Tuesday, 19 January 2016

Juzuu 14 Ikhlasi na Akhlakii njema ------Kujenga Uongofu katika nyoyo za Vijana





Ikhlasi katika kauli na vitendo ni wajibu na hamna budi nayo kwani Allah Subhanahu Wataala hapokei (haikubali) kauli wala kitendo bila ya ikhlasi ya kumkusudia Allah Subhanahu Wataala Aliyesema:-


       الزمر: ٣

“Wa kuitakidiwa Mola ni Allah tu”.


                 البينة: ٥

“Wala hawakuamrishwa ila kumuabudu Allah kwa kumtakasia Dini”.


                   النساء: ١٤٦

“Isipokuwa wale waliotubu (baada ya unafiki wao) na wakajitengeneza na wakamshika Allah na wakaukhalisisha utii wao kwa Allah.”


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam katika hadithi Al-Qudsiy:- “Ikhlasi ni siri katika siri yangu nimeihifadhi katika moyo wa niliompenda katika waja wangu”. Ameitoa Al-Hassan. Aliy bin Taalib  amesema: Msitie wasi wasi kwa upungufu wa amali (vitendo) walakini mtie wasiwasi kwa kukubaliwa kwake hivyo vitendo kwani Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amesema kumwambia Muadh bin Jabal:- “Ikhalisishe amali yako yakutosha kidogo katika hiyo”. Na amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :- Watu wa mwanzo wanaoulizwa Siku ya Kiyama watu watatu, mtu amepewa na Allah elimu basi ataulizwa na Allah Subhanahu Wataala : “Umeifanyia nini elimu uliyopewa? Atajibu Ewe Mola wangu nilikuwa nikiitumia (kwa kukuabudu) usiku na mchana” atamjibu Allah Subhanahu Wataala umesema uwongo na watasema Malaika umesema uwongo bali ulikuwa wataka uambiwe (na watu) kuwa fulani ni Mwanachuoni (mtaalamu) na umeambiwa hivyo. Na mtu Allah Subhanahu Wataala amempa mali akamwambia Allah umeifanyia nini akajibu nilikuwa naitolea sadaka usiku na mchana Akasema Allah Subhanahu Wataala umesema uwongo na wakasema Malaika umezua, bali ulikuwa wataka uambiwe kuwa fulani karimu na umeambiwa hivyo. Na mtu ameuliwa katika jihadi (katika njia ya Allah) na Amwambia Allah umefanya nini. Na hujibu ewe Mola wangu nimeamrishwa kupigana jihadi na nikapigana mpaka nikauliwa basi Allah Subhanahu Wataala humjibu umesema uwongo na wasema Malaika umesema uwongo bali ulikuwa wataka uambiwe fulani shujaa na umeambiwa hivyo, akasema Abu Huraira kisha akanipiga Mtume Salallahu Alayhi Wasalam pajani na akasema:-

 ( يا أبا هريرة أولئك أول خلق تسعر نار جهنم بهم يوم القيامة)

“Ewe Aba Huraira hao ni watu wa mwanzo Moto wa Jahannam utakokwa nao Siku ya Kiyama.”

           

Kifuatacho ni kisa cha mja na mti:-

Inasemekana kuwa kulikuwa na mja ambaye imemfikia habari kuwa kuna watu wanaabudu mti fulani. Akatoka kwa kila ikhlasi nae ameazimia kwenda kuukata akamjia Iblisi wakati yuko njiani enda huko (kuukata mti) akamuuliza Je waenda wapi? Akamjibu naenda kuukata ule mti (unaoabudiwa) pasi na Allah Subhanahu Wataala. Basi yule Iblisi akampa nasaha asifanye hivyo akamwambia sio wewe unaouabudu huo mti. Lakini hakuikubali nasaha yake na mwishowe ikafikia hiyo hali kuwa wapigane mieleka ikasalia yule mja kumshinda Iblisi. Akasema Iblisi Je nikuoneshe kitu kitakachokufaa zaidi kuliko kukata huo mti mimi nakupa ahadi kuwa kila siku utapata dinari mbili chini ya mto wako kila asubuhi, wewe masikini zitumie dirham mbili hizo kwa watoto wako, kuwapa sadaka ndugu zako (Waislamu wenzako) na kuwaliwaza mafakiri, nawe unajua fadhila gani iliyokuweko katika kutoa sadaka. Ama kuukata huo mti haitakupatia thawabu yoyote na pengine hao wanaouabudu wapande badala yake mti mwengine au pengine wakugomee (kuukata) na wakudhuru kwa hiyo utajitia kwa mkono wako katika hilaki. Yule mja yakamwingia na akayakubali yale maneno. Akarudi asubuhi akazikuta zile dirham mbili kama alivyomuahidi yule Iblisi, akaongeza matumizi yake na miongoni mwake akazitolea sadaka na siku ya pili ikiwa kama siku ya kwanza. Ama siku ya tatu hakukuta kitu basi akaghadhibika na akachukua shoka lake kwenda mtini akakutana na yule Iblisi kama mara ya kwanza na akataka kumzuia hakukubali na mwishowe wakapigana mieleka na Iblisi akamshinda yule mja na akampiga mhuri katika kifua chake na akasema (yule mja kumwambia Iblisi) vipi hivi  umenishinda mara hii? Iblisi akasema nimekushinda mara hii kwa sababu umekuja mara hii umeghadhibika kwa ajili ya zile dinari mbili na ama mara ya kwanza ilikuwa ghadhabu yako kwa ajili ya Allah, basi akawa pamoja na wewe kwani yule aliyekuwa Allah yu pamoja naye hashindwi na kitu. Na kisa hichi kinaayidiwa na kauli ya Allah Subhanahu Wataala :


          الحجر: ٤٠

“Isipokuwa wale waja wako katika wao waliosafika kweli kweli”


Kwani hawezi kushindwa yule aliyeisafisha amali (kitendo) yake kwa ajili ya Allah.


Baadhi yao wamesema kufanya ikhlasi muda wa saa moja tu ni kuokoka kwa milele. Na yasemekana elimu ni mbegu na vitendo ni vipando (vinavyopandwa) na maji yake ni ikhlasi. Na wamesema wataalamu kwa yule anaefanya amali ajikurubisha kwayo kwa Allah lakini ndani yake kuna uchafu (wa kutaka radhi ya mwingine pasi na Allah) kuwa kitendo hicho hakina ikhlasi kwa Allah na wamepigia mfano kitendo hicho kama mtu aliefunga kutaka kujikurubisha kwa Allah lakini pamoja na hivyo kataka kupunguza chakula kwa kupata siha nzuri (anafanya “diet”). Na vile vile mfano mwingine kama mtu asali kwa kujikurubisha kwa Allah Subhanahu Wataala (Sala ya usiku) kwa sababu amekosa usingizi au alinda bidhaa au alinda masahibu wake na haya ni mambo madogo kabisa ambayo huyafikirii kuwa yanaweza kuharibu ikhlasi je vipi yule anaetoa sadaka ili amridhishe yule anaempa hiyo sadaka na mengineyo kama hayo? Kwa hivyo kwa ujumla anaefanya kwa ajili ya Allah Subhanahu Wataala na kwa jili ya maslaha ya nafsi yake hapo inatoweka ikhlasi yake na kuchafuka usafi wa kitendo chake. Na bila ya shaka ametokana na ujumla huu yule aliyelala, kwa mfano, ili apate nguvu ya kusimama kusali Sala za usiku kwani huyu ijapokuwa yeye anapata katika huku kulala faida ya haraka (ihusikayo na Dunia) isipokuwa yeye makusudio yake ni kupata hadhi ya Akhera (faida ya Akhera yaani Al-Jannah na radhi ya Allah). Kwa hiyo imesemwa kuwa kulala kwa aliye funga ni ibada na vile vile kula kwa niya ya kupata nguvu ya kumuabudu Allah Subhanahu Wataala ni ibada na kama hivyo kwenda mtu na mkewe kwa niya ya kujizuiya kutazama (mume kutazama wanawake wa nje na mke kutazama wanaume wa nje) na kuvunja matamanio na kwa kutaka kupata mtoto kitendo hichi ndani yake kuna faida ya haraka ya Duniani lakini niya imekibadilisha kupata mafanikio ya Dunia na Akhera. Inawezekana mtu kufanya mambo akaamini kuwa amali hiyo ni safi kwa (ina ikhlasi) ajili ya kupata radhi ya Allah Subhanahu Wataala kumbe ndani yake yameingia mambo madogo (yanayo haribu hiyo ikhlasi) na hatanabahi nayo hayo na kujiepusha nayo isipokuwa aliepata tawfiiq katika Dini yake na mwenye kuifanyia hesabu nafsi yake na hakika tawfiiq iko katika mikono ya Allah Subhanahu Wataala:


         التغابن: ١٦

“Mcheni Allah muwezavyo (mwisho wa jitihada yenu).”


