudumia wale wanaoifanyia vitimbi Dini na Waislamu, kisha Akhera anakuwa katika waliohasirika.


Hakuna jambo lenye sharafu kubwa kwa (Muislamu) kuwa kama ngome inayokinga Umma wake na vile vile kuwa na Ikhlasi na Dini yake na watani wake kwani ameumbiwa kwa ajili ya hivyo viwili. Hakuna Salama kwa jamii ila kwa ukweli wa watu wake na kufanya kila lenye maslaha kwake. Na ataulizwa kila mmoja wetu katika siku ambayo kila nafsi italipwa kwa ilichokitenda. Hapa yamekwisha maneno ya Abu Is-haaq Allah Amrehemu.



Mpita njia ni mtu aliyeachana na watani wake na mali yake. Huyu ashughulikiwe zaidi kuliko mgeni kwani yeye anahitajia zaidi. Inamlazimu anayempata huyu amkaribishe na kumkirimu vizuri na amsaidie anayoyahitaji katika safari yake na apewe kutokana na mali ya wakfu, mali ya msikiti au Zaka ijapokuwa yeye ni tajiri kwake.



Huyu mwenzio katika safari ana haki ya usuhuba na kumliwaza kwa kumpa chakula safarini na kumhudumu na kumpa anachokihitajia safarini na kumtanguliza kabla ya nafsi yako usimuudhi na umkinge na maudhia na wala usimtoe kwa anaetaka kumfanyia ubaya. Anaependwa zaidi katika wao na Allah Subhanahu Wataala aliye mpole zaidi kwa mwenziwe. Na wala mtu hana ubora zaidi kuliko mwenzake isipokuwa kwa kumcha Allah. Hakika mtu ni mkubwa kwa kushikana na mwenzake wala hana heri rafiki aliekuwa hakupendelei anacho kipendelea nafsi yake. Rafiki bora ni yule anayemsaidia mwenye kukumbuka na anamsaidia mwenye kusahau. Amesema haya Qutub Al-Aima.


Haki za Wote (Ujumla)

Kuwafanyia wema mayatima na masikini na wenye haja kama ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 ( المسلمون كالبنيان يشد بعضه بعض ، وكالجسد إذا اشتكى منه عضو تداعى له سائر الجسد بالسهر والحمى )

و (كاليدين تغسل إحداهما الأخرى )

و (لا تجسسوا ولا تحسسوا ولا تقاطعوا ولا تدابروا وكونوا عباد الله إخواناً )


“Waislamu ni kama jengo (moja), kila sehemu inatiliya nguvu sehemu nyingine na ni kama kiwili wili, kikishtaki kiungo kimoja basi mwili mzima hupata maumivu na homa na kukosa usingizi” na “Kama mikono miwili kila mmoja wao unauosha mwingine” na “Msichunguzane na msipelelezane na msipigane pande na msifanyiane vitimbi na kuweni waja wa Allah (mnapendana kama) ndugu.”


Kukidhi haja ya Muislamu na kwenda kwa ajili ya kuikidhi ni bora zaidi kuliko kufanya “Itikaaf” muda wa miezi miwili. Na inakupasa umpendelee ndugu yako (wa Kiislamu) kama unavyojipendelea nafsi yako. Na anaemuudhi Muislamu amelaaniwa. Na aliyesalimika ni yule aliyewasalimisha watu na ulimi wake na mkono wake.


Na katika haki za ujumla kumtolea Salamu umuonae. Amepokea Muslim hadithi ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 ( لا تدخلو الجنة حتى تؤمنوا ، ولا تؤمنوا حتى تحابوا ، أولا أدلكم على شيء إذا فعلتموه تحاببتم ....  أفشوا السلام بينكم )

“Hamuingii Peponi mpaka muamini, na hamuamini mpaka mpendane. Je! Nikujulisheni jambo ambalo mkilifanya mtapendana? Toleaneni Salamu”.