Na hii Aya iliyoko katika kitabu cha Allah inampa mtu moyo kuwa afanye kadiri ya uwezo wake (mwisho wajitihada yake) na baada ya hapo Allah hamkalifu kiumbe wake zaidi ya uwezo wake. Naye ni Mwingi wa Rehema na Maghufira.


Anasema Imam Al-Ghazaliy:- Viumbe waliokuwa na khatari kubwa zaidi kusibiwa na fitina hii (ya kuchafuka ikhlasi yao) ni wataalamu kwa sababu lengo la wengi wao la kueneza elimu ni kutaka aonekane hakuna kama yeye katika elimu na kufurahika kwa kufuatwa na watu (wafuasi) na kutaka ashukuriwe na asifiwe na Iblisi awapambia hayo na kuwaambia kuwa lengo lenu ni kutaka kueneza Dini ya Allah na kuitetea sharia ya Dini aliokuja nayo Mtume Salallahu Alayhi Wasalam.


Utamuona mtoaji mauidha (nasaha na kumbusho) anamsumbulia Allah Subhanahu Wataala kwa kukumbusha kwake watu na kunasihi kwake wafalme na afurahika kwa watu kukubali kauli yake na kumkusanyikia kwa wingi katika muhadhara wake lakini ajidai kuwa furaha yake hiyo ni kwa urahisisho alioupata wa kunusuru Dini ya Allah Subhanahu Wataala lakini husikitika na hapendezewi akimuona katika jamaa yake aliye hodari zaidi kuliko yeye kwa mauidha na kuwa watu waondoka kwake kumuendea yeye na lau kwamba nia yake ni nzuri ya kueneza Dini ya Allah angelishukuru kuwa Allah Subhanahu Wataala amempunguzia uzito huu kwa kumpa mwengine aufanye badala yake. Basi huyo shetani hamwachi na huzidi kumshawishi kuwa wewe kusikitika kwako ni kwa kukukatikia thawabu sio kwa kukuondokea watu kwani lau kwamba wangenufaika na ukumbusho wako ungepata wewe thawabu kwa hiyo kusikitika kwako huku kwa jili ya kukosa thawabu kuzuri basi sijui kama angesikitika Omar RA kwa kuwa Abu Bakkar RA amemtangulia kwa Uimamu na ukhalifa ingekuwa kusikitika kwake kuzuri au kubaya bila shaka mwenye Dini yake hawachi kun’gamua kuwa kusikitika kwake kungekuwa kubaya. Na huenda mtu akakhadaika na udanganyifu wa shaitani na kujisemesha nafsi yake kuwa angetokea alie bora kuliko yeye kwa jambo hili angelifurahi lakini akitokea mtu huyo hubadilika na kurejea kutokana na fikira yake hiyo. Hayatambui haya isipokuwa mjuzi wa vitimbi vya shetani na nafsi na amejishughulisha navyo muda mrefu.(Mwisho wa kunukuu)


Ukweli:

Ukweli ni wajibu nao ni kinyume ya uwongo. Uwongo mwenye kuwa nao achukiwa na alaaniwa. Basi ukiwa uwongo katika hali kama hiyo bila shaka ukweli (uliokuwa kinyume ya uwongo) ni tabia yenye kusifika na kupendwa. Na Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amewasifu sana wakweli (wanaume kwa wanawake) na anaejizowesha ukweli hubadilika akapata cheo cha Siddiq. Na Allah Subhanahu Wataala Amewachagulia cheo hichi wengi katika Mitume wake na Abu Bakkar Siddiq RA ameitwa Siddiq kwa sababu ya wingi wa ukweli wake na kumwaamini kwake Mtume Salallahu Alayhi Wasalam bila ya hata ya kumsikia mwenyewe Mtume Salallahu Alayhi Wasalam anazungumzia habari hiyo ya Israa na Miraji wakati aliporejea Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kutoka Beit Al-Maqdis na akawaambia Maqureish nao hawakumsadiki wakasema haiwezekani mtu kutoka Makka kwenda Shaam katika usiku mmoja na juu ya kuwa kawaletea dalili zinazothibitisha ukweli wake lakini bado hawakumsadiki. Hapo ndipo walipotoka baadhi yao kwenda kwa Abu Bakkar kama kumkebehi wakamwambia umesikia maneno anayoyasema sahibu yako, niya yao wampoteze, amesema hivi, hivi, akawajibu Abu Bakar إن كان قال فقد صدق  yaani “Ikiwa kasema maneno hayo basi amesema kweli” na hapo ndipo alipoitwa Siddiq na Allah Subhanahu Wataala kwa njia ya Jibriil AS, alipoulizwa vipi umemsadiki akajibu mimi namsadiki katika habari ya mbingu (inayotoka mbinguni) na mbingu iko wapi kutokana na sisi basi vipi nisimsadiki katika habari ya ardhi tuliyo sisi tumo ndani yake au maneno aliyoyasema (Siddiq RA) yako katika maana hii.

Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :- “Hakika ukweli unaongoza kwenye mambo mema (ya kumtii Allah Subhanahu Wataala) na mambo mema yanaongoza kwenye Al-Jannah. Na hakika mtu anasema ukweli mpaka anaandikwa kwa Allah Subhanahu Wataala “Siddiq” na hakika uwongo unapeleka kwenye mambo maovu (maasi) na mambo maovu yapeleka Motoni na hakika mtu anasema uwongo mpaka huandikwa kwa Allah kuwa muongo. Ameitoa hadithi hii Ibn Masoud. Inatosha kujua kuwa ukweli una fadhila kubwa kuwa neno la “Siddiq” limetolewa kutokana na “Sidq” ukweli. Amesema Ibn Abbas:- Mwenye kuwa na mambo manne amefaidika:- Ukweli, haya, tabia njema na shukrani na wamesema baadhi ya wanavyuoni:- Wamekubaliana wataalamu kuwa mambo matatu akiwa nayo mtu basi humuokoa sharti yote yajumuike: Uislamu safi usiokuwa na bidaa wala matamanio (ya nafsi) na ikhlasi katika vitendo kwa Allah Subhanahu Wataala na riziki halali kwa ajili ya Allah (chakula halali).


Haijuzu kudanganya kwa hali yoyote ile isipokuwa katika hali tatu ambazo wanavyuoni wameruhusu kudanganya ndani yake nazo:

Katika kupatanisha watu wawili unaweza ukasema kitu kisichokuwa kweli kwa ajili ya kulainisha nyoyo za hao unaowapatanisha.

Akiwa mtu ana wake wawili anaweza akamwambia mmoja wao maneno yasiyokuwa na asili ya ukweli ili kumridhisha sharti yasilete madhara katika mali au nafsi.

Kuwahadaa maadui wa Dini wakati wa vita na kuna kauli ambayo inatia nguvu maneno haya:

( إن في المعاريض لمندوحة عن الكذب )

“Katika kusema neno ambalo halifunui uwazi wa jambo kunatoa ukumbi wa kuepukana na uwongo”


Na hali kama hii inatokea mara nyingi na inamuepusha mtu kusema uwongo kama vile akilazimika kufanya “taqiya”  (kumwambia Mfalme dhalimu neno ambalo dhahiri yake litamsalimisha na ujabari wake lakini undani wake lina maana nyengine) au kukataa kufanya jambo jema ambalo hana uwezo wa kulifanya au mfano huo.


Inasemekana kuwa kuna mtu aliitwa na mfalme Jabbar wakati yuko nyumbani kwake (huyo mtu) akamwambia mkewe achore mstari katika ardhi kisha aweke vidole vyake juu yake halafu amwambie hayupo hapa yule Jabbari akafikiri kuwa hayuko nyumbani kumbe yeye kamaanisha kuwa hayupo katika ule msitari. Akasalimika nae.

Alikuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam akitaka kwenda vitani avistiri (hivo vita) kwa kusema neno lenye maana nyingine hata akisikia mtu hilo neno han’gamui kuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam anakwenda vitani. Imetolewa kutokana na Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kuwa wakati fulani bibi mmoja mzee alimtaka amuombee kwa Allah Subhanahu Wataala amtie Peponi akamjibu:

( العجائز لا يدخلن الجنة )

“Wanawake wazee hawaingii Peponi”


Basi hapo akalia (kumuona hivyo akamuonea huruma) na akamwambia kuwa maana yake mwanamke mzee atarudishwa kuwa kijana akiingia Peponi.


Qur’ani imewasifu wale watu wenye ukweli na Allah na wenye ukweli na watu:

              ﭘﭙ                ﭠﭡ        الأحزاب: ٢٣

“Wapo watu miongoni mwa walioamini waliotimiza waliyoahidiana na Allah. Baadhi yao wamekwisha maliza umri wao (wamekwisha kufa) na baadhi yao wanangoja (siku yao kufika), wala hawakubadilisha (ahadi yao) hata kidogo”.


Basi hii ndio shahada sahihi ambayo anatakiwa Muumini aitegemee, sio shahada za Kidunia ambazo wanazipata watu baada ya masomo (k.m. BA, PHD n.k). Basi anaeipata shahada hii na akairidhia huyo ndie aliyefuzu hakika. Na sio kuwa shahada hii ni hasa kwa wale masahaba ambao Aya hiyo hapo juu imeteremshwa kwa ajili yao bali imewakusanya wao na wengineo walio wakweli na Allah na wakapigana jihadi na adui yake na kumuabudu kwa ikhlasi na wako wapi mfano wa hawa leo wakati hima za watu zimekuwa dhaifu na nafsi zimetosheka na kuhadaika na raha ya Dunia na zimesahau raha ya milele (Peponi) walioekewa na Allah wale wanaopigana jihadi katika njia yake na wanaotoa nasiha kwa Dini yake na wakaipendelea Akhera zaidi ya Dunia na wakaogopa kikao cha Allah (siku wataokutana na Allah) katika siri yao na dhahiri na wakiwa peke yao au pamoja na watu. Ikiwa siri ya muumini na dhahiri yake imekuwa sawa sawa huwa na nguvu katika makao mawili ya Dunia na Akhera na awajibika kusifiwa, lakini uwazi wake ukienda kinyume na undani wake basi hapati malipo yoyote (mazuri) kwa anayoyatenda isipokuwa tabu. Amesema mtu katika watu wema:- Ikiwa undani wa muumini unawafikiana na uwazi wake Allah Subhanahu Wataala Amsifu kwa Malaika wake.



Kufanya kazi kwa ajili ya kupata maisha ni wajibu na haifai mtu kuwa mzigo kwa mwenzake yaani amtegemee mwenzake kwa maisha yake na Allah Subhanahu Wataala Muumbaji wa viumbe na Mgawaji wa riziki ameijaalia Dunia nyumba ya kufanya kazi na Akhera nyumba ya malipo mazuri na mabaya. Kwa hiyo kila anaetafuta maisha yake kwa njia ya halali anapewa mafanikio katika Dunia na apewa thawabu (pepo) Akhera na anaetafuta maisha yake kwa njia haramu apata hasara katika Dunia na Akhera. Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amesema :-

“Anaekusanya mali katika njia ya unyan’ganyi na kuiba, Allah Subhanahu Wataala, ampeleka kwenye hilaki na kuingia Jahannam”. Allah atuepushe nayo. Kutafuta maisha ni njia inayopeleka kwenye malipo mazuri na uvivu na kutegemea wengine sio katika sifa za Muumin.


Amesema Noor Ddiin Assalmy (rehema za Allah ziwe juu yake) Nampenda mtu mwenye azimio la nguvu (katika moyo wake na kutaka kufanya kazi) anaefanyia Dunia na Akhera kwa bidii kubwa, amma mwenye kupenda usingizi (kulala) huyo hakaribishwi.


Na uzuri ulioje wa mali halali unaompeleka sahibu yake Peponi. Na kitu gani kizuri zaidi kama Dini na Dunia vikikutana! na ubaya ulioje ukafiri na kufilisika ukikutana katika binaadamu!

Allah Subhanahu Wataala ameamrisha kutafuta kipato katika kitabu chake kitukufu:-

                  الجمعة: ١٠

“Tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Allah.”


Na amesema:-

          ﭿ    المزمل: ٢٠

“Na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila za Allah”.


               البقرة: ١٩٨

“Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila za Mola wenu (kwa kufanya biashara njiani mnapokwenda kuhiji).”


Na amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( من الذنوب ذنوب لا يكفرها إلا الهم في طلب المعيشة )

“Yako madhambi ambayo hakuna kinachoyafuta isipokuwa wasiwasi wa kutafuta maisha.”


Na amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( التاجر الصدوق يحشر يوم القيامة مع الصديقين والشهداء )

“Mfanya biashara mkweli atafufuliwa siku ya Kiyama pamoja na Masidiqiin na Mashahidi (waliokufa katika njia ya Allah).”


Na amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

( من طلب الدنيا حلالا وتعففاً عن المسألة وسعيا على عياله وتعطفاً على جاره لقي الله ووجهه كالقمر ليلة البدر )

 “Mwenye kutaka  Dunia kwa kutafuta riziki ya halali na kuepukana na kuomba (watu msaada wa maisha) na kuwatoshelezea mahitaji ya watoto wake na kumhurumia jirani yake akutana na Allah na uso wake kama mwezi usiku wa mbaa mwezi”.


Siku moja alikuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amekaa na masahaba zake wakamuona kijana anasulubu na nguvu na ametoka mapema atafuta riziki wakasema, ole wake huyu, kama ungekuwa ujana wake na usulubu wake katika njia ya Allah. Akasema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( لا تقولوا هذا فإنه إن كان يسعى على نفسه ليكفيها عن المسألة ويغنيها عن الناس فهو في سبيل الله وإن كان يسعى على أبوين ضعيفين أو ذرية ضعاف ليغنيهم ويكفيهم فهو في سبيل الله وإن كان يسعى تفاخراً متكاثراً فهو في سبيل الشيطان )

 “Msiseme hivyo kwani ikiwa katoka atafuta riziki ili aitosheleze (haja ya) nafsi yake kwa kujiepusha kuomba na kuwategemea watu basi ni katika njia ya Allah. Na ikiwa katoka kwa ajili ya wazee wake wawili dhaifu au watoto wake dhaifu ili awatosheleze haja zao ni katika njia ya Allah. Na ikiwa atafuta riziki ili ajifakharishe na azidishe mali yake basi ni katika njia ya shaitani”. Ameitoa hadithi hii Attabariy.


Kadhalika amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( عليكم بالتجارة فإن فيها تسعة أعشار الرزق )

“Ishikeni biashara kwani ndani yake kuna sehemu tisa katika sehemu kumi za riziki”.


Na akasema Salallahu Alayhi Wasalam:-

( لأن يأخذ أحدكم حبله فيحتطب على ظهره خير له من أن يأتي رجلا أعطاه الله من فضله فيسأله أعطاه أو منعه )

 “Kuchukuwa mmoja wenu kamba yake na kukusanya kuni na kujitwika juu ya mgongo wake ni bora kuliko kumuendea mtu ambaye Allah kampa katika fadhila zake, ili amuombe basi amkubalie kumpa au asimpe”.


Na akasema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( من فتح على نفسه باباً من السؤال فتح الله عليه سبعين باباً من الفقر )

“Aliejifungulia nafsi yake mlango mmoja wa kuomba Allah amfungulia milango sabini ya ufakiri”.


Na alisema Luqman mwenye hekima RA:-

 ( يا بني استعن بالكسب الحلال عن الفقر فإنه ما افتقر أحد قط إلا أصابه ثلاث خصال رقة في دينه وضعف في عقله وذهاب مروءته وأعظم من هذه الثلاث استخفاف الناس به )

 “Ewe mwanangu jisaidie kwa kipato cha halali uepukane na ufakiri kwani hafukariki mtu katu isipokuwa hupatwa na mambo matatu:- ulaini katika Dini yake, udhaifu katika akili yake na unaondoka utu wake (mambo yake mazuri ya kuonesha ubinaadamu wake) na juu ya yote haya matatu kudharauliwa na watu”

Alisema Omar RA: Asikae mmoja wenu akawa hatafuti  riziki akasema “Ewe Mungu wangu niruzuku, kwani mnajua kuwa mbingu hainyeshi dhahabu wala fedha”.