Na katika haki vile vile kutaka idhini kabla ya kuingia majumbani. Na msipopewa idhini basi msiingie. Asema Allah Subhanahu Wataala :


                          ﯻﯼ      ﯿ                             ﭚﭛ           ﭠﭡ       ﭤﭥ             النور: ٢٧ - ٢٨

“Enyi Mlioamini! Msiingie nyumba ambazo si zenu mpaka muombe ruhusa, (mpige hodi) na muwatolee Salamu waliomo humo. Hayo ni bora kwenu; huenda mtakumbuka (mkaona ni mazuri haya mnayoambiwa). Na kama hamtamkuta humo yeyote, basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa “Rudini”, basi rudini; hili ni takaso kwenu. Na Allah anajua mnayoyatenda”.


Vilevile kumpa mkono ndugu yako ukikutana nae na kuwakumbatia wazee wawili na kaka mkubwa na kuwabusu watoto.


Na katika kumtukuza Allah ni kumtukuza mzee na kumtukuza mwenye elimu, pia katika sunna kuwa na uso mkunjufu kwa watu, na kuwa na bashasha nao isipokuwa wale wazushi (wenye “bidaa”) hao haifai kuwakunjulia uso. Mfano wa hao kama mwenye kunyoa ndevu, au mwenye kuvaa dhahabu katika shingo yake au mkononi kwani kuwafanyia bashasha kama hao kuwasababisha watopee katika uzushi wao isipokuwa ukikusudia (kwa bashasha yako hiyo) kitu kingine (kama kumlainisha moyo wake aongoke kwenye njia ya kheri) basi hapo tena mezani ni nafsi yako na niya yako.

((Na mola anayajua yaliyo siri na yaliyofichika))


Na katika sunna ni kuitumia Dunia kwa kuitia nguvu Dini ya Allah Subhanahu Wataala (Al-Mudaaraah) na kuna tafauti baina yake na kuitumia Dini kwa ajili ya maslaha ya Dunia (hii sifa mbaya haitakiwi Muislamu awe nayo inaitwa Mudaahanah).


Vile vile katika haki za wote ni kupatanisha baina ya Waislamu na kufanya juhudi ili waliozozana wakubali mapatano. Pia miongoni mwa haki ni kumuombea Dua apigaye chafya, amwambie يرحمك الله       ikiwa baada ya kupiga chafya atasema  الحمد لله       na ikiwa hakusema hatapewa haki hiyo (ya kuombewa Dua), na mwenye mafua akenda chafya vile vile hana haki hiyo. Katika haki vile vile kumtembelea mgonjwa, na anaemtembelea mgonjwa huwa ameingia katika mabustani ya Peponi, na anaekaa nae ni kama aliekaa katika mabustani ya Pepo. Na inatakiwa afupishe kikao chake kwa mgonjwa. Vile vile afuate jeneza la Muislamu na anayefanya hivyo hupata malipo (makubwa) “Qiiraat” na ukubwa wake ni kama mlima wa “Uhud”.


Inasemekana kuwa kuna mambo kumi Allah humpa ampendaye.

1.   Kusema ukweli.

2.   Kumpa aombaye.

3.   Kumlipa mwenzako kwa kilicho bora zaidi.

4.   Kuwasiliana na jamaa waliokuhusu.

5.   Kuhifadhi amana.

6.   Kumkirimu mgeni.

7.   Kusamehe.

8.   Kumhishimu jirani.

9.   Kumhishimu mwenzako.

10. Kuwa na haya na ndio kubwa yao.


Kikao cha elimu ni bora kuliko kikao chochote kingine. Inasemwa kuwa kikao kimoja kizuri (cha elimu) kinafuta madhambi ya vikao elfu mbili elfu (milioni mbili) viovu. Na hawakai kwa kumkumbuka Mola wao isipokuwa wazungukwa na Malaika na wafunikwa na Rehema (za Allah) na Allah awataja kwa aliokuwa nao (Malaika), kikao cha elimu ni bora kuliko kusali rakaa elfu (sunna), kufunga siku elfu, kutoa sadaka dirhamu elfu, Hija elfu, kupigana Vita elfu isipokuwa yaliyo faridha. Kwa sababu Allah aabudiwa kwa elimu, atiiwa kwa elimu basi nyumba mbili (Dunia na Akhera) ubora wake huja kwa elimu na ushari wake ni kwa ujinga. Aseme mtu akihudhuria (majlis) kikao cha elimu:-