Wamesema baadhi ya wataalamu:-

“Kwa sisi  kufanya ibada sio kuinyoosha miguu yako (miwili katika Sala) na kumuachia mwenzako kazi ya kukutafutia chakula lakini uanze kuutafuta mkate wako ukishaupata fanya ibada”


Hadithi hizi zihishimikazo hazimaanishi kuwa ujizamishe katika (kutafuta maisha ya) Dunia na ujichokeshe kufanya hivyo. Sivyo hivyo lakini zamaanisha kuwa utafute maisha yako kiasi ya kujiepusha na kuomba watu na bila ya kusahau wajibu wako unaokulazimikia kwa Mola wako, lazima utanabahi sana na kitu hichi. Ama kuuza na kununua kuna masharti yake, anaetaka kufanya kazi hiyo juu yake arejee kwenye vitabu vya fiqhi kwani ndani yake atayapata yatakayo muongoza na kumfundisha na kumuokoa na biashara za haramu hasa katika wakati wetu huu wamejishughulisha watu kukusanya mali kwa wingi bila ya kujali nini chanzo cha mali hayo. Haya mabenki yaliyoondosha baraka na kuwaletea watu mambo mazito (adhabu) na yakawadanganya watu kwa madai yake yaliyopambwa na wakawa watu wanayadhania ni mepesi (na sivyo hivyo) na hayo mabenki yanyan’ganya zaidi kuliko yanavyotoa (hapa Duniani) na huko Akhera adhabu yake ni zaidi. Allah Subhanahu Wataala ni Mjuzi zaidi kitu gani yatakuletea mambo hayo, hesabu iliyo ndefu na adhabu iumizayo huko Akhera. Akifikiria huyu aliechukua huo mkopo wa riba (interest ya Benki) kuwa ataweza kulilipa hilo deni, vipi ataweza kufanya hivyo? Na nani atakaemlipa kwani hiyo mali imechanganyika yaani imewahusu watu chungumzima na inamsabibishia (huyo mtu aliechukua huo mkopo) moyo wake kuwa na “rain” yaani kufunikwa na maasi na mtu kama huyu hafaliwi tena mauidha Allah Subhanahu Wataala atuepushe na hali kama hiyo.


Enyi ndugu zangu biashara si kitu chepesi kama wanavyofikiria watu wengi. Hebu chukueni zingatio na mfano kutokana na kisa kilichotolewa juu ya Imam Abdul Wahab Arrustumiy na mtoto wake Aflah radhi za Allah ziwe juu yao. Inasemekana kuwa Aflah amemuomba baba yake ruhusa kwenda kufanya biashara akamwambia kwanza jifundishe fiqh ya biashara kisha niambie, basi alipoazimia safari yake akaleta vipando vyake na akamwambia baba yake. Hapo baba yake akamuuliza maswali mia tatu yanayohusu biashara na akamwambia ukinijibu nitakupa ruhusa. Yasemekana kuwa Aflah alijibu maswali 297 katika 300 na akasita katika maswali 3 kisha akayajibu. Hapo baba yake akamwambia bora uakhirishe kwenda mwanangu usije ukatulisha haramu basi hebu pima hali yao hao na wafanya biashara wa wakati wetu wa leo.



Tumekwisha taja katika jezuu ya tano ya kitabu hichi kitu kidogo kinachohusu tabia njema. Ama katika jezuu hii tatuzungumzia kwa mapana zaidi ili kuwahimiza vijana kukamata tabia njema na sira za watu wema zinazotakiwa kufatwa ili kupata ridhaa ya Allah Subhanahu Wataala na tawfiiqi inatoka kwake Mola Subhanahu Wataala. Amesema Mwenye zi Mungu Subhanahu Wataala kumwambia Mtume wake Salallahu Alayhi Wasalam:-

           القلم: ٤

“Na bila shaka una tabia njema kabisa”


Amesema Assidiiqa(msema kweli) Aisha bint Assidiiq (msema kweli) Allah Subhanahu Wataala awaridhie wakati alipoulizwa juu ya tabia ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam akasema “Tabia yake ni Qur’ani” na alimuuliza mtu Mtume Salallahu Alayhi Wasalam juu ya tabia njema akasema Salallahu Alayhi Wasalam kauli ya Mola Subhanahu Wataala:-


                 الأعراف: ١٩٩

“Shikamana na kusamehe na amrisha mema na wapuuze masafihi”.


Kisha akasema:-

( هو أن تصل من قطعك وتعطي من حرمك وتعفو عن من ظلمك )

 “Nayo (hiyo tabia njema) ni kumtembelea aliekukata(asiyekuzuru) na kumpa aliyekunyima na kumsamehe aliyekudhulumu”.


Akasema:-

( بعثت متمماً لمكارم الأخلاق )

“Nimetumwa ili kukamilisha tabia njema”.


Akasema Salallahu Alayhi Wasalam:

 ( أثقل ما يوضع في الميزان يوم القيامة تقوى الله وحسن الخلق )

 “Kilicho kizito zaidi kinachoekwa juu ya mizani Siku ya Kiyama ni kumcha Allah na tabia njema”.


Alikuja mtu kwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam mbele yake akamuuliza:- nini Dini? Akamjibu “tabia njema” akamjia kushotoni kwake akamuuliza nini Dini? Akamjibu “tabia njema” kisha akamjia nyuma yake akamuuliza: Ewe Mtume wa Mungu: nini Dini akamgeukia (na kumwambia) huelewi? Ni kuwa usighadhibike. Akaulizwa ewe Mtume wa Allah ni nini الشؤم   yaani “mkosi” (kinyume cha baraka) akajibu Salallahu Alayhi Wasalam الخلق سوء yaani “tabia mbaya”.  Mtu mmoja kamwambia Mtume Salallahu Alayhi Wasalam niusie akamjibu    اتق الله حيثما كنت“Mche Allah popote pale ulipo”. Akamwambia nizidishie akamwambia Salallahu Alayhi Wasalam  أتبع السيئة الحسنة تمحها   “Fatilia ubaya kwa uzuri utafuta (ubaya)”. Wasema wanavyuoni uzuri unaofuatia ubaya ni toba (utubie lile baya ulilolifanya). Akamwambia yule mtu Mtume Salallahu Alayhi Wasalam niongeze akamwambia:-  

 خالق الناس بخلق حسن  “Kuwa na watu mwenye tabia njema”.

Aliambiwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kuwa:- Fulani (mwanamke) afunga mchana na asimama usiku (kusali) isipokuwa tabia yake mbaya awaudhi majirani zake kwa ulimi wake akajibu لا خير فيها هي من أهل النار  “Hana kheri naye ni katika watu wa Motoni”.


Akasema Salallahu Alayhi Wasalam:- 

 ( سوء الخلق يفسد العمل كما يفسد الخل العسل )

 “Tabia mbaya yaharibu vitendo kama siki inavyoharibu asali”.


Kasema Wahab ibn Munabbih:- Mfano wa tabia mbaya ni kama chombo cha udongo kilichovunjika hakiwezi kuungika wala kukifinyanza tena mara nyingine. Amesema Ibn Abbaas RA:- “Kila jengo lina msingi na msingi wa Uislamu tabia njema”. Kauli za wanavyuoni katika tabia njema zimekithiri na mimi nasema kauli naomba iwe sawa:- “Tabia njema imeelezwa katika kauli ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:-

 (المسلم من سلم المسلمون من لسانه ويده)

“Muislamu ni yule aliewasalimisha Waislamu na ulimi wake na mkono wake”.


Huenda mtu akawa mwenye tabia nzuri lakini anaudhi kwa ulimi wake na huenda mtu mwenye tabia ya kutoa (kusaidia watu kwa njia tofauti) lakini awasengenya watu. Na ndivyo hivyo ukamilifu kwa binadamu tabu sana na ukamilifu ni wa Allah Subhanahu Wataala Peke yake. Na wanasema wanavyuoni kuwa msingi wa tabia njema ni mambo manne:-

Hekima

Ushujaa

Kujiepusha  na haramu

Uadilifu, na yaliyobakia ni matawi.

Na hakuna aliyekamilika katika mambo haya manne isipokuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na watu wengine baada yake Salallahu Alayhi Wasalam wametofautiana katika kukaribiana nae na kuwa mbali nae na hapana shaka kuwa anaekaribiana nae Mtume Salallahu Alayhi Wasalam basi yeye ni karibu na ridha ya Allah Subhanahu Wataala. Na Qur’ani tukufu imetoa ishara kuonesha tabia hizi wanazosifika waumini.


Amesema Subhanahu Wataala:-


                               ﯛﯜ         الحجرات: ١٥

“Wenye kuamini kweli kweli ni wale waliomuamini Allah na Mtume wake; kisha wakawa si wenye shaka, na wakapigania Dini ya Allah kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio wenye kuamini kweli kweli.”


Na hapana budi mtu kupigana jihadi na nafsi yake katika kujaribu kuitengeneza tabia yake kwani haipatikani (tabia njema) isipokuwa kwa kujizoeza. Ama walioumbwa nayo ni kidogo sana kama Manabii kwa mfano na wengineo kidogo ambao Allah Subhanahu Wataala amewajaalia na tabia njema katika maumbile yao. Na kila Muislamu akijitahidi kufanya mambo ya taa (utiifu) aongezewa thawabu na apewa na Allah tawfiiqi.


         ﮤﮥ          العنكبوت: ٦٩

“Na wale wanaojitahidi kwa ajili yetu, kwa yakini Tunawaongoza kwenye njia zetu. Na bila shaka Allah Yu pamoja na wafanyao mema”.


Tabia mbaya yasababishwa zaidi na ghadhabu na shahawa (matamanio ya jimaa na kula chakula). Kwa hiyo Muislamu atakiwa ajichunge na mambo haya mawili yasimtawale na ijapokuwa hayo ni katika maumbile ya mwanaadamu na hayawezi yakaondoka kabisa na yakiondoka basi kutakuwa na uharibifu mkubwa, kwa mfano ikiondoka shahawa ya chakula moja kwa moja itamsababisha mtu kuhilikika kwa njaa, na kadhalika ikiondoka shahawa ya jimaa (kuingiliana mke na mume) kitakatika kizazi, na ikitoweka ghadhabu hatoweza Muislamu kujitetea na yanayomhiliki, kwa hiyo ataingia katika haramu kwani kujitetea mtu nafsi yake na mali yake ni wajibu, lakini muradi unaotakiwa kuwa kila kitu kiwe cha kiasi na wastani kama ilivyowasifu Qur’ani Masahaba waliopata radhi ya Allah kwa kauli yake:-


             الفتح: ٢٩

“Ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao.”


Yaani wao wanaweka ukali katika mahala pake na wanaweka huruma katika mahala pake. Na kila jambo likiwa wastani ndilo lapendeza na kusifiwa. Kwa mfano ukarimu ni sifa iliyo katikati baina ya israfu na ubakhili, ushujaa ni sifa iliyo baina ya uoga na kujitia mtu katika hatari bila ya dharura na kujali. Na vile vile kujitenga na haramu ni sifa iliyo katikati baina ya kufanya kila kitu (halali na haramu) na kujizuia kufanya lolote. Kuchanganyika na watu kuna taathira kubwa kwa mtu kwani ikiwa kuchanganyika huko ni pamoja na watu wema basi atapata kutoka kwao tabia nzuri. Ama ikiwa kuchanganyika huko ni pamoja na watu waovu hapati kwao isipokuwa tabia mbaya. Wametoa mfano wa haya kama anaekaa na muuzaji mafuta mazuri na anaekaa na mfua vyuma, wa kwanza akutia harufu  nzuri na wa pili akusibu na macheche ya moto. Basi ajichagulie mwenye akili nani kati ya hawa ataka kukaa nae. Na kawaida ya mambo kuwa tabia inaiba tabia nyingine (yaani watu wakikaa pamoja tabia zao hulingana kwa njia ya mmoja kumwiga mwenzake) na kuna methali ya Ki-Omani inayosema:- “Mfunge farasi pamoja na punda atachukua mlio na mngurumo wake”.  Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amemsifu Muumini kwa sifa nyingi na zote zimeashiria kuwa ni tabia njema. Amesema:-

( المؤمن يحب لأخيه ما يحب لنفسه )

 “Muumini ampendelea ndugu yake kile anachojipendelea nafsi yake.”


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:

( من كان يؤمن بالله واليوم الآخر فليكرم ضيفه )                                                               

 “Anaeamini Allah na siku ya mwisho basi amkirimu mgeni wake”.


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

 ( من كان يؤمن بالله واليوم الآخر فليقل خيرا أو ليصمت )

 “Anaeamini Allah na siku ya mwisho basi aseme lililo na kheri au anyamaze”


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

( أكمل المؤمنين إيمانا أحسنهم أخلاقا )

 “Waumini waliokamilika mno Imani zao ni wale walio na tabia njema zaidi”.


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

 ( إذا رأيتم المؤمن صموتا وقورا فادنوا منه فإنه يلقن الحكمة )

 “Mkimuona muumini mkimya, mpole (upole wa kufikiri na kusubiri) muendeeni (ili mpate faida kwake) kwani huyo anafahamishwa hekima”.


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

( من سرته حسنته وساءته سيئته فهو مؤمن )

 “Mwenye kufurahishwa na vitendo vyake vizuri na kuhuzunishwa (kuona vibaya) na vitendo viovu basi huyo ni muumini.”


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

( لا يحل لمؤمن أن يشير إلى أخيه بنظرة تؤذيه )

 “Si halali kwa muumini kumuashiria ndugu yake (muumini) mtazamo utakaomuudhi (asimtazame kwa macho makali, kwa uadui)”.


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

(لا يحل لمسلم أن يروع مسلماً )  

 “Si halali kwa Muislamu amtishe Muislamu (mwenzake)”.


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

 ( إنما يتجالس المتجالسان بأمانة الله عز وجل فلا يحل لأحدهما أن يغشى على أخيه ما يكرهه )

 “Hakika wakaa (kuzungumza) wazungumzaji wawili kwa amana ya Allah Aliye na nguvu na kutukuka basi haimuhalalikii mmoja wao kumtolea kitu mwenzake anachokichukia kutolewa”.


Na hadithi ziko nyingi sana katika hayo tumezitaja hapa baadhi yake ili kuhimizana kusoma na kutafuta elimu zaidi. Ahnaf bin Qays aliambiwa umejifundisha subira kutoka kwa nani? (ikiwa mtu amemkosea humsamehe hata ikiwa ana uwezo wa kumlipiza).  Akajibu kutoka kwa Qays bin Aasim alikuwa siku moja azungumza na marafiki zake akaletewa mtoto wake ameuliwa na mtoto wa ndugu yake amefungwa, akaambiwa huyu mtoto wa ndugu yako kamuua mtoto wako, akasema: Wallahi hakuacha alichokuwa akikifanya wala hakukata maneno yake. Kisha akamgeukia mtoto wa ndugu yake akamwambia kitu gani kilichokufanya ewe mwanangu uukate mkono wako wa kulia kwa mkono wako wa kushoto. Halafu akawambia watoto wake mfungueni pingu mtoto wa ami yenu na mtayarisheni ndugu yenu (kwenda kumzika) na mpelekeeni mama yenu diya yake kwani yeye sio katika kabila yetu. Mara moja aliugua akaona vibaya kwa sababu watu hawakuja kumtembelea akauliza sababu yake akajibiwa kuwa watu wamuonea haya kwa sababu ya madeni anaowadai basi hapo akaamrisha mtu apige mbio sokoni kuwa yeyote anayedaiwa na Qays bin Aasim kasamehewa deni lake. Akasema alietowa hadithi hii kuwa siku ya pili ilivunjika ngazi ya nyumba yake kwa wingi wa watu waliokwenda kumtizama.




Malezi mema ya watoto yanawahusu zaidi wazee wawili kwani wao wana sehemu kubwa ya kufanya katika kuwalea watoto wao. Na nadra kuona mtoto amelelewa vizuri bila ya maangalizi ya wazee wake wawili na kumfuatilia katika harakati zake na tulitangulia kusema kuwa ni wajibu wa baba kuchagua mwanamke mwenye Dini na asili ili mtoto awe kama wazee wake wawili kama ilivyosema hadithi tukufu ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( اختاروا لنطفكم فان العرق دساس )

 “Chagueni kwa ajili ya vizazi vyenu kwani mzizi wafukika”(asili ya mama na tabia yake inaendelea na hujitokeza katika mtoto).