أشهد أن لا إله إلا الله وأن محمدا عبده ورسوله و أشهد أن الدين كما شرع وأن إلاسلام كما وصف، وأن الكتاب كما نزل  وأن القول كما حدث وأن الله هو الحق المبين ذكر الله محمدا بخير وصلى عليه وحياه بالسلام

Haya yote ameyaleta Qutub Al-Aimma.



Maneno haya yametokana na Sheikh Ahmed Al-Khaliliy Mufti Mkuu wa Sultanate ya Oman:

Suala – Je wenye madhambi makubwa watapata uombezi Akhera ikiwa wamekufa katika hali hiyo ya maasi?

Jawabu: Nataka kumjulisha huyo muulizaji na wengineo kuwa Qur’ani Tukufu imetuletea katika Aya nyingi kuwa kila afanyaye mema hulipwa kwa aliyoyafanya na aliyefanya maovu kadhalika hulipwa kwa aliyoyafanya. Na amehadharisha Allah Subhanahu Wataala Umma huu (wa Kiislamu) kwa  kudanganyika na matamanio. Amesema Mola Subhanahu Wataala:


               ﭮﭯ                                النساء: ١٢٣

  “(Kuingia Peponi) si kwa matamanio yenu, wala si kwa matamanio ya watu waliopewa kitabu (kabla yenu, lakini mambo ni haya): Atakayefanya ubaya atalipwa, wala hatapata mlinzi wala msaidizi kwa ajili yake mbele ya Allah.”


Na katika kutaja matamanio ya watu waliopewa kitabu pamoja na matamanio ya Umma huu kuna ishara kuwa baadhi ya watu wa Umma huu watadanganyika kama walivyodanganyika hao waliopewa kitabu na watayan`gan`gania hayo matamanio wakimtarajia Allah Subhanahu Wataala kuwa atawaghufiria madhambi yao kwa kuwemo kwao tu katika Dini hii na kumuamini Mtume Salallahu Alayhi Wasalam.

Pia katika kutaja matamanio ya watu waliopewa kitabu pamoja na matamanio ya Umma huu kuna mahadhirisho kwa Umma huu kufuata mwendo ule ule wa waliopewa kitabu ili kila mmoja (katika Umma huu) achukue hadhari na ajitahidi awezavyo kumtii Allah Subhanahu Wataala.  Na kuna Aya nyingi katika Qurani zinazotilia nguvu yaliyokuja katika Aya hii (iliyo hapo juu) ya kuwa kila mtu atalipwa kwa mujibu wa vitendo vyake. Katika hizo ni kauli yake Allah Subhanahu Wataala:

                                                                    النمل: ٨٩ - ٩٠

“Watakaoleta mema watapata mema kuliko hayo, nao katika mahangaiko ya siku hiyo watasalimika nayo. Na watakaoleta ubaya, basi zitasinukishwa nyuso zao Motoni: Waambiwe kwani mnalipwa kwa mengine isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda?”


Na kauli yake Allah Subhanahu Wataala:


             ﯼﯽ    ﯿ                               القصص: ٨٤

“Atakayefanya wema atapata jaza bora kuliko huo wema aliofanya, na atakaye fanya ubaya basi hawatalipwa wale wafanyao ubaya ila yale waliyokuwa wakiyafanya.”


Na hizi Aya ziko wazi kabisa hazikubali upinzani kuwa Allah Subhanahu Wataala amlipa kila mtu kwa vitendo vyake vikiwa vizuri au vibaya. Vile vile amebainisha Allah Subhanahu Wataala kuwa yeye husamehe madhambi ya waliotubu siyo madhambi ya wanaoshikilia kufanya maasi.