Moyo wa mtoto ni johari yenye thamani kubwa hautakiwi uachwe bila ya kutiwa nakshi nao unakubali kila kinachonakishiwa juu yake ukinakishiwa kitu kizuri juu yake nao unakuwa mzuri na ukinakishiwa kitu kibaya nao unakuwa mbaya. Na wazee wawili washiriki katika ubaya au uzuri wa mtoto na ni kitu cha ajabu sana kuwa wazee wawili wamkinga mtoto wao na kila kinachomdhuru kwanini basi hawamkingi na madhara makubwa kabisa nayo ni kuporomoka (kuhiliki) Duniani na adhabu kubwa huko Akhera, ghafla gani hii waliyokuwa nayo wazee na asema:

وليس يضر القوم موت خيارهم ولكن يضر القوم أن خدج النسل

Hawadhuriki watu kwa kufiwa na wabora wao lakini hudhurika na kizazi kikiwa kasoro.


Msiba gani kwa mtu kumlea mtoto wake na kumtaabikia akiwa mdogo na akiwa mkubwa ampoteza na kuwa pamoja na wapumbavu na wahuni ambao huchukiwa na watu na kutizamwa mtizamo mbaya. Hasara gani hii kwa wenye akili amma walio kuwa hawafikirii, nafsi zao zimekufa, hawajali usalama wa nafsi zao vipi watajali usalama wa watoto wao. Basi inataka kwa mababa wawashughulikie watoto wao kutoka wakati wa kunyonyeshwa mpaka wakati wa kubaleghe. Akibaleghe na hali amefaliwa na ulezi basi hiyo ni fadhila kubwa kutoka kwa Allah Subhanahu Wataala kwa wao wote. Na ikiwa haukumfaa ulezi na baada ya kubaleghe anahiliki mtoto na hali hii ni nadra kutokea kwani uasi (ubaya) huwa umemzidia huyo mtoto. Na hapa wazee wanakuwa hawana la kufanya wala hawalaumiwi wala wasijin’gate kiganja kwa majuto ya kuharibu malezi ya mtoto wao lakini hapana shaka anaewajibika kulaumiwa ni yule ambaye alipuuza kumlea mtoto wake akaja akagutuka (kutaka kumlea mtoto) umekwisha pita wakati wa kumlea na kumrudisha mtoto wake kutoka katika upotevu wake.


Wanawajibika wazee wawili kumtizama na kumpeleleza katika kulala, kula, kuvaa na kusoma kwake na akirudi kutoka shule wamuulize amesoma nini na wapi amekwenda, nani amesuhubiana nae njiani, amekula nini, na nani amempa na kwanini amempa hata ajue kuwa nyuma yake kuna maswali atakayoulizwa. Wasimwache ende kama mnyama azurure ovyo na wasiseme kuwa shule inatosha kumuilimisha na kumfundisha adabu na kumtengeneza awe mtu mwema sio hivyo bali shule sehemu yake ya kumlea mtoto ni ile wakati mtoto anapokuwa asoma ndani yake akimaliza ni kazi ya wazee wawili na mara nyingi mtoto anaharibika katika ule wakati anapokuwa baina shule na nyumbani ikiwa wazee hawampelelezi harakati zake.


Kitu cha kwanza kinachodhirika katika ulezi wa mtoto udogoni kwake ni haya, ukimuona mtoto aona haya wakati unapoonekana utupu wake au kikifanyika kitu kibaya basi hiyo ni dalili ya kupambazuka kwa nuru ya akili yake nayo ni bishara inayoonyesha kuwa mustakbali wake ni mzuri basi kama huyu haifai kupuuzwa bali furusa hii ya wingi wa akili yake itumiwe na afahamishwe vitendo vizuri avijue na vibaya kadhalika. Na aambiwe sira za watu wema ili achukue mfano wao na watu wabaya ili ajiepushe nao, na kama hivi isiachiwe fursa ipite bila ya kufaidika nayo, ahimizwe kuhifadhi Qur’ani na hadithi za Mtume Salallahu Alayhi Wasalam na aqiida iliyo sahihi na mambo waliyosema maimamu kuhusu hayo, hivyo wanakuwa wazee wake wawili ni washirika wa thawabu wa vitendo vizuri atakavyovifanya na hata baada ya kufa kwao zinaendelea thawabu hizo kuwafikilia kwa mujibu wa hadithi iliyosema:-

الدال على الخير كفاعله

“Anayeionyesha heri ni kama anayeifanya”


Na vile vile  hadithi:-

كل عمل ابن آدم ينقطع بعد موته إلا من ثلاث ولد يدعو له أو نهر أجراه أو مصحف وقفه

“Kila kitendo cha binadamu chakatika baada ya kufakwake isipokuwa mambo matatu mtoto anaemuombea Dua, au mfereji (wa maji) ameupitisha na msahafu ameuweka waqfu”.


Wasiwazoeshe watoto wao maisha ya raha na yanayosahaulisha Akhera kwani hayo si katika alama za watu wema. Na wamhifadhi asichanganyike na watu wa raha na michezo na vile vile ajitenge na mashairi yanayotajwa ndani yake mapenzi na mambo ya utupu (matusi) na wote wanayoshughulika na hayo kwa hoja kuwa huo ndio ujanja na tabia nzuri (kama kumsema mtu fulani hafifu) na ukweli wa mambo hayo yapanda katika nyoyo za watoto mbegu ya ufisadi. Basi ndio hivyo kila ikidhihirika kwa tabia njema inapasa asifiwe na kukirimiwa hata ajue kuwa amefanya kheri na aendelee nayo na upande mwingine asichukuliwe akifanya makosa na hasa kugombezwa mbele ya watu au hata akiwa peke yake, ikiwa akirudia basi hapo anapasa kupewa nasiha akiwa peke yake na ikiwa haikumfaa nasiha hapo atiwe adabu ili asijasiri kufanya maovu.


Baba yangu aliniona siku moja nimekojoa bila ya kujipangusa na jiwe “Istijmaar” (siku hizi makaratasi ya “tissues” yatumiwa badala ya mawe halafu ndio “Istinjaa” yaani kujiosha kwa maji) na mimi umri wangu miaka kumi akanipiga, vile vile kaniona siku nyingine nimepatwa na hamu ya kula chakula kigeni kimeletwa akanipiga na akaninyima hicho chakula kwa ajili ya hamu (uroho) iliyonishika kula hicho chakula na mimi umri wangu wakati huo sijapindukia miaka sita basi zikabakia kumbukumbu hizi katika moyo wangu kila kikija chakula au nikikidhi haja (kwenda chooni) yanijia hofu mpaka sasa nami mtu mzima umri wangu umepindukia miaka sitini. Alikuwa baba yangu Allah amjazi kheri hacheki na sisi wala hafanyi mzaha na sisi kwa kutahadhari tusije tukajasiri kufanya kitu kibaya akitukataza kukifanya kwani tutakuwa hatumuogopi tena kwa vile alivyokuwa katuzoesha kutufanyia mzaha. Mithali yasema:-

لا تري الصبي سنك فيريك إسته

“Usimuoneshe mtoto wako jino lako asije naye akakuonesha utupu wake (ukimchezesha na kumlegezea mtoto wako hatokuogopa, kila kitu kwa wastani).”



Maradhi manne yanayomuandama Muislamu ambayo habandukani nayo ila kwa jitihada kubwa. Maradhi hayo nayo ni tumbo, utupu, ulimi na jicho na kiongozi wa maradhi haya ni nafsi kwani yote hayo manne yamsibu mtu kwa kuamrishwa na nafsi. Na kila makosa yanayofanywa na Muislamu ukipeleleza utaona kuwa asli yake ni haya manne. Tumbo kwa mfano lamletea mtu matamanio na unajua hatari ambayo inaletwa na matamanio kama baba yetu Adam AS na mkewe Hawaa walivyokuwa katika Al-Janna Allah Subhanahu Wataala aliwaruhusu kula kila kilichokuwa humo katika vinavyoliwa isipokuwa mti mmoja kawakataza kula ndani yake. Yakawapelekea matamanio ya matumbo yao kutaka kula katika huo mti waliokatazwa kuula kisha zikiwadhihirikia aibu zao wakatolewa nje ya starehe za Pepo kwenda katika taabu ya Dunia. Ikiwa haya yamewatokea Adam AS na Hawaa na daraja yao waliokuwa nayo mbele ya Allah Subhanahu Wataala vipi basi wengineo. Tizameni hatari ya matamanio licha ya kuwa wameruhusiwa miti yote katika Pepo isipokuwa mti mmoja tu juu ya hivyo hawakuweza kujiepusha nao kwa matamanio mtu akiyaweka mbele.

Na akishashiba mtu mambo mengi yasababishwa na shibe kwani ni chanzo cha matamanio na mara nyingi amehimiza Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kupunguza kula kama katika kauli yake:-

 ( الفكر نصف العبادة وقلة الطعام هي العبادة )

“Fikra ni nusu ya Ibada na kula kidogo ndiyo Ibada”.


Imekuja habari kuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam alikuwa akaa na njaa kwa kutaka mwenyewe sio kwa kuwa hana chakula.


Amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

 ( لا تميتوا القلوب بكثرة الطعام والشراب فإن القلب كالزرع يموت إذا كثر عليه الماء )

 “Msiziuwe nyoyo zenu kwa kula na kunywa sana kwani moyo kama kipando kinakufa kikizidiwa na maji”.


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

( ما ملأ ابن ادم وعاء شرا من بطنه حسب ابن ادم لقيمات يقمن صلبه وإن كان لابد فاعلا  فثلث لطعامه وثلث لشرابه وثلث لنفسه)

 “Hakujaza binaadamu chombo cha shari zaidi kuliko tumbo lake, vyamtosha binaadamu vitonge (kiasi ya) kumsimamisha mgongo wake na ikiwa hana budi kufanya (kula chakula) basi theluthi iwe ya chakula chake na theluthi iwe ya kinywaji chake na theluthi iwe ya pumzi yake”.


Imetolewa hadithi kuwa Aba Hujeifah alipiga mbwewe katika majlisi ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam akamwambia punguza kupiga mbwewe kwako kwani watu watakao kuwa na njaa zaidi Siku ya Kiyama wale wanaoshiba zaidi Duniani. Isichukuliwe maana ya hadithi hizi moja kwa moja ambazo daima zinakataza shibe iliyopindukia kiasi inayomzuia mtu kufanya wajibu wake lakini pengine shari ya kukaa na njaa ikawa zaidi kuliko kuwa na shibe, na pengine njaa ikawa shari kuliko kuvimbiwa”. Inakuwa njaa iko karibu zaidi na ukafiri kuliko shibe lakini shari yake (shibe) ni kuwa inasababisha matamanio ambayo yamtoa Muislamu nje ya radhi ya Allah Subhanahu Wataala na kufanya yaliyokatazwa kama tulivyotangulia kusema juu ya kisa cha Nabii Adam AS. Inasemekana kuwa Nabii wa Allah Issa AS alikutana na Ibliis mara moja akamwambia Je uliwahi hata mara moja kunipoteza? Akamjibu: Ndio mara moja ulishiba na ikakusahaulisha shibe kumtaja (kumkumbuka) Allah Subhanahu Wataala akasema Issa AS basi tokea leo sitashiba tena na akasema Ibliis nami tokea leo simpi nasaha mtu yoyote.



Maradhi yanayohusika na utupu:

Nao ni mfalme mwenye nguvu isipokuwa kwa yule aliyewafikiwa akaimiliki nafsi yake. Na inasemekana kuwa ikisimama dhakari ya mwanamme basi theluthi mbili ya akili yake haifanyi kazi na imetolewa kutokana na Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kuwa amesema:-

( النساء حبائل الشيطان ولولا هذه الشهوة لما كان للنساء سلطة على الرجال )

 “Wanawake ni kamba za sheitani (zinazofungiwa watu kuwavuta kwa sheitani yaani kuwapoteza) na lau kama sio kwa haya matamanio basi mwanamke asingekuwa na uwezo juu ya mwanamme”.


Wamesema baadhi ya watu kuwa sheitani humwambia mwanamke wewe ni nusu wa askari wangu na wewe ndiwe mshare wangu ambao nikiurusha sikosei (kuwapata watu ili kuwapotosha) na wewe ndiwe mahala pa siri yangu na wewe ni mjumbe katika haja yangu kwani nusu ya askari wake ni matamanio na nusu ya pili ni ghadhabu.


Amesema Al-Ghazaliy: Na makubwa ya matamanio ni matamanio ya wanawake na matamanio haya yana kupindukia mpaka, yaliyopungua sana yakawa yametoweka na yaliyokuwa katikati yaani yako wastani. Yaliyopindukia mpaka hayo yatawala akili mpaka yakasababisha hima ya mwanamme iwe katika kustarehe na wanawake na huyu anakuwa mbali na njia ya Akhera au (hayo matamanio) yatawala Dini mpaka yakapelekea  kufanya madhambi makubwa na yaliyopunguwa humfanya mwanamme asitake wanawake au kuwa dhaifu katika kustarehe. Nao aina zote mbili hizi za matamanio zina makosa na hazitakiwi amma iliyokuwa yatakiwa ni kuwa matamanio yako wastani na kuwa yanafuata amri ya akili na sheria katika kuzuia kwake na kutoa kwake na yakizidi kutaka kupindukia mpaka basi huvunjwa kwa njaa na kwa kuoa.


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( معاشر الشباب عليكم بالباءة فمن لم يستطع فعليه بالصوم فالصوم له وجاء )

 “Enyi vijana jitahidini kuoa na aliyekuwa  hawezi basi afunge kwani funga ni kinga ya matamanio kwake.”


Amesema Saeed bin Al-Musayyab:

Hakuvunjika moyo Ibliis na mtu (kwa kushindwa kumpoteza) isipokuwa atamjia kwa upande wa wanawake na asema (haya) na yeye umri wake wakati huo miaka themanini na nne na jicho lake moja limepoteza nuru na la pili lakaribia kupoteza kuwa hakuna kitu kinachoniogopesha zaidi kuliko wanawake na anaeweza kujimiliki nafsi yake katika hali ambayo anaweza kutimiza matamanio yake basi huyo ni mtu kamili. Na mtu wa kwanza wa aina hii ni Yusuf Assadiiq AS na kisa chake kimo ndani ya Qur’ani tukufu basi na kila anaefanya kama yeye huyo amejifundisha kutoka kwake. Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( من عشق فعف فكتم فمات مات شهيدا )

 “Aliyependa kisha akajizuia (kuzini) halafu akaficha (asimwambie mtu siri hiyo) akafa basi amekufa shahidi”.


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

“Watu saba Allah Subhanahu Wataala Awafunika katika kivuli chake akawahisabu na miongoni mwao mtu ameitwa na mwanamke mwenye sura nzuri ili azini nae akasema mimi namuogopa Allah Subhanahu Wataala Mola wa walimwengu”. Na hii daraja kubwa haiwafikii isipokuwa wanaume waliokamilika inawezekana akatokea mwanamme kujizuia kuzini na mwanamke kwa sababu hana nguvu ya uume au kwa kumuonea haya mtu fulani au mengineo yanayomzuia sio mtu kama huyu aliokusudiwa na hadithi zilizotajwa hapo juu lakini aliekusudiwa ni yule mwanamme aliyesabiliwa kila uwezekano wa kuzini akajikataza nafsi yake kwa hofu ya Allah Subhanahu Wataala huyu ndiye mwanamme aliyekamili.


Kudhulumu ni katika mambo yanayopendwa na nafsi na ukimpata anaeweza kujizuia na zinaa basi huyo hadhulumu. Sababu ziko nyingi amma sababu ya kumcha Mungu ndio sababu inayoshukuriwa.


Matamanio ya Ulimi

Ulimi ni neema kubwa katika neema nyingi za Allah Subhanahu Wataala na licha ya udogo wake kimwili haubainiki ukafiri kutokana na Imani ila kwa ulimi na uongofu wa waja haupatikani na kulingania Dini ya Allah Subhanahu Wataala isipokuwa kwa ulimi na uwanja wake ni mkubwa sana hauna mipaka sio kama viungo vingine kwani manufaa yake yana mipaka.