Amesema Mola Alietukuka:-


                    طه: ٨٢

“Na hakika mimi ni msamehevu sana kwa anayetubia na kuamini na kutenda mema, tena akashika uongofu(barabara).”


Amebainisha Subhanahu Wataalaa kuwa anasamehe mabaya ya wale wanaojiepusha na maasi makubwa yaani anasamehe madhambi madogo sio madhambi makubwa, na hasamehe dhambi ndogo isipokuwa kwa kujiepusha na madhambi makubwa, na sharti kutoendelea kuyafanya hayo madhambi madogo kwa kauli yake Subhanahu Wataala:


                                 النساء: ٣١

“Kama mkijiepusha na maovu makubwa mnayokatazwa, tutakufutieni makosa yenu madogo na tutakuingizeni mahala patukufu kabisa (Napo ni Peponi).”


Basi akielewa mtu hayo atakuwa amefahamu maana ya kauli yake Mola Subhanahu Wataala:


                            النساء: ٤٨

“Hakika Allah hasamehe kushirikishwa, na husamehe yasiyokuwa haya kwa amtakaye”.


Allah husamehe yasiyokuwa shirki kwa amtakaye ama kwa kutubia na kuacha kufanya madhambi makubwa na kurejea kwa Allah Subhanahu Wataala au kwa kujiepusha madhambi makubwa pamoja na kufanya madhambi madogo bila ya kukusudia kuendelea nayo na bila ya kuendelea kuyafanya.

Haya ndiyo yaliyokusudiwa kwa kauli yake Subhanahu Wataala:


               النساء: ٤٨

“Na husamehe yasiyokuwa haya kwa amtakaye”.


Kwani amebainisha Mola Subhanahu Wataala katika Aya nyinginezo wale anaotaka kuwasamehe, nao ni wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na wala hawaendelei na kufanya madhambi madogo madogo. Imekuja hadithi kutoka kwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam (kutilia nguvu haya):

 (لا صغيرة مع إصرار ولا كبيرة مع استغفار )

“Hakuna dhambi ndogo ikiwa itaendelea kufanywa (hugeuka kubwa) na hakuna dhambi kubwa pamoja na kutubia”


Vile vile Mola Subhanahu Wataala amehadharisha na mategemeo ya kughufiriwa madhambi na amebainisha kuwa kila mtu atalipwa kwa aliyoyafanya. Amehadhirisha vile vile na mategemeo ya kupata uombezi, na kuhadhirishwa huku kumeletwa kwa Umma huu. Amesema kuwaambia Waumini:


                                       ﮝﮞ        البقرة: ٢٥٤

“Enyi Mlioamini! Toeni katika vile tulivyokupeni kabla haijafika siku ambayo hapatakuwa kujikomboa wala urafiki (wa kusaidiana) wala uombezi. Na waliokufuru ndio waliojidhulumu kweli kweli”


Katika haya pia kuna mahadharisho kwa Umma huu na kwa wengine kuhusu kushikilia matarajio ya uombezi. Kuwa mtu watamuombea Manabii Siku ya Kiyama na kwa hivyo ataepuka na adhabu. Basi Allah Subhanahu Wataala amebainisha nani wanaostahiki uombezi wa Mitume na wengineo katika kauli yake:-

          الأنبياء: ٢٨

“Na hawamuombei (yoyote) ila yule anayemridhia (mwenyewe Mola).”

(Na ziko Aya nyingi zenye maana hiyo).


Basi Uombezi anaustahiki yule aliyeridhiwa (na Mola Subhanahu Wataala) pasipo mwingine, na ikiwa aliyeridhiwa ndio mwenye haki ya kuingia Peponi basi huenda akatubia mwenye kutubu kutokana na maasi yake akaujalia Allah (Subhanahu Wataala) huo Uombezi (atakaopewa) ukachangia katika kukubaliwa toba yake.

Ama wale wanaoendelea kufanya madhambi makubwa (bila ya kutubu na wakafa katika hali hiyo) basi hao hawapati Uombezi kutokana na Aya hizi zilizo wazi kabisa.

No comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.