Inataka kutumiwa neema hii ili kufikia radhi za Mola Subhanahu Wataala kwani kama Angelitaka angekujaalia bubu kama mnyama basi Je inapendeza kwa aliye huru kurudisha ubaya kwa uzuri (wema) kwa hiyo amche Allah Subhanahu Wataala juu ya kile alichomruzuku asikitumie katika kutekeleza matamanio yake. Ulimi una matamanio mengi yanayomtia sahibu wake Motoni kama alivyosema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

( و هل يكب الناس على وجوههم أو قال على خياشيمهم إلا حصائد ألسنتهم )

 “Je yawamwaga watu Motoni kuangukia nyuso zao au amesema kuangukia pua zao isipokuwa mavuno ya ndimi zao.”


Yafuatayo ni maradhi ya ulimi yanayosababishwa na matamanio yake:-

Kusema zaidi ya haja.

Kujifanya bingwa wa kuzungumza hasa wale watoaji hotuba na wale wenye fasaha na wepesi wa kutoa maneno.

Kuzungumzia yalio batili (kinyume ya haki).

Kujadiliana katika kununua.

Kufanyiana khusuma.

Kusema kwa kuyatolea maneno kooni.

Maneno machafu, matusi, ulimi mrefu (unaochukiza).

Kulani mnyama au kilichokuwa hakina roho au binadamu.

Kuimba na kutoa mashairi yaliyo haramu.

Mzaha.

Kejeli na stihizai.

Kutoa siri za watu.

Kuvunja ahadi.

Kusema uongo.

Kuapa kwa kitu batili.

Nyuso mbili – kuwa na huyu kwa uso na mwingine kwa uso tofauti.

Kusifiana.

Kuwauliza watu wa kawaida (wasiokuwa na elimu) juu ya sifa za Allah Subhanahu Wataala.

Kusengenya.

Kufitinisha.


Haya maradhi ishirini ni baadhi tu ya mengi yaliyokuwa hayakutajwa na yote katika madhambi makubwa na kusengenya na kufitinisha ni yaliyo mabaya zaidi katika hayo na wanavyuoni wamepima kwa haya madhambi mawili makubwa kuwa madhambi yote mengine yanayovunja udhu na Saumu vile vile katika makubwa kwa hadithi iliyokuja ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:-

 ( الغيبة والنميمة ينقضان الوضوء ويفطران الصائم )

 “Kusengenya na kuchonganisha (kufitinisha au usabasi) kwavunja udhu na kwamfungulisha aliefunga”.


Kwa hiyo baadhi ya wanavyuoni wamesema kuwa madhambi makubwa yote yatengua udhu na yafungulisha aliefunga kwa kuchukulia kipimo cha madhambi haya mawili na wengine wamesema kuwa yanayovunja Saumu na udhu ni haya haya mawili tu kama ilivyosema hadithi. Kwa hiyo sheria imehimiza na kutilia mkazo kunyamaza kwa kutahadhari na maafa yanayoletwa na ulimi. Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amesema:-  من صمت نجا   “Mwenye kunyamaza aokoka” na amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-  الصمت حكم وقليل فاعله   “Kunyamaza ni hekima na watu kidogo wafanyao hivyo” na mmoja katika masahaba alimwambia Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-  Nijulishe kitu katika Uislamu ambacho sitahitajia kumuuliza juu yake mtu yeyote mwingine baada yako akamwambia Salallahu Alayhi Wasalam:-

( قل آمنت بالله  ثم استقم )

“Sema nimemwamini Allah kisha nenda mwendo mzuri”.


Nikasema (yaani anaendelea huyo sahaba kumuuliza Salallahu Alayhi Wasalam) nijiepushe na kitu gani? Akafanya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam ishara kwa mkono wake kuonyesha ulimi wake. Na akasema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam :-

 ( و من يتكفل لي بما بين لحييه  ورجليه أتكفل له بالجنة )

 “Mwenye kunipa dhamana ya kilicho baina ya taya zake mbili (ulimi) na baina ya miguu yake miwili (utupu wake) nampa dhamana ya kupata Pepo.”


Na amesema Salallahu Alayhi Wasalam:-

(من وقي شر قبقبه وذبذبه ولقلقه فقد وقي الشر كله )

 “Anayeepushwa na shari ya tumbo lake na utupu wake na ulimi wake basi ameepushwa na shari yote.”


Na shari hizi tatu ndizo zinazowahilikisha watu wengi, twamuomba Allah Subhanahu Wataala atuepushe nazo Amin.


Amesema Anas bin Malik RA amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:-

لا يستقيم إيمان العبد حتى يستقيم قلبه ولا يستقيم قلبه حتى يستقيم لسانه ولا يدخل رجل الجنة لا يأمن جاره بوائقه )

 “Haiwi nzuri imani ya mja mpaka moyo wake uwe mzuri na hauwi mzuri moyo wake mpaka unyooke ulimi wake na haingii Al-Janna mtu ambaye hamuepushii jirani yake kero lake(maudhi yake).”


Hadithi iliyotolewa na Saeed bin Jubeir kutokana na Mtume Salallahu Alayhi Wasalam kasema:-

( إذا أصبح ابن آدم أصبحت الأعضاء كلها تذكر اللسان تقول : اتق الله فينا فإنك إن استقمت استقمنا وإن اعوججت اعوججنا )

 “Akiamka binaadamu viungo vyote vyaukumbusha ulimi vikauambia:- Mche Allah juu yetu kwani ukenda mwendo mzuri nasi tutakuwa na mwendo mzuri (tutanyooka) na ukenda mwendo mbaya nasi tutakwenda mwendo mbaya (tutapotea).”


Amesema Mtume Salallahu Alayhi Wasalam:

 (ألا أخبركم بأيسر العبادة وأهونها على البدن الصمت وحسن الخلق )

 “Je niwaambieni ibada iliyokuwa nyepesi zaidi juu ya mwili: kukaa kimya na tabia njema.”


Nabii Suleiman bin Dawood AS amesema:-

Ikiwa kuzungumza ni fedha basi kunyamaza ni dhahabu.


Nabii Eessa AS amesema:-

Ibada ni sehemu kumi, tisa miongoni mwa hizo ni katika kunyamaza na sehemu moja katika kuwakimbia watu (kuepukana nao).


Ameandika Omar bin Abdul Aziz:- “Amma baada: mwenye kukithirisha kukumbuka mauti anaridhika na kidogo Duniani na mwenye kuyahisabu mazungumzo yake kuwa ni miongoni mwa vitendo vyake basi huyafupisha mazungumzo yake isipokuwa (huzungumza) katika kile kinachomhusu”. Imetolewa na Bilal bin Al-Haarith kuwa Mtume Salallahu Alayhi Wasalam amesema:-

( إن الرجل ليتكلم بالكلمة من رضوان الله ما يظن أن تبلغ به ما بلغت فيكتب الله له بها رضوانه إلى يوم القيامة وإن الرجل ليتكلم بالكلمة من سخط الله ما يظن أن تبلغ به ما بلغت فيكتب الله عليه بها سخطه إلى يوم القيامة )

 “Hakika mtu huenda akasema neno katika yanayomridhisha Allah Subhanahu Wataala bila ya kufikiria kuwa (neno hilo) limefika hapo lilipofika (daraja kubwa).Basi Allah akamwandikia kwa hilo neno Radhi yake mpaka Siku ya Kiyama. Na hakika mtu huenda akasema neno katika (maneno) yanayomghadhibisha Allah Subhanahu Wataala bila ya kudhania kuwa (neno hilo) limefika hapo lilipofika (daraja ya chini). Basi Allah humwandikia kwa hilo neno ghadhabu yake mpaka Siku ya Kiyama.”


Yasemekana kuwa mtu fulani alimsifu mtu mwingine mbele ya Mtume Salallahu Alayhi Wasalam basi akasema Salallahu Alayhi Wasalam:-

( ويحك قطعت عنق صاحبك لو سمعها ما أفلح ) ثم قال : ( إن كان أحدكم لا بد مادحا أخاه فليقل أحسب فلانا ولا يزكي على الله أحداً حسيبه الله إن كان يرى أنه كذلك )

 “Ole wako umeikata shingo ya mwenzio kama angesikia (huko kumsifu kwako) basi asingefuzu” kisha akasema “Ikiwa mmoja hana budi ila kumsifu ndugu yake aseme namfikiria hivyo fulani na siwezi mimi kujua zaidi ya Allah Subhanahu Wataala kuwa mtu fulani mzuri, Allah ndiye anayemjua ikiwa kweli kama nilivyomfikiria mimi.”

No comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